Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Azungumza na Balozi Mpya wa Cuba Tanzania Ofisi Kwake Vuga Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi zawadi ya Mlango Balozi Mpya wa Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Balozi Mpya wa Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernandez  Polledo  Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika kujitambulisha rasmi hapo Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif kati kati akiwa katika picha ya pamoja na Mtaalamu wa Benki ya Dunia anayesimamia Kampuni ya MIGA Bwana Yasumitsu Himeno    wa kulia yake baada ya kufanya mazungumzo Ofisini kwake kuhusiana na miradi ya Uwekezaji.
Wa kwanza kutoka kulia ni Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Japan Balozi Mathias Chikawe aliyeambatana na Ujumbe huo katika mazungumzo hayo.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR. 
Jamuhuri ya Cuba iko tayari kutumia Utaalamu, Maarifa, Uzoefu na hata fedha katika kuona  Zanzibar inafikia maendeleo makubwa ya Wananchi wake  Kiuchumi kama ilivyofikia Nchi hiyo.

Balozi Mpya wa Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernandez Polledo alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika kujitambulisha rasmi hapo Vuga Mjini Zanzibar.

Profesa Lucas Domingo alisema Cuba haina sababu ya kutoiunga  mkono Zanzibar katika harakati zake za kuimarisha uchumi kutokana na Historia ya muda mrefu iliyopo baina ya Visiwa hivyo  ambapo Cuba ni miongoni mwa Nchi za awali zilizounga mkono Mapinduzi ya Zanzibat ya Mwaka 1964.

Alisema Wananchi wa Jamuhuri ya Cuba tayari wameshaonyesha Ukarimu mkubwa kwa wenzao wa Zanzibar akitolea mfano mafungamano ya Sekta ya Afya yalivyoimarika na kupata mafanikio makubwa hasa ule uanzishwaji wa Chuo cha Madaktari kinachosimamiwa na Wataalamu wa Nchi hiyo.

Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo alieleza kwamba wakati umefika kwa Mawaziri wa pande hizo mbili rafiki kukaa pamoja kujadili namna viongozi hao wanavyoweza kushirikiana katika mambo yanayoonyesha kufanana katika utekelezaji wao wa pamoja.

Alisema vikao hivyo endapo vitajengewa msingi wa kudumu vinaweza kuibua mambo ya msingi ndani ya sekta ambazo kwa kisi kikubwa zinaweza kusaidia Wananchi hasa kwenye miradi ya Kilimo, Biashara na miradi ya ujasiri Amali.

Balozi huyo wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania amemuahidi  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kipindi chake cha utumishi wa Kidiplomasia kwamba atazingatia zaidi kuimarisha uhusiano wa Kihistoria wa pande hizo mbili.

Akitoa shukrani zake  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema iwapo Zanzibar na Jamuhuri ya Cuba zitashirikiana kwa karibu zaidi katika miradi iliyomo ndani ya Sekta za Kilimo, Afya na Utalii yapo maendeleo ya haraka yanayoweza kubadilisha maisha ya Wananchi wa pande hizo mbili.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapainduzi ya Zanzibar tayari imeshatoa msukumo zaidi katika Sekta ya Utalii inayoonyesha matumaini ya uhimili wa Uchumi wa Taifa kwa vile itakuwa na fursa nyingi zinazoweza kutoa ajira sambamba na kuongeza Mapato ya Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kuishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Cuba kwa juhudi inazochukuwa za kuiunga mkono Zanzibar katika Sekta ya Afya ambayo tayari imeshazalisha Madaktari wazalendo wasiopungua 50 kupitia Chuo cha Madaktari kinachosimamiwa na Wataalamu wa Nchi hiyo.

Balozi Seif alisema mpango huo wa kusomesha Madaktari Wazalendo hapa Nchini ulioanza kuleta mafanikio makubwa ulibuniwa kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano alipotembelea Nchini Cuba.

Alisema moja ya fanikio kubwa lililopatikana na ubanaji wa matumizi ya Serikali ambayo mwanafunzi Mmoja wa kada ya Udaktari angelazimika kulipitia masomo yake kwa zaidi ya Dola za Kimarekani 17,000 elfu.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Wataalamu wa Benki ya Dunia wanaojishughulisha na kusimamia miradi ya uwekezaji kupitia Kampuni ya MIGA yenye Makao Makuu yake Nchini Japan.

Mazungumzo hayo ambayo  pia yalimjumuisha  Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Japan Balozi Mathias Chikawe aliyeambatana na Ujumbe huo yalifanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Mtaalamu huyo wa Benki ya Dunia anayesimamia Kampuni ya MIGA Bwana  Yasumitsu Himeno alimueleza Balozi Seif  kwamba Taasisi hiyo imeundwa  kwa lengo la kusukuma Wawekezaji kutumia fursa za ujenzi wa miundombinu ya Kiuchumi katika Mataifa yanayopata msaada au ufadhili wa Benki ya Dunia.

Bwana Yasumitsu alisema ipo miradi mingi iliyoanzishwa katika Mataifa mbali mbali yenye uwanachama wa Benki ya Dunia ambayo hupata mikopo chini ya Makampuni yanayodhaminiwa na Benki hiyo yanayotozwa gharama za asilimia 50% ya mradi wanaoutekeleza.

Alitoa mifano ya miradi hiyo kuwa ni pamoja Hospitali kubwa zenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa katika Mikoa Mikoa na Miji Mikubwa, majengo ya Vyuo Vikuu, Viwanja vya Ndege, miradi ya Ulinzi na hata miuondombinu ya Bara bara.

Bwana Yasumitsu Himeno alifafanua kwamba miradi hiyo yenye kulenga kuhudumia jamii hupewa upendeleo maalum wa kurejesha mikopo kidogo kidogo  baina ya miaka 20 na 30 kwa mujibu wa mikataba inavyofikiwa.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  ameushauri Uongozi wa Kampuni hiyo ya MIGA kuangalia uwezekano wa kuunga mkono Mpango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kutaka kuziimarisha Hospitali Mbili za Mikoa ya Kukisini na Kaskazini za Kisiwa cha Unguja.

Balozi Seif alisema mpango huo umelenga kwenda sambamba na wazo la Serikali Kuu la kutaka kujenga Hospitali ya kufundishia Madaktari katika eneo la Binguni Wilaya Kati.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo kwamba bado una fursa nyingi za kufikiria maeneo ambayo wanaweza kuwekeza, au kusaidia na hata kuingia katika miradi ya ubia Visiwani Zanzibar  kwa kufanya ziara maalum ya kukutana na taasisi zinazosimamia masuala hayo hapa Zanzibar.

Alisema ipo miradi ya utanuzi wa Uwanja wa ndege wa Pemba, upatikanaji wa Umeme Mbadala ambao kwa sasa Zanzibar  inategemea kianzio kimoja tu kutoka Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.