Habari za Punde

Msivifanye kinga vyandarua kwenye vitalu vya miche: Ushauri

Na.Haji Nassor, Pemba.
WANANCHI wanaoatika miche kwenye vitalu, wameonywa kuacha tabia ya kutumia vyandarua kama kinga ya miche yao, na badala yake, wabuni njia nyengine ikiwa ni pamoja na kuzungurushia makuti.
Kuali hiyo imetolewa na Afisa Mipango wa wilaya ya Chakechake Kassim Juma, alipokuwa akizungumza kwenye mafunzo ya utayarishaji wa vitalu bora yalioandalia na Jumuia ya Mazingira Vitongoji VECA na kufanyika skuli ya maandalizi Madungu Chakechake.
Alisema vyandarua vinayotolewa na serikali ni kwa ajili ya kinga ya mbua wanaosababisha malaria, na sio kutumika kwenye kukinga wadudu wanaoharibu miche.
Alisema VECA aipo kwa ajili ya kutoa elimu hiyo, hivyo ni vyema wanaoatika miche na wenye malengo ya kufanya hivyo, wasisite kuitumia jumuia hiyo ili wapate taaluma ya kina.
Aidha Afisa mipango huyo, alisema moja ya kosa linalofanywa na wanaotika miche kwenye vitalu ni kufanya kazi hiyo zaidi kwa ajili ya kujipatia kipato badala ya kuwa na lengo la kuhifadhi mazingira.
“Kila mkulima anaesimama hapa anasema anatumia chandarua kwa ajili ya kuhifadhia miche, hiyo sio njia sahihi maana hivyo ni kwa ajili ya wananchi kujikinga na mbu wanaosababisha malaria hivyo acheni utamaduni huo’’,alifafanua.
Katika hatua nyengine Afisa mipango huyo amepongeza VECA kwa jitihada zake za makusudi katika kuwapa taaluma wananchi wakiwemo wa upandaji miti na wanaoatika vitalu.
Mapema akifungua mafunzo hayo ya siku tatu, Katibu wa VECA Sifuni Ali Haji aliwataka waatika miche hao kuhakikisha mafunzo walioyapata wanawapa na wenzao ili lengo la VECA la kuhifadhi mazingira lifikiwe.
Hata hivyo Katibu huyo alisema wanawake wanayonafasi kubwa ya kuwaelimisha wanaume kuacha kuangusha miti bila ya kuwa na utaratibu wa kupanda mengine.
“Wanaume ndio hasa wanaoongoza kwa kukata miti iwe ni kwa ajili ya kupiga mkaa, ujenzi, kuni au kutengenezea fanicha, sasa sisi wanawake lazima hili tulikemee, maana waathirika wakubwa ni sisi’’,alifafanua.
Akiwasilisha njia sahihi ya utayarishaji wa vitalu, mtoa mada Mohamed Najim Omar, alisema suala la chanzo cha maji, usawa na eneo ni miongoni mwa mambo ya kuzingatia kwa muatikaji wa miche.
Baashi ya washiriki wa mafunzo hayo, wamesema laiti kama VECA ingepata ufadhili zamani na kuwapa mafunzo hayo, wengekuwa wameshapiha hatua kubwa ya kuhifadhi mazingira.

Mafunzo hayo ya siku tatu, ambayo yametayarishwa na Jumuia ya Maendeleo Vitongoji ‘VECA’ na kufadhiliwa na Shirika la Uhifadhi wa kimataifa la ‘Global green grant fund’ la Marekani kupitia mfuko wa kimazingira wa duinia, mada kadhaa zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na wanawake na mazingira, utayarishaji wa vitalu na athari za kutohifadhi mazingira.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.