Habari za Punde

Kampuni ya Uhandisi Garware ya India yaonesha nia ya kutaka kujenga ukumbi mpya wa kisasa wa mikutano Zanzibar

 Mkurugenzi Miradi wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Miundombinu ya Ujenzi ya Garware ya Nchini India  Bwana Deepak Menghnani kati kati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Hoteli ya Kimataifa ya Eros Mjini New Delhi India.

Kulia ni Balozi Seif na wa kwanza kutoka Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya Kampuni ya Garware Bwana Jatindery V. Sehgal.
 Mkurugenzi wa Miradi wa Kampuni ya Garware Bwana Deepak Mnghnani Kushoto akifafanua jambo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyekaa kati kati na wa kwanza kulia ni Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya Kampuni ya Gaware Bwana Jatindery V. Sehgal.

Balozi Seif Ali Iddi wa Pili kutoka Kulia akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Kampuni ya Garware mara baada ya kumaliza mazungumzo yao katika Hoteli ya Kimataifa ya Eros Mjini New Delhi India.

Wa kwanza kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Miradi wa Kampuni ya Garware Bwana Deepak Mnghnani na kulia ya Balozi Seif ni Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya Kampuni ya Gaware Bwana Jatindery V. Sehgal pamoja na
Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini India Balozi Mohamed Hija Mohamed.

Picha na –OMPR – ZNZ


Na Othman Khamis, India


Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa  miundombinu ya Ujenzi ya Garware yenye Makao Makuu yake Mjini Bumbay Nchini India imeonyesha nia yake ya kutaka kujenga Ukumbi Mpya wa Kisasa wa Kimataifa wa Mikutano Zanzibar endapo itapata fursa ya kufanya kazi hiyo.



Uwamuzi huo umekuja kufuatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na mpango wa Kutaka kujenga Ukumbi wenye hadhi hiyo katika azma yake ya kuimarisha Sekta ya Utalii inayoonekana kuimarika na kuleta ufanisi
mkubwa.



Mkurugenzi Miradi wa Kamuni Garware  Bwana Deepak Menghnani alithibitisha hilo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mwishoni mwa ziara ya Wiki Moja ya Ujumbe wa Zanzibar hapo katika Hoteli ya Kimataifa ya Eros Mjini New Delhi India.



Bwana Deepak Menghnani alimthibitishia Balozi Seif  kwamba Wahandisi wa Kampuni ya Garware iliyoanzishwa karibu miaka sita iliyopita wana uwezo wa Kujenga Jengo la Mikutano katika kipindi kisichozidi miaka Mitatu kwa mujibu wa uwezo wa mahitaji ya muhusika.


 
Alisema teknolojia rahisi inayotumika katika Kampuni hiyo imewawezesha Wataalamu na Wahandisi wake kuendesha ujenzi wa Mjengo tofauti ikiwemo Hospitali, Skuli, Ofisi za Serikali na hata Taasisi Binafsi pamoja na
nyumba za Makaazi kwa bei inayomuwezesha mtu wa kawaida kumudu kununua.


 
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa  miundombinu ya Ujenzi ya Garware alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Taasisi hiyo ya ujenzi imekuwa ikishirikiana na Wahandisi waliobobea kutoka Nchini Misri ili kuiwezesha kuwa na uhimili wa Kimataifa.



Bwana Deepak Menghnani alisema Garware tayari imeshatoa huduma za ujenzi katika Mataifa ya Bukinafaso,Sri Lanka na Dubai ndani ya kipindi cha miaka Minane tokea kuanzishwa kwake.



Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuuandalikia barua ya mualiko Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni hiyo katika muda mfupi ujao ili kujionea mazingira ya Zanzibar na kuona hatua gani zinastahiki kuchukuliwa katika mwanzao wa kuelekea kwenye mpango huo wa ujenzi wa Ukumbi wa Kimataifa.



Balozi Seif alisema Zanzibar imeshafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika uimarishaji wa Sekta ya Utalii lakini kinachokosekana kwa wakati huu ni uwepo wa Ukumbi wa Kimataifa unaotoa fursa kwa Wageni na hata Nchi
rafiki kuelekeza nguvu zao za kufanya makongamano, Mikutano na hata Vikao vya Kimataifa.



“ Zipo kumbi za Mikutano zinazotumika katika baadhi ya Mahoteli Mjini na sehemu za Vijijini Zanzibar lakini hazikidhi mahitaji halisi kutokana na udogo wake ”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.



Balozi Seif alisema ipo mikutano na baadhi ya semina za Kimataifa zinazopangwa kufanyika Visiwani Zanzibar lakini wajumbe wa Mikutano hiyo hulazimika kuishi mbali na maeneo yao ya mikutano jambo ambalo huleta usumbufu wa kujipangia mambo yao mengine  binafsi.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemaliza ziara yake Nchini India na sasa amewasili Dubai kwa Mapumziko mafupi ya siku mbili na baadae atarejea Nchini Tanzania kuendelea na majukumu
yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.