Habari za Punde

Mafunzo ya TAMWA yawapa uhakika wa soko wasusi wa mikoba


NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAJASIRIAMALI wa ususi wa mikoba ya kisasa inayotumia ukindu na kitambaa kisiwani Pemba, wamesema mafunzo ya utengenezaji wa mikoba, waliopatiwa na Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA, kupitia mradi wa WEZA II, yanaweza kuwapa uhakika wa soko.

Walisema mikoba hiyo ambayo ni tofauti na ile walioizoea, hawana wasiwasi mkubwa wa soko, kutokana na aina hiyo kuwa mpya na haijakuwa mengi sokoni.

Wakizungumza na mwandishi hizi kwa nyakati tofauti, walisema baada ya mafunzo hayo, sasa kazi iliobakia mbele yao, ni kutengeneza mikoba hiyo, ili wapate njia ya kujikwamua kiuchumi.
Mmoja kati ya wajasiriamali hao kutoka Kiuyu, Maulid Saleh Hamad, alisema yeye mikoba ya aina hiyo, kwake ni mipya na anaamini akishapa vifaa, hatarajii kukosa soko.

“Mikoba ni mizuri na wala hujui kuwa ni ya ukindu, hapa TAMWA kupitia WEZA II, imetuonyesha njia ya kufikia malengo yetu kicuhumi sisi wanawake wajasiriamali’’,alifafanua.

Nae Time Khamis Juma kutoka Tumbe Magharibi alisema, anachoomba ni kuona TAMWA, inawapatia cherahani za kisasa kwa ajili ya kushonea mikoba hiyo.

“Mafunzo tayari, sasa kazi iliobakia kwa TAMWA kupitia WEZA II, kabla ya mradi kumalizika mwaka 2019 watupatie vyerahani, ili kazi na malengo yetu yafikie haraka’’,alieleza.

Kwa upande wao Mafunda Faki Hamad wa Kiungoni kimango, na Zamu Khamis Saburi wa Kengeja walikipongeza TAMWA, kutokana na kuwapatia mafunzo hayo, ambayo walipaswa kumlipa mtaalamu fedha nyingi, ili kuwapatia mafunzo hayo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, mratibu wa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi, Asha Abdi Makame kutoka TAMWA, alisema wanalo lengo la kuwapatia wajasiriamali hao vifaa.

“Kwenye mradi huu wa miaka mitatu, tunalo lengo la kuwanunulia vifaa wajasiriamali hao, ikiwa ni pamoja na vyerahani, ingawa hawatoenea wote 100’’,alifafanua.

Hata hivyo Mratibu huyo, aliwataka waliopata mafunzo hayo, kuhakikisha wanawapa na wenzao, ili lengo la TAMWA la kuwainua wanawake kiuchumi, lifanikiwe.


Zaidi ya wajasiriamali wanawake wa ususi wa mikoba 100 kutoka shehia 25 kisiwani Pemba, wamepatiwa mafunzo ya ususi wa mikoba ya kisasa, inayotumia ukindu, kitambaa, zipu na vipolo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.