Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Aendelea na Ziara Yake Nchini India

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi   na ujumbe wake wakitembezwa chumba cha wagonjwa Mahututi { ICU }katika Hospitali ya Kimataifa ya Miot iliyopo Jimbo la Chennai akiwa ziarani Nchini India.
Balozi Seif akipata maelezo ya Kitaamu ndani ya Chumba cha Maaba kwenye Hospitali ya Miot Nchini India. Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar bibi Asha Ali Abdulla na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Waziri asiye na Wizara Maalum Dr. Sira Ubwa Mamboya.
Balozi Seif akimfariji Bwana Ahmed Murdhed wa Chake chake Kisiwani Pemba aliyelazwa kwa kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Miot iliyopo katika Jimnbo la Chennai Nchini India.
Bibi Faida Tajir Ali Mkaazi wa Kisiwandui Mjini Zanzibar akielezea faraja yake kufuatia ujio wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Mabara la Mapinduzi Dr. Sira Ubwa Mamboya wakimpa pole kwenye Hospitali ya Miot India.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Sheha wa Shehia ya Maungani Bwana  Ali Kibwana Juma aliyelazwa kwenye Hospitali ya Miot akipatiwa matibabu.
Mzazi wa Mtoto Hemed Hafidh aliyelazwa Hospitali ya Miot India Baba Hafidh Hamid Suleiman akiwasilisha salamu za shukrani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Balozi Seif kwa jinsi SMZ inavyowajali wananchi wake kwa kuwagharamia huduma za matibabu Nchini India.
Mmiliki wa Hospitali ya Kimataifa ya Miot Jimboni Chennai Nchini India Dr. V.A. Mahandazaz akiagana na Makamu wa Pili wa Rais wa Znzibar Balozi Seif mara baada ya kula pamoja chakula cha mchana Hospitalini pake Miot
.(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na Othman Khamis OMPR India.

Uongozi wa Hospitali ya Kimataifa ya Miot katika Jimbo la Chennai Nchini India umeahidi kuendelea kushirikiana na Zanzibar  katika kuona Sekta ya Afya inatengamaa ili huduma zinazotolewa kwenye Hospitali pamoja na Vituo vyote vya  Afya zinawafikia Wananchi  wote wa Visiwa wa Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa na Mmiliki wa Hospitali hiyo Dr. P.V.A Mahandazaz wakati akizungumza na Ujumbe wa Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi uliofika Hospitalini hapo kuwakaguwa Wagonjwa wa Kitanzania wanaogharamiwa  kimatibabu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dr.Mahandazaz  alisema mkataba uliotiwa saini hivi karibuni kati ya Uongozi wa Wizara ya Afya ya Zanzibar na Uongozi wa Hospitali hiyo ya Miot ni mwanzo wa safari ndefu ya matumaini inayoashiria ushirikiano mwema utakaoleta faraja kwa Wagonjwa wote Kitanzania waopangiwa kupata huduma za Afya kwenye Taasisi hiyo.

Alisema yapo mambo mengi ambayo Miot imekusudia kuyatekeleza katika kipindi kifupi kijacho likiwemo suala la kupatiwa mafunzo kwa Madaktari na baadhi ya wataalamu wa Afya wa Zanzibar lengo likiwa kuwajengea uwezo wa kutoa huduma za Afya zinazokusudiwa kupatikana katika kiwango cha Kimataifa.

Dr. Mahandazaz alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ujumbe wake uliomo Nchini India kwa ziara ya Wiki moja kwamba Hospitali hiyo itaendelea kuwahudumia Wagonjwa wa Kitanzania wakati wowote wanapoamuliwa kupelekwa katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kupata Huduma za Afya.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Asha Ali Abdulla ameushuruku Uongozi na Madaktari wa Hospitali ya Miot Jimboni Chennai kwa jitihada wanazochukuwa za kuwapatia huduma za Afya Wagonjwa wa Kitanzania wanaofikishwa kwenye Hospitali hiyo.

Bibi Asha alisema inaleta faraja na kuona zaidi ya Wagonjwa 171 wa Zanzibar tayari wameshapatiwa huduma za Afya zikiwemo operesheni za maradhi mbali mbali baina ya mwaka 2012 hadi 2015.

Alisema katika kupunguza idadi ya wagonjwa na gharama zake za kupelekwa nje ya Nchi Wananchi wanaopatwa na matatizo makubwa ya Kiafya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha huduma za Afya katika hatua ya kuwa na Hospitali za Rufaa.

Hata Hivyo Bibi Asha alisema Zanzibar inahitaji kuwa na Madaktari Wataalamu zaidi ambapo Hospitali ya Miot inaweza kutoa mchango wake mkubwa wa Taaluma itakayokwenda sambamba na  upatikanaji wa huduma za Afya katika Hospitali hizo za Rufaa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  na Ujumbe wake alipata wasaa wa kutembelea Vitengo mbali mbali vya Hospitali hiyo ya Miot ili kujionea uwajibikaji wa watendaji wake na baadae kukagua baadhi ya wagonjwa wa Kitanzania waliolazwa kwa ajili ya kupata huduma za afya ziliwemo operesheni.

Akielezea faraja wanayoipata kutokana na huduma zinazotolewa kwenye Hospitali hiyo Mzazi wa Mgonjwa Hemed Hafidh anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka miwili Baba Hafidh Hemed Suleiman kwa niaba ya wagonjwa wa Kitanzania ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa moyo thabiti  inayoonyesha wa kugharamia Matibabu ya Wananchi wake.

Baba Hafidh alimthibitishia Balozi Seif  na Ujumbe wake kwamba Wagonjwa wa Zanzibar hadi sasa ndio pekee wanaogharamiwa  na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huduma za Matibabu wakati wanapopekekwa katika Hospitali hiyo.

Alisema Wapo Wagonjwa kadhaa wanaotoka katika baadhi ya Mataifa ya Afrika kama Madagaska, Somalia, Kenya, Ethiopia, Sudan na hata  Uganda kwa ajili ya kupatiwa  matibabu Hospitalini hapo lakini wamekuwa wakijigharamia wenyewe au familia zinazowapeleka.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake atamalizia ziara yake ya Siku Tano katika Mji wa New Delhi kwa kutembelea Kiwanda cha Matrekta cha Mahindra, kukutana kwa mazungumzo na Wafanyabiashara pamoja na Wawekezaji wa India.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.