WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kuendeleza juhudi za kutafuta masoko ya nje ili kuongeza mauzo yatakayowezesha nchi kupata fedha za Kigeni.
Amesema kuwa TanTrade inapaswa kufanya tafiti za uhakika na uchambuzi wa masoko ambayo bidhaa za Tanzania zinaweza kuuzwa na kutoa taarifa hizo kwa wafanyabiashara kote nchini.
Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 13, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufungaji wa Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar-es-Salaam.
“Masoko yamekuwa ya ushindani sana siku hizi, nilipotaja Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) nilikuwa nataka kuwaambia kwamba leo hii tunapotaka kufanya uchambuzi wa masoko yetu, hayo ndio maeneo ya kufanya biashara, TanTrade fanyeni tafiti za uhakika na uchambuzi wa kina”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wazalishaji wote nchini kuweka mkakati wa kuongeza uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa ambazo zina mahitaji makubwa katika masoko ndani na nje ya nchi. “Maonesho haya ya 49 ya biashara yanapaswa kuwapa mwanga wa bidhaa gani zina mahitaji makubwa ili muweze kuongeza uzalishaji tunahitaji kupanua wigo wa masoko kwenye mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi”
Kadhalika, amewataka Wazalishaji hao kuzalisha bidhaa zenye ubora mkubwa ili watumiaji waweze kuridhika ubora wake na ziweze kumudu ushindani wa kimataifa. “Pamoja na hayo msisahau kutumia ile haki ha nembo ya Tanzania ambayo ni alama yetu ya Taifa letu, kila bidhaa unayoizalisha hakikisha pale chini umeandika made in Tanzania, hiyo ndiyo nembo yetu ya Taifa”
Pia Mheshimiwa Majaliwa amezitaka taasisi zote zinazosimamia Biashara na Uwekezaji, Tanzania Bara na Zanzibar, zihakikishe zinaondoa urasimu na kuwezesha Biashara zaidi badala ya kuwa kikwazo.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia washiriki wa maonesho hayo muwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji zaidi katika maeneo ya kimkakati ili kuchangia kikamilifu katika pato la taifa na kunufaisha wananchi wetu.
Kwa Upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo katika kipindi cha siku 16 cha maonesho hayo, watu zaidi ya milioni 2.4 wameweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za maonesho hayo ya kimaitaifa ya biashara.
Pia ameongeza kuwa kupitia nembo ya Made in Tanzania, itaiwezesha nchi kuuza biadhaa zikiwa na nembo ya Taifa. “Hii ni fahari kubwa sana kwetu sisi watanzania”
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA.
JUMAPILI, JULAI 13, 2025.
No comments:
Post a Comment