Habari za Punde

Balozi Seif ataka uchunguzi ufanyike haraka kuwabaini watu waliohusika na upotevu wa baadhi ya vyarahani

 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Abdulla Juma Abdulla { Mabodi } akizungumza na Viongozi wa CCM Ngazi ya Shina hadi Wilaya ya Kaskazini “B” wakati akijitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni hapo katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Jimbo la Mahonda iliyopo Kinduni.
 Makamu wa Pili wa  Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa kushoto akimpa agizo Mkuu wa Kituo cha Polisi Mahonda kuchunguza Watu waliochukuwa baadhi ya vyarahani vya mradi wa mafunzo ya Vijana kwenye Ofisi ya Jimbo la Mahonda Kinduni.

Wa kwanza kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Abdulla Juma Abdulla { Mabodi } NA Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kaskazini Unguja Nd. Juma Haji Juma.

  Mmoja  wa Viongozi wa  CCM ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Almas Jamal Ramdhan akichangia kwenye Mkutano huo wa kutambulishwa  kwa Naibu Katibu Mkuu Mpya wa CCM  Zanzibar Dr. Mabodi hapo Kinduni.
Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Mapinduzi kuanzia ngazi ya Shina hadi Wilaya ya Kaskazini “B” wakifuatilia hotuba za Viongozi kwenye Mkutano huo wa utambilishi.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemuagiza Mkuu wa Kituo cha Polisi Mahonda na Timu yake kufanya uchunguzi wa kuwabaini watu waliohusika na upotevu wa baadhi ya vyarahani vilivyokuwa vikitumiwa na Vijana katika mafunzo maalum ya kuwajengea  uwezo wa ajira  ndani ya Ofisi ya CCM Jimbo la Mahonda hapo Kinduni Wilaya ya Kaskazini “B”.

Aliagiza uchunguzi huo uende sambamba na watakaohusika na wizi huo kuwekwa ndani kwa muda wa siku tatu na baadae taratibu za kisheria za kuwafungulia mashtaka zifuatwe kutokana na kitendo chao kiovu cha ukosefu wa nidhamu na maadili.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati wa Mkutano wa kutambulishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Abdulla Juma Abdulla {Mabodi } mbele ya Viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya Shina hadi Wilaya ya Kaskazini “B” hapo katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Jimbo la Mahonda Kinduni.

Akiwa Mbunge wa lililokuwa Jimbo la Kitope Mwaka 2010 hadi 2015 alilazimika kutumia maarifa na nguvu zake nyingi kuanzisha mradi wa Vyarahani 30 uliolenga kutoa mafunzo ya ufundi kwa Vijana wa Jimbo hilo ili kuwapa uwezo wa kujitegemea kimaisha kwa vile  fursa za ajira Serikalini kwa sasa zimepungua.

Alisema inasikitisha na kutia uchungu kuona baadhi ya Watu wameufanyia dhihaki mpango huo kwa kufikiria zaidi maslahi na mahitaji yao binafsi jambo alisema halikubaliki kabisa kwa vile linarejesha nyuma maendeleo ya Vijana walio wengi katika maeneo hayo ambao idadi yao inaongezeka kila mwaka baada ya kumaliza masomo yao.

Balozi Seif Ali Iddi amempa Mkuu wa Kituo hicho cha Polisi Mahonda kipindi kifupi cha kukamilisha uchunguzi huo na kuwasilisha ripoti ya uchunguzi huo kwake  huku taratibu za kuwapeleka mahakamani zikiendelea ili kuwabaini wabadhirifu hao wa mali na vifaa vilivyotolewa kwa ajili ya Jamii.

“ Tulilazimika kutafuta Walimu kutoka Sehemu mbali mbali hapa Zanzibar kwa ajili ya kuwafundisha Vijana wetu kazi za Ufundi ili waweze kujitegemea lakini wenzetu waliona mchezo “. Hili halikubaliki kabisa. Alisisitiza Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda.

Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi  alimpongeza Naibu Katibu Mkuu Mpya wa CCM Zanzibar Dr. Abdulla Juma Abdulla { Mabodi } kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Balozi Seif alimuahidi Dr. Mabodi kuwa Uongozi wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B” umemuhakikishia kumpa ushirikiano wa karibu katika kuona utekelezaji wa majukumu yake aliyokabidhiwa unakuwa mzuri na kuleta ufanisi mkubwa.

Mapema akizungumza na Viongozi hao wa CCM Kunazia ngazi ya Shina hadi Wilaya ya Kaskazini “B” Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dr. Abdulla Juma Mabodi aliwatahadharia wana CCM kuwa makini na Watu waliojitoa mshipa wa fahamu kuanza kutengeneza safu ya Uongozi wakijiandaa na uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.

Dr. Mabodi alionya kwamba kitendo hicho kilicho nje ya sheria kanuni na taratibu za Chama kamwe hakikubaliki kabisa wakati huu mbao Wananchi wanategemea kupata maendeleo kutoka Viongozi waliowachagua ndani ya kipindi cha sasa cha miaka Mitano.

Alipendekeza kwa Wanachama wa Chama cha Mapinduzi kuanzia ngazi ya shina kuwachagua wanachama wenzao wanaouzika kutokana na ushawishi mkubwa walionao na kuachana na wale wanaotaka madaraka kwa kutumia uwezo wa kifedha.

“ Mtaji wa Chama ni Wanachama wenyewe. Hivyo hata mkichagua  Mama Lishe, Mchuuzi wa Samaki na muuza karanga iwapo anakubalika na jamii iliyomzunguuka basi mpeni ridhaa akutumikieni “. Alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar.

Dr. Mabodi alieleza wazi kwamba Vyama vya TANU na ASP vilivyozaa Chama cha Mapinduzi vimetengeneza msingi imara na mizuri ya kupata Viongozi makini na wigwa na wana CCM wa Kizazi kipya ili kurejesha heshima ya Chama hicho kilichozaa Tanzania Mpya.

Akizungumza zoezi la uchukuaji fomu kwa ajili ya kujiandaa kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi ndani ya CCM Dr. Mabodi alisema alilazimika kuongeza muda wa saa 48 za uchukuaji wa fomu ili kuwapa fursa Wanachama wa CCM kutumia haki yao ya Kidemokrasia.

Alisema yapo malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya Wanachama wa CCM kufanyiwa mahojiano wakati wa uchukuwaji wa fomu hizo kitendo ambacho wanaelewa kuwa ni kinyume na kanuni na utaratibu wa Chama.

Aliwaonya Viongozi na watendaji wanaosimamia zoezi hilo kuacha mara moja tabia hiyo inayoashiria cheche ya rushwa katika kupanga safu ya Uongozi mambo yaliyopigwa mstari mwekundu ndani ya CCM Mpya isidita kuwafyeka mara moja watu hao ikibaini kuhusika na vitendo hivyo.

Akichangia kwenye Mkutano huo Mmoja wa Viongozi hao wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Almas Jamal Ramadhan alisema wakati huu Wana CCM wanahitaji Wanasiasa watakaokuwa makini kuchapa kazi ili kwenda sambamba na CCM Mpya iliyozaa Tanzania Mpya.

Nd. Jamal alisema kuendelea kutegemea Viongozi wa Kisiasa kipindi hichi ni sawa na kukirejesha Chama cha Mapinduzi { CCM } ndani ya dimbwi la mazonge wakati tayari k imeshajisafisha kujiendesha katika uwajibikaji wa Kitaalamu zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.