STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 20.03.2017

RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Idara ya
Uhamiaji Tanzania kwa kuendelea kupata mafanikio na kusisitiza haja ya mafunzo
kwa wafanyakazi wa Idara hiyo ili iendelee kufanya kazi kwa ufanisi zaidi hapa
nchini.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Kamishna Jenerali mpya wa Uhamiaji
Tanzania Dk. Anna Peter Makakala, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya
kujitambulisha rasmi kwa Rais.
Katika maelezo yake,
Dk. Shein alimueleza Kamishna Jenerali Makakala kuwa Idara ya Uhamiaji Tanzania ni Idara kongwe
ambayo imeweza kupata mafanikio makubwa kutokana na uzoefu mkubwa uliopo kwenye
Idara hiyo, hivyo suala la mafunzo linahitajika ili Idara hiyo iendelee kufanya
kazi kwa wakati uliopo.
Aidha, Dk. Shein
alimueleza kiongozi huyo kuwa licha ya mafanikio yaliopo pia zipo changamoto
ambazo kwa mashirikiano ya pamoja zinaweza kutatuliwa huku akipongeza juhudi za
Idara hiyo za kujenga Ofisi mpya za Makao yake makuu kwa upande wa Zanzibar.
Dk. Shein aliongeza
kuwa ipo haja kwa Idara hiyo kuwandaa wafanyakazi wake kwa kuwapatia mafunzo yanayoendana
na kazi zao kwani kazi hiyo inahitaji mafunzo na utaalamu unaoenda sambamba na
kazi hiyo hasa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia duniani ambapo Idara
hiyo inapaswa kwenda sambamba na hali hiyo.
Alisisitiza umuhimu wa
kuwasikiliza na kuwawezesha wafanyakazi ili waendelee kuwa na ari ya kufanya
kazi zao kwa ustadi na kuweza kupata mafanikio zaidi ha ikizingatiwa kuwa
sayansi na teknolojia imezidi kukua duniani.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alimueleza Mkuu huyo wa Uhamiaji kuwa kuna umuhimu wa kuendeleza
mashirikiano na vikosi vyengine vya ulinzi na usalama hapa nchini ili Idara
hiyo iweze kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliendelea kutoa pongezi kwa Idara
hiyo kwa kuendelea kufanya kazi vizuri na kwa mashirikiano kati ya wafanyakazi na viongozi wakuu wa Idara hiyo waliopo
Zanzibar na wale waliopo Tanzania Bara.
Nae Kamishna Jenerali
wa Uhamiaji, Tanzania Dk. Anna Peter Makakala alitoa shukrani kwa Dk. Shein kwa
kuendelea kuiunga mkono Idara hiyo na kumueleza kuwa licha ya kazi zake inazofanya
Idara hiyo ya Uhamiaji pia, ina kazi ya kukusanya mapato.
Kamishna Makakala
alieleza kuwa azma ya Idara hiyo ni kuelekea kwenye teknolojia zaidi na juhudi
za makusudi zimekuwa zikiendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha hilo
linafanikiwa.
Alieleza kuwa licha ya
baadhi ya changamoto zilizopo katika Idara hiyo ambazo zinaendelea kupatiwa
ufumbuzi suala la mafunzo kwa wafanyakazi wake limepewa kipaumbele kwa kiasi
kikubwa.
Aliongeza kuwa Idara
ya Uhamiaji ni Idara ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo itaendelea
kufanya kazi zake kwa mashirikiano ya pamoja katika maeneo yote ya ndani ya
Jamhuri hiyo ya Muungano wa Tanzania yaliopo Tanzania Bara na Zanzibar.
Pia, Kamishna Jenerali
wa Uhamiaji huyo, alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Idara hiyo itaendelea kufanya kazi kwa
mashirikiano na vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama nchini Tanzania kwa kutambua
umuhimu huo katika kufikia lengo walilojiwekea katika utendaji wao wa kazi.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment