STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.03.2017
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezindua mashindano
ya Mpira wa miguu ‘Majimbo Cup’ na kuwataka vijana wanaoshiriki mashindano hayo
kucheza kwa maadili na nidhamu kama kilivyo chama chao cha CCM.
Uzinduzi huo umefanyika katika uwanja wa
Amaan mjini Zanzibar ikiwa ni maadhimisho ya mwaka mmoja tokea kuapishwa kwa Dk.
Shein kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kufuatia
ushindi wa kishindo alioupata katika uchaguzi mkuu uliopita na kuweza kuendelea
katika kipindi cha pili cha uongozi wake ambapo timu zilizofungua dimba ya
mashindano hayo ni Mfenesini na Mpendae
Akitoa salamu zake katika uzinduzi huo, Dk.
Shein alitoa pongezi kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa mchango wao
mkubwa waliotoa kwa Majimbo yao kwa lengo la kuendeleza mashindano hayo.
Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa wale wote
waliochangia na kusimamia mashindano hayo ikiwemo Kamati maalum iliyoundwa
kuendesha mashindano hayo, viongozi, Mwenyekiti wa Kamati pamoja na Mwakilishi
wa Uzini Mohammed Raza kwa kuyafadhili mashindano hayo.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa
pongezi kwa Wawakilishi wa Majimbo yote ya Pemba na wale wa viti maalum kwa
mchango wao wa Tsh. Milioni 12 kwa ajili ya mashindano kama hayo
yatakayofanyika katika majimbo kisiwani humo.
Dk. Shein ambaye pia, ni Makamu Mwenyekiti
wa CCM Zanzibar alisisitiza kuwa mashindano hayo pia ni mwendelezo wa
maadhimisho ya miaka 40 tokea kuzaliwa kwa CCM.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza imani
yake kubwa kuwa mashindano hayo yataenda vizuri kutokana na mazingira mazuri ya
uwanja wa Amaan unaochezewa mashindano hayo pamoja na kukamilika vyema kwa
maandalizi yake.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Abdalla Juma Mabodi alitoa pongezi kwa niaba ya wanaCCM na wale wote wapenda
amani kwa Rais Dk. Shein kwa kutimiza mwaka mmoja tokea kuchaguliwa tena na
wananchi kuiongoza Zanzibar katika uchaguzi uliopita.
Mabodi alisisitiza kuwa michezo ni afya,
amani, upendo na kustahamiliana hivyo, alieleza haja kwa timu zote kucheza
vyema mashindano hayo ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Mapema Mwenyekiti wa mashindano hayo ambaye
pia, ni Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Khamis alitoa
pongezi kwa Kamati ya mashindano hayo ambayo itasimamia mashindano hayo hadi
tamati ya mashindano.
Hadi mwisho wa mtanange huo wa uzinduzi wa
mashindano hayo kati ya Mfenesini na Mpendae, timu ya Mfenesini ilitoka kidedea
kwa kushinda magoli mawili katika kipindi cha pili cha mchezo huo magoli ambayo
yote yalifungwa na mshambuliaji machachari Ali Seif Bausi na Mpendae haikupata
kitu.
Viongozi mbali mbali, wa chama na Serikali,
wanaCCM na wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar walihudhuria katika mashindano
hayo ambapo mapema Wanamichezo wakiongozwa na Brass Band waliingia uwanjani hapo
na kupita mbele ya Mgeni Rasmin Dk. Ali Mohamed Shein.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment