Na.Haji Nassor PEMBA
WANACHAMA 135 wa ushirika wa ‘tufaane saving and credit’
wa wizara ya ardhi, makaazi, maji na nishati Pemba, wameshakopeshwa mikopo
yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 239, hadi kufikia mwezi disemba
mwaka 2014 kwa wanachama wake.
Kati ya fedha hizo shilingi milioni 122.5 tayari zimesharejeshwa
na wakopaji, wakati shilingi milioni 150.3 bado ziko mikononi mwa wanachama,
wakiendelea kurejesha taratibu.
Akisoma risala ya ushirika huo, kwenye mkutano mkuu uliofanyika
ofisi ya mamlaka ya maji ‘ZAWA’ Machomane Chakechake, Katibu Khamis Hamad
Hassan, alisema hayo ni miongoni mwa matunda ya uhsirika wao.
Alieleza kuwa, pia ushirika umefanikiwa kukopesha shilingi zaidi
ya milioni 6.5 kama mikopo ya dharura na shilingi milioni 143.8 mikopo ya
kawaida miongoni mwa wanachama.
Katib huyo alifafanua kuwa, iwapo wanachama waliochukua mikopo
hiyo wameekeza kwenye mitaji mbali mbali, itakuwa wameshapiga hatua ya
kimaendeleo.
“Ushirika wetu umefikia pahala pazuri, maana wapo wanachama 135
hadi kufikia mwaka juzi, wameshachukua mikopo, na ndio miongoni mwa malengo
yetu’’,alifafanua.
Akifungua mkutano huo Katibu tawala wilaya ya Chakechake Abdalla
Rashid Abdalla, aliwashauri wanachama hao kuwa makini wanapochukua mikopo, ili
faida ya kukopa kwao ionekane.
Alieleza kuwa, wapo wanachama katika vyama vyengine vya ushirika,
wamekuwa wakikopa fedha na kisha kujinunulia chakula badala kuanzisha mitaji
yenye thamani.
Katika hatua nyengine, Katibu huyo Tawala aliwasisitiza wanachama
wa ushirika huo, kuendelea kutoa michango na ada zao, wakiamini kwa njia hiyo
inaweza kukuza ushirika wao.
Afisa ushirika Yussuf Seif Yussuf, alisema lazima uongozi wa
ushirika huo, ujiwekee malengo ya kutoa mikopo mikubwa kwa njia ya kuongeza hisa
za wanachama.
Mshika fedha wa ushirika huo Juma Ali Juma, alisema kiujumla
ushirika huo, umepiga hatua ya kimaendeleo na ndio maana, umefikia kutoa hadi
mikopo yenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 239.
Ushirika wa ‘Tufaane saving and credit’ ambao umeanzishwa mwaka
1992, ukiwa na waanchama 45 na sasa ukiwa na wanchama 201, bado unaendelea
kukumbwa na changamoto ya uhaba wa mitaji.
No comments:
Post a Comment