STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
18.03.2017

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kufanyika kwa mashindano ya
michezo ya Majeshi mwaka huu ni dalili njema ya kuwepo kwa mikakati katika
vikosi vya ulinzi na usalama ya kuunga mkono jitihada za Serikali zote mbili
katika kuimarisha sekta ya michezo ili kurudisha hadhi ya Tanzania katika
medani za michezo Kimataifa.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo katika ufunguzi wa Michezo ya 17 ya Majeshi iliyoandaliwa na Baraza la
Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMATA) mwaka 2017, ufunguzi uliofanyika huko
katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk.
Shein alieleza kuwa Watanzania wanatamani sana kuwapata akina Filbert Bayi,
Suleiman Nyambui na Juma Ikangaa wengine kutoka katika vikosi vya ulinzi na
usalama au kutoka timu za utraiani
zitakazotoa wachezaji watakaoweza kuwakilisha katika michezo ya Kimataifa.
“Tunaamini kuwa
wachezaji kama hawa tunao ila kinachokosekana ni jitihada za kuwaibua na
kuwaendeleza zaidi jitihada ambazo ndizo zinazohitajika hivi sasa’,alisema Dk.
Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema
kuwa pamoja na kupata fursa ya burudani katika mashindano hayo, vile vile
kupitia michezo hiyo, wanamichezo wanaoshiriki mashindano hayo hupata kujuana
na kupata kujifunza kutoka kwa wenzao.
Aliongeza kuwa fursa
hiyo huchangia kuongeza idadi ya mashindano ya michezo ya ndani na kupanua
zaidi nafasi ya wanamichezo kuweza kujinoa na kujiweka tayari kwa michezo
mengine ambayo timu za majeshi huwa zinashiriki.
Dk. Shein alisema kuwa
mashindano hayo pia, yanatoa nafasi nzuri kwa maafisa na wapiganaji wa vyombo
vya ulinzi na usalama vya Tanzania na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kukuza ushirikiano zaidi baina yao katika masuala mbali mbali.
Pamoja na Hayo, Dk.
Shein alitoa pongezi maalum kwa viongozi wa Baraza la Michezo ya Majeshi
Tanzania (BAMMATA) kwa kuirudisha tena michezo hiyo mwaka huu kwani mashindano
hayo kwa mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2004.
Alisisitiza kuwa ni
dhahiri kwamba kusita kwa mashindano hayo kwa kipindi cha miaka 13 kulileta
athari, hivyo baada ya kuzibaini athari hizo jitihada zimefanyika na
imewezekana kuyaendeleza tena mashindano hayo.
Dk. Shein alieleza kuwa
hatua ya kuiendeleza tena michezo hiyo baada ya miaka 13 ya kusita kwake ni
hatua muhimu ya kuendeleza sekta ya michezo katika Jamhuri ya Muugano wa
Tanzania na ndani ya vikosi hivyo ambavyo vimekuwa vikitoa mchango muhimu kwa
maendeleo ya michezo mbali mbali.
Kwa maelezo ya Dk. Shein
michezo ina umuhimu mkubwa katika jamii hasa katika kuleta amani, upendo, furaha,
mshikamano pamoja na afya kwa wanamichezo ambapo pia, kwa hivi sasa michezo ni
chachu ya ajira kwa vijana.
Aliongeza kuwa kwa
upande wa vyombo vya ulinzi na usalama michezo ina mchango muhimu katika
kuimarisha afya, nidhamu na kwa wapiganaji ni kuwa tayari wakati wowote katika
kuilinda nchi na kuifanya Tanzania kuendeleza sifa ya kuwa na wapiganaji imara.
Mapema Mwenyekiti wa BAMMATA
Bregedia Jenerali Martin Kemwaga ilitumia fursa hiyo kueleza historia ya Baraza
hilo tokea kuanzishwa kwake, mafanikio yaliopatikana pamoja na changamoto zilizopo.
Nae Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo alieleza miongoni mwa
malengo ya mashindano hayo kwa vikosi hivyo na kuahidi michezo hiyo kuendeleza
vuguvugu lake kama ilivyokuwa siku za nyuma ambapo timu za majeshi zilitoa
wanamichezo bora huku akitumia fursa hiyo kuipongeza Zanzibar kwa kupata
uwanachama wa CAF.
Mashindano hayo
yanatarajiwa kufungwa tarehe 25 mwezi huu ambapo jumla ya michezo mitano
itashindaniwa ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete kwa wanawake, mpira wa
kikapu kwa wanawake na wanaume, mpira wa mikono kwa wanawake na wanaume na
mpira wa wavu kwa wanawake na wanaume ambapo kauli mbiu ya mashindano hayo ni “
Michezo ni Kazi na Mshikamano”.
Katika ufunguzi wa
mashindano hayo nyimbo maalum kwa ziliimbwa na vikosi hivyo pamoja na viapo kwa
wachezaji pamoja na waamuzi huku timu ya mpira wa miguu ya vikosi vya SMZ
ikafungua dimba na timu ya Uhamiaji hapo hapo katika uwanja huo wa Amaan mjini
Zanzibar ambapo Dk. Shein alizikagua timu hizo na kushiriki pamoja na viongozi wengine,
wananchi na vikosi shiriki kuangalia pambano hilo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment