Kutokana na kile kinachoonekana kua ni ufaulu mbovu wa wanafunzi nchini katika masomo ya lugha ya kiingereza na hesabati hatimae taasisi ya Milele Zanzibar Foundation leo imetambulisha rasmi vitabu 200,000 vya kiingereza kwa wanafunzi wa msingi hapa visiwani,lengo ni kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi atakaefanya vibaya katika masomo hayo.
Hayo yameelezwa leo huko katika ukumbi wa hoteli ya Misali sun set beach Wesha mkoa wa kusini Pemba ambapo taasisi ya Milele Zanzibar Foundation iliwakutanisha walimu wa somo la kiingereza kisiwani Pemba na wadau wengine wa sekta ya elimu katika mkutano ulioambatana na mafunzo kwa lengo la kuvitambulisha vitabu hivyo pamoja na kutoa mwongozo wa namna ya kuwafundisha wanafunzi.
Akiufungua mkutano wa kuvitambulisha vitabu hivyo pamoja na kutoa mwongozo kwa walimu Bi Safia Ali Rijali mkurugenzi wa elimu ya msingi (Director Pre-Primary and Primary Education) amesema kua taasisi ya Milele Zanzibar Foundation imefanya jambo moja kubwa linalofaa kuigwa na taasisi nyengine.
Amesema hali ya ufaulu kwa wanafunzi nchini hairidhishi na kwamba uwepo wa vitabu hivyo utasaidia pakubwa kuinua sekta ya elimu nchini.
"mwaka jana wanafunzi 16000 wa darasa la nne walifeli na 4000 hawakufanya mitihani kwa sababu tofauti, hii si hali nzuri hata kidgo" alisema Rijali.
Rijali amesema kutokana na haja kubwa ya uwepo wa vitabu hivyo nchini kila siku alikua akiandamwa na wadau kwa maswali ya kutaka kujua vitabu hivyo ni lini vitakuja nchini, amesema hivi sasa ameshapata jibu muwafaka huku akisema kua mambo katika sekta ya elimu yanaelekea pazuri hususan katika lugha ya kiingereza.
Awali akimkaribisha Bi Safia Mkuu wa Programu kutoka Milele Zanzibar Foundation Bi Khadija A Sharif amesema kua lengo la kuleta vitabu hivyo ni kutaka kukuza uwelewa wa wanafunzi katika lugha ya kiingereza.
Bi Khadija amewataka walimu waliyohudhuria katika mkutano huo kua makini na miongozo waliyopatiwa ili kuwafundisha wanafunzi wao kiufasaha zaidi hatimae lengo lifikiwe.
Mratib wa kituo cha elimu Wingwi (TC Co-rdinator) mwalimu Shoka Hamad Abeid ambae ni mshiriki katika mafunzo hayo amesema kua, kilichofanywa na taasisi ya Milele ni ukombozi katika sekta ya elimu kwani kila kitu katika mafanikio kunahitajika nyenzo na uwepo wa vitabu hivyo ni nyenzo kubwa itakayowawezesha kufanya vizuri.
Kwa upande wake mwalimu Rehema Ali Said wa skuli ya Amini Islamic Primary ameonyesha kufurahishwa sana juu ya utambulisho wa vitabu hivyo huku akisema kua ana matumaini makubwa ya kufanya vizuri wanafunzi katika lugha ya kiingereza tofauti na hali ilivyokua.
Amefahamisha kua, vitabu hivyo ni tofauti na vya awali kwakua hivi vya sasa kiurahisi zaidi vitamuwezesha mwanafunzi kuweza kutamka maneno ya kiingereza kwa wepesi na kwa kasi zaidi hali ambayo itapelekea uchapu katika kuzungumza.
Katika mafunzo hayo walimu wamepatiwa mbinu mbalimbali zitakazo mfanya mwanafunzi kufahamu kwa kwaharaka kupitia michoro na maelezo elekezi yaliyomo katika vitabu hivyo vinavyotakiwa kutumika kuanzia sasa katika skuli zote za unguja na pemba.
Milele Zanzibar Foundation ni taasisi iliyojikita zaidi katika kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo afya, elimu na fursa za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya kijamii kupitia miradi ya maendeleo yenye ukamilifu na endelevu.
No comments:
Post a Comment