STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 28.03.2017

RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua juhudi katika
kutatua changamoto zote zilizopo kwenye sekta ya elimu hatua kwa hatua.
Dk. Shein aliyasema hayo leo
wakati alipokuwa na mkutano na Waalimu wa Skuli za Sekondari kwa skuli za Mikoa
yote mitatu ya Unguja, huko katika ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi.
Katika maelezo yake Dk.
Shein alieleza kuwa changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiikabili sekta ya
elimu tayari zimeshaanza kufanyiwa kazi na Serikali anayoiongoza hatua ambayo
ni uthibitisho kwamba Serikali ina dhamira ya dhati katika kuimarisha sekta ya
elimu kwa kuzingatia umuhimu kwa maendeleo.
Alisema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutatua changamoto hizo kwa mujibu wa fedha
zilizopo Serikalini ili kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu
2016/2020, Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020, Mpango wa MKUZA III pamoja na mipango mengine ya maendeleo ya
Kitaifa na Kimataifa.
Dk. Shein alisisitiza kuwa
Serikali itaweka kipaumbele maalum katika kuimarisha mazingira ya kufanya kazi
walimu ili yawe bora zaidi ambapo itahakikisha muundo wa utumishi wa Wizara ya
Elimu unafanyiwa kazi ili kila mfanyakazi wakiwemo walimu wapate stahiki zao
kwa mujibu wa sifa za kitaaluma, uzoefu na dhamana zao.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza
haja ya kuimarisha uhusiano baina ya walimu na wazazi ili kuongeza ufanisi
katika ufaulu wa wanafunzi hasa ikizingatiwa kuwa hivi sasa katika skuli nyingi
Kamati za Wazee zimepoteza nguvu na hivyo kushindwa kuwaunganisha wazazi na
walimu.
Hivyo, Dk. Shein alitoa
wito kwa uongozi wa skuli kuziimarisha Kamati za skuli na hata kuwa na siku za
wazazi kwa lengo la kuimarisha uhusiano baina ya wazazi na uongozi wa skuli.
Pia, Dk. Shein alisisitiza
haja kwa walimu kuwa na mbinu bora za kufundishia na kuwasaidia wanafunzi ikiwa
ni pamoja na walimu kujiandaa kabla ya kufundisha na vile vile wawe tayari
kujiendeleza kitaaluma na kujifunza kwa wengine wanaofanya vizuri.
Akisisitiza suala la
ukaguzi wa skuli na walimu.
Dk. Shein alisema kuwa kwa
bahati mbaya katika baadhi ya skuli wapo walimu wachache wanaofanya kazi kwa
kuripua ambapo baadhi yao hawakamilishi silibasi na wengine husaza baadhi ya
mada na kutilia mkazo masomo ya ziada.
Vile vile, Dk. Shein
alisema kuwa wapo baadhi ya walimu wanaweka mbele zaidi miradi yao wakati wa
kazi na wengine hutumia muda wa kazin kwa porojo za kisiasa na mambo mengine
kinyume na wajibu wao wa kusomesha na kufanya hivyo wanakuwa hawasaidii na ni
vyema wakachagua kusomesha ama kufanya siasa.
Dk. Shein aliitaka Idara
ya Ukaguzi wa Elimu kuongeza kasi za ukaguzi katika skuli za Serikali na za
binafsi ili malengo ya kutoa elimu iliyo bora yaweze kufikiwa kwa ufanisi
mkubwa pia, skuli binafsi kuzingatia sheria za utumishi ikiwa ni pamoja
kuwapatia mikataba ya kazi watumishi, haki za likizo na stahiki zao pamoja na
kuwaajiri walimu wenye sifa.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alisisitiza haja ya kuweka
mazingira bora katika skuli kwa lengo la kupata matokeo mazuri sambamba na
kusisitiza haja kwa walimu kuimarisha michezo katika skuli zao kwani Serikali
imeanzisha Idara ya Michezo na Utamaduni kwenye Wizara ya Elimu kwa malengo
maalum.
Sambamba na hayo Dk. Shein
alitoa wito kwa Wizara ya Elimu kuandaa utaratibu wa kuwazawadia walimu na
skuli zinazofanya vizuri zaidi.
Nae Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Dk.
Shein kwa uwamuzi wake huo wa kuzungumza na walimu wa skuli za Sekondari ambao
watakuwa mabalozi kwa wenzao.
Mapema Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Khadija Bakari Juma kwa
niaba ya walimu na Wizara alitumia fursa hiyo kuungana na wananchi kumpongeza
Dk. Shein kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake katika kipindi cha Pili na
kueleza mafanikio yaliopatikana katika sekta hiyo ya elimu ikiwa ni pamoja na
ongezeko la skuli, madarasa, vitabu, vifaa vyenginevyo.
Katibu Mkuu huyo pia,
alieleza kuwa Wizara hiyo ina kauli mbiu ya “Elimu Bora Kwanza” ikiwa ni
msisitizo wa ubora wa elimu kwa wananfunzi wote na kueleza kuwa tayari Serikali
imeshakamilisha ujenzi wa Skuli ya Msingi ya Mgonjoni, Skuli ya Sekondari ya
Mohammed Juma Pindua ya Mkanyageni na Skuli ya Kwarara ambayo ina kituo cha
kurushia matangazo ya redio na televisheni.
Aidha, alisema kuwa
Serikali imeshatangaza zabuni za ujenzi wa skuli tisa za ghorofa zikiwemo skuli
tano kwa upande wa Unguja na nne kwa upande wa Pemba huku akieleza kuwa mchakato wa kumpata
mkandarasi mwengine wa kuendeleza ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Kibuteni
umekamilika na mkataba wa ujenzi unatarajiwa kusainiwa hivi karibuni.
Pamoja na hayo, Bi Khadija
alieleza mafanikio zaidi yaliopatikana katika kiwango cha ufaulu katika
mitihani ya taifa katika ngazi ya Kidato cha Pili, Kidato ca Nnne na Kidato cha
Sita pamoja na ongezeko la wanafunzi waliopatiwa mikopo kupitia Bodi ya Mikopo
ya Elimu ya Juu Zanzibar pamoja na mambo mengineyo katika sekta hiyo ya elimu.
Nao walimu hao walipata
nafasi za kutoa risala zao kwa kila mkoa
ndani ya mikoa mitatu ya Unguja ambao walieleza mafanikio yaliopatikana katika
sekta hiyo ya elimu pamoja na kueleza changamoto zinazowakabili.
Walimu hao pia, walipata
fursa ya kutoa michago yao, maoni na ushauri kwa Dk. Shein kwa lengo moja la
kuimarisha sekta elimu hapa nchini ambapo kwa upande wa walimu wa skuli za
binafsi nao walisisitiza haja ya kuwepo mashirikiano ya pamoja.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment