Habari za Punde

Majaliwa: Tanzania ina utashi wa dhati kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli inautashi wa dhati wa kuboresha mazingira ya uwekezani na biashara nchini kwa kuondoa rushwa na urasimu katika sekta ya umma, hivyo amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Mauritius kuja nchini.

Amesema Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa kubadili mifumo yake ya kisheria, kitaasisi na kifedha ili kuhakikisha wawekezaji wanahudumiwa ipasavyo na kupewa umuhimu wanaostahili kwani ni wadau muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu amesema hayo jana (Alhamisi, Machi 23,2017) wakati akifungua kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Mauritius lilifanyika katika Hotel ya Labourdonnaise mjini Port Louisnchini Mauritius. Kongamano hilo liliandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Alisema Tanzania ina uchumi imara unaofuata misingi ya soko huria, ambapo mwekezaji ana uhuru wa kufanya biashara bila ya kuingiliwa na Serikali, hivyo sekta binafsi imepewa kipaumbele katika shughuli za kiuchumi na kibiashara nchini.
“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli nawakaribisha kwa mikono miwili kuja na kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda na utalii na kutembelea vivutio vya utalii na kupata burudani ya aina yake na kwa wafanyabiashara Tanzania ni mahali pazuri kwa kuwekeza,” alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.