Habari za Punde

HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA KUHUSIANA NA MSWADA WA SHERIA YA KUFUTA SHERIA YA TUME YA UCHAGUZI NAM.9 YA 1992 NA KUTUNGA SHERIA YA KUANZISHA AFISI YA TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR, MAJUKUMU, UWEZO NA MAMBO MENGINE YANAYOHUSIANA NA HAYO.


Mheshimiwa Spika,
Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa utukufu kwa kutujaalia uhai na afya njema na kutuwezesha kufika hapa kujumuika kwa pamoja kwa lengo la kuendelea na majukumu yetu, pili naomba kuchukua fursa hii adhimu kukushukuru wewe mheshimiwa Spika kwa kunipa nafasi hii ya kusimama mbele ya Baraza lako tukufu kwa lengo la kuwasilisha maoni ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa kitaifa kuhusu mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Tume ya Uchaguzi Nam.9 ya 1992 na kutunga Sheria ya kuanzisha Afisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, majukumu, uwezo na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuwashukuru watendaji wa Ofisi ya Makamo wa pili wa Rais pamoja na watendaji wa Tume ya Uchaguzi kwa mashirikiano yao makubwa wanayoendelea kutupatia katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku hususan katika kuupitia na kuuchambua mswada huu adhimu. Sambamba na shukurani hizi napenda kutumia fursa hii nawapongeza sana wadau mbali mbali waliojitokeza katika Kamati yetu na kuwasilisha maoni yao kwa lengo la kuufanya mswada huu uwe bora zaidi, kwa kuthamini mchango wao ndio maana kila tunapokuwa na miswada huwa tunawaalika wadau ili waweze kutusaidia kuichambua miswada hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Mswada huu wa kuanzisha Afisi ya Tume ya Uchaguzi ni muhimu sana kwani umekuja kuweka misingi bora ambayo itakuwa inaenda sambamba na Katiba ya Zanzibar ambayo ndio iliyoanzisha Tume hii. Hivyo mswada huu umekuja kuanzisha uwepo wa Afisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambayo itaongozwa na Mkurugenzi na ambae atakuwa Katibu wa Tume ya Uchaguzi. Pia Mswada huu wa Sheria  umeanzisha Afisi za Tume za Wilaya ambazo zitakuwa kwa kila Wilaya ambazo zitakuwa jukumu la kuhakikisha uchaguzi au kura ya maoni zinaendeshwa katika misingi ya demokrasia na utawala bora.
Mheshimiwa Spika
Kamati yangu baada ya kuupitia mswada huu imependekeza baadhi ya marekebisho ambapo naamini waraka wa marekebisho hayo kila mjumbe ameshapatiwa nakala yake, hivyo ni vyema tukaupitia kwa makini ili tuweze kutoa mapendekezo zaidi kwa lengo la kuufanya mswada huu muhimu kuwa bora zaidi. Baadhi ya marekebisho ambayo Kamati imependekeza ni kuongezwa kwa kifungu kidogo cha (3) kitakachosomeka “Afisa Uchaguzi wa Wilaya atakuwa msimamizi wa jimbo au majimbo katika Wilaya yake katika kipindi cha Uchaguzi”.
Sababu ya mapendekezo haya ni kuhakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri wa uchaguzi katika majimbo ambao utafanywa na Afisa huyo wa Wilaya ambae atakua ni Afisa wa Tume, kinyume na utaratibu uliopo sasa ambapo msimamizi wa uchaguzi katika majimbo anakua sio mwajiriwa wa Tume hivyo anapotenda kosa lolote Tume haina mamlaka ya kumuwajibisha.
Mheshimiwa Spika
 Katika kifungu cha 26(2) Kamati imependekeza kuingizwa neno “zitawasilishwa” baina ya neno “fedha” na neno “kwa”. Sababu ya marekebisho hayo ni Sheria hii kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali baada ya kumaliza ukaguzi wa Hesabu za Tume kuwasilisha Ripoti yake kwa Waziri.
Mheshimiwa Spika,
Ni wazi kuwa utekelezaji wa Sheria hii hautakamilika bila ya kutungwa Kanuni zake, kwahivyo, Mhe. Waziri mara baada ya Baraza lako tukufu kupitisha Sheria hii na kusainiwa na Mhe. Rais, Kanuni za Sheria hii zitungwe haraka iwezekanavyo kwa ajili ya utekelezaji mzuri wa Sheria hii.
Mheshimiwa Spika,
Kazi ya kuupitia mswada huu tumeifanya kwa mashirikiano ya pamoja baina ya Wajumbe wa Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa kitaifa ambao ni Wajumbe wenye kupenda kujituma na kufanya kazi kwa bidii ya hali ya juu, Mheshimiwa Spika kwa ruhusa yako naomba niwatambue kwa kuwataja majina Wajumbe hao kama hivi ifuatavyo:-
1.    Mheshimiwa Omar Seif Abeid                                           Mwenyekiti
2.   Mheshimiwa Panya Ali Abdalla                                    M/Mwenyekiti
3.   Mheshimiwa Mtumwa Suleiman Makame                          Mjumbe
4.   Mheshimiwa Mussa Ali Mussa                                           Mjumbe
5.   Mheshimiwa Simai Mohammed Said                                 Mjumbe
6.   Mheshimiwa Amina Iddi Mabrouk                                    Mjumbe
7.   Mheshimiwa Hussein Ibrahim Makungu                             Mjumbe
8.   Ndg KassimTafana Kassim                                                 Katibu
9.   Ndg Maryam Rashid Ali                                                    Katibu.

Mheshimiwa Spika,
Mwisho kabisa nachukua nafasi kukushukuru tena Mheshimiwa Spika kwa kuniruhusu kuwasilisha maoni ya Kamati juu ya Mswada huu uliombele yetu lakini pia kuwashukuru Wajumbe wote wa Baraza lako tukufu kwa kunisikiliza kwa makini, hivyo nawaomba waupitie, waujadili, wakosoe na hatimae kuupitisha mswada huu muhimu kwa ajili ya kukuza Demokrasia na maendeleo ya katika nchi yetu na hatimae kuwa Sheria itakayotumika katika kuendesha shughuli za Tume ya Uchaguzi.
Mheshimiwa,
Kwa niaba yangu na kwa niaba ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa kitaifa naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.


Ahsante,
………
         Omar Seif Abeid,  
          Mwenyekiti,
Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa,
           Baraza la Wawakilishi,
            Zanzibar.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.