MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kukamilika kwa ujenzi wa diko na soko la kisasa la samaki katika eneo la Fungurefu lililopo Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, kutatoa fursa kwa zaidi ya wananchi 10,000 kufanya biashara katika soko hilo.
Mhe. Hemed ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua miradibali mbali ya maendeleo inayojenga katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwemo mradi wa ujenzi wa diko na soko la samaki linaojengwa na kampuni ya Emirate Construction Ltd.
Amesema ujenzi huo utakapokamilika utatoa fursa kwa wananchi wenye vipato vya chini kuviimarisha vipato vyao kwa kufanya kazi katika mazingira mazuri yenye kukidhi mahitaji muhimu kwenye diko na soko la samaki.
Amefahamisha kuwa kabla ya ujenzi huo wajasiriamali walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukosa eneo rasmi na salama kwa ajili ya kufanyakazi zao, hivyo litakapokamilika watafanya biashara katika soko lenye hadhi na ubora.
Amewagiza viongozi wenye dhamana ya kushughulikia mradi huo kuhakikisha wanafanya wajibu na majukumu yao kwa wakati ili kuhakikisha mradi huo ukamilike kwa wakati hatua ambayo itawawezesha wafanyabiashara kutekeleza majukumu yao.
Makamu wa Pili wa Rais, amewapongeza wananchi kwa uamuzi wa kuondoka katika eneo hilo na kupisha ujenzi wa soko, jambo linalodhihirisha utayari wao wa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Dk. Hussein Mwinyi za kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Shaaban Ali Othman, amesema wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, zipo katika mchakato wa kukamilisha taratibu za ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa soko hilo ambao wameondoka kwa hiari.
Waziri Shaaban amesema wizara itahakikisha inasimamia vyema mradi wa ujenzi wa diko na soko la samaki la Fungu refu ili liweze kujengwa katika viwango vyenye ubora na kumalizika kwa wakati.
Naye, Mkurugenzi wa kampuni ya Emirate Construction Ltd. Mhandisi Suleiman Amour Salim ambaye ndiye mjenzi wa soko hilo, amesema ujenzi huo utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 11 na kuahidi kujenga kwa viwango na kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Katika hatua nyengine kwenye ziara hiyo, Mhe. Hemed pia alitembelea mradi wa uhuishaji na uboreshaji wa huduma ya maji safi na salama katika eneo la Kilindi Nungwi unaojegwa na kampuni ya National Energy Center unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.
Akikagua mradi huo, ametoa agizo kwa wizara ya Maji, Nishati na Maadini kuhakikisha wakandarasi wanaongeza kazi ya ujenzi itakayowezesha kukamilika kwa wakati ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama haraka iwezekanavyo.
Aidha Makamu wa Pili, alikagua ujenzi wa skuli ya Maadalizi Donge Karange inayojengwa na Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) ambapo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 95 na inatarajiwa kukabidhiwa serikalini mwezi Septemba mwaka huu.
Mhr. Hemed amewapongeza Dk. Abdulhalim Mohamed Ali na Mohamed Kombo Mohamed kwa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa skuli ya maadalizi Donge Karange pasipo kuhitaji malipo yoyote ni jambo la kupigiwa mfano linalodhihirisha kuunga mkono maendeleo yanayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Miradi mingine iliyokaguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ni ujenzi wa skuli ya msingi Potoa, skuli ya maandalizi Kibuyuni, ujenzi wa skuli ya maadalizi Kinyasini na ujenzi wa barabara ya Bumbwini-Pangatupu- Mahonda.
Miradi mingine ni ujenzi wa daraja la Pangatupu, ujenzi wa nyumba za wafanyakazi katika hospitali ya Wilaya Pangatupu, mradi wa kuimarisha maeneo ya kihistria Mangapwani, skuli ya maandalizi Kitope na ujenzi wa skuli ya maandalizi Vuga Mkadini.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 14.07.2025
No comments:
Post a Comment