Habari za Punde

MWAIPAJA: TUTAENDELEA KUTOA ELIMU KWENYE MAJUKWAA MENGINE BAADA YA SABASABA

Mkuu wa Kitengo chanMawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja,akiwapongeza wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha wakati wa mahojiano na Mwandishi wa Habari Bw. Richard Steven, baada ya kuhitimishwa kwa Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) katika Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Timu ya ushindi  wa Banda Bora na utoaji elimu kwa wananchi kwa weledi, ikiwa inaonesha ishara ya ushindi baada ya kuhitimishwa kwa  Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) katika Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam. 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)



Na. Peter Haule na Joseph Mahumi,WF, Dar es Salaam

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja amewataka wananchi kuendelea kutumia majukwaa ya Wizara hiyo kujifunza kuhusu uchumi na fedha baada ya kuhitimishwa kwa Maonesho ya  Sabasaba kwa mwaka 2025.   

Rai hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam  wakati wa kuhitimisha Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) katika Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa.

Bw. Mwaipaja amewapongeza na kuwashukuru wananchi wote waliopata fursa za kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu uchumi na fedha na kuahidi kuendelea kutolewa kwa elimu hiyo katika majukwaa mengine.

Alisema Wizara kupitia Idara, Vitengo na Taasisi zake imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa weledi kuhusu, Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge na matumizi yake katika kutekeleza miradi ya maendeleo na Sera ya uchumi ilivyowalenga wananchi katika shughuli zao za maendeleo. 

Alitaja mambo mengine yaliyotolewa kwa wananchi kuwa ni elimu ya sekta ya fedha, maktaba, pensheni itolewayo na hazina, miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, mifumo ya fedha, uwekezaji, mabenki, masoko ya bidhaa na mitaji, mnyororo wa ugavi na kozi mbalimbali zinazotolewa na Vyuo vya elimu ya juu vilivyo chini ya Wizara ya Fedha.

Bw. Mwaipaja amesema ubora wa Banda la Wizara na weledi katika kutoa elimu sahihi kwa wananchi kumeifanya Mamlaka ya Uendelezaji Biashara nchini, Tantrade, kutoa tuzo ya ushindi kwa nafasi ya tatu kati ya Wizara zote zilizoshiriki Maonesho hayo ya Mwaka huu, jambo ambalo ni ushindi mkubwa kwa Wizara na Viongozi wanaosimamia weledi wa watumishi ndani ya Wizara na Taasisi zake. 

Aidha Bw. Mwaipaja ametoa rai kwa wananchi kuendelea kulipa kodi na wafanyabiashara kuendelea kutoa risiti ili Serikali iendelee kutekeleza miradi mikubwa kama Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere na miondombinu mingine wezeshi.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.