Habari za Punde

TOVUTI ZA MIKOA NA WILAYA ZIONGEZE TIJA KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA SERIKALI KWA UMMA.

Na Ismail Ngayonga                                                                                                        
Maelezo Dar es Salaam.
TANZANIA ni mwanachama wa Mpango kimataifa wa uendeshaji wa shughuliza Serikali kwa uwazi (OGP) uliobuniwa mwaka 2011 na wadau mbalimbali zikiwemo Serikali na Asasi za kimataifa zisizo za kiserikali.

Katika Bara la Afrika nchi wanachama ni Tanzania, Afrika ya Kusini, Kenya, Liberia, Tunisia, Ghana, Malawi na Siera Leone.

Mpango wa OGP unajikita katika maeneo makuu manne ambayo ni uwazi, ushirikishwaji wa wananchi, uwajibikaji na maadili na matumizi ya teknolojia na ubunifu. Mpango huu una lengo la kuboresha utoaji huduma, kuwajibika kwa wananchi na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao.

Miongoni maeneo makuu ya yaliyopewa kipaumbele na Serikali katika Mpango huo ni pamoja na utoaji wa taarifa kwa uwazi ili kuwawezesha wananchi kuweza kuifuatilia utekelezaji wa shughuli za Serikali yao katika ngazi mbalimbali za mamlaka ikiwemo Serikali, Mikoa na Wilaya.

Pamoja na maelekezo hayo ya Serikali, ilibainika tovuti za Mikoa na Wilaya ni miongoni mwa mitandao ya kijamii inayotumiwa na wananchi wengi pamoja na changamoto mbalimbali inazozikabili tovuti hizo ikiwemo uhuishaji wa taarifa mpya na za wakati.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, hivi karibuni Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) ziliendesha mafunzo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti kwa Maafisa Habari na TEHAMA kutoka Mikoa 5 na Halmashauri 33 za Mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Simiyu. 

Akifunga mafunzo hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Dkt. John Ndunguru anasema Serikali haitovumulia watendaji wake wenye tabia ya kubania upatikanaji taarifa kwa wananchi kwani zama hizo zimepitwa na wakati.

Aliongeza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa tovuti zinakuwa na habari na taarifa mpya ili kuongeza uwazi kati ya Serikali na wananchi na hivyo kuondoa utata na upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu juu ya taarifa za Serikali.

“Naamini kwamba baada ya mafunzo haya, taarifa kama vile bajeti, MTEF, mpango mkakati pamoja na fomu mbalimbali kama za maombi ya leseni za biashara, zitakuwa hazina urasimu tena” alisema Dkt. Ndunguru.

Aidha Dkt. Ndunguru aliwataka watendaji wa Serikali kutoa ushirikiano kwa Maafisa Habari katika maeneo yao ya kazi kwa kuwa suala la utoaji na taarifa litasaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi wake.

Kwa mujibu wa Mhandisi Ndunguru anasema mafunzo hayo ya utengenezaji wa tovuti yametokana na matokeo ya utafiti yaliyofanywa na wataalamu mbalimbali katika kubaini changamoto na vikwazo zinakabili Mikoa na Halmashauri nchini, katika suala la utoaji wa huduma kwa jamii.

Mhandisi Ndunguru anasema kuwa ni wajibu wa Maafisa Habari na TEHAMA kuwajibika kikamilifu katika kuzisimamia na kuziendesha tovuti hizo kwa kuweka taarifa mpya kwa kuwa uwajibikaji huo utaweza kuongeza imani kwa wafadhili wa mradi huo, Shirika la misaada la Marekani (USAID) na hivyo kuwekeza katika miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

“Nitoe wito kwa Maafisa Habari kujitahidi sana kutoa sahihi na kwa wakati, kwani mlipokuwa Dodoma katika mkutano wenu, Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliwaasa msome, kuilewa na kuifanyia kazi sheria zinazowaongoza, ambazo ni Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na ile ya Haki ya kupata Taarifa ya mwaka 2016” alisema Dkt. Ndunguru.

Akifafanua zaidi Dkt. Ndunguru alisema uwekaji wa taarifa sahihi zilizozingatia muda na wakati katika  tovuti hizo zitaweza kuifanya Tanzania kuigwa na nchi nyingine Barani Afrika na duniani kote kwa kuwa na Serikali yenye utawala bora na uwazi kwa wananchi wake.

Akitoa salamu za Mkurugenzi wa Mradi wa PS3, Dkt. Emmanuel Malangalila, Meneja Mradi wa PS3 Mkoa wa Morogoro David Ole Laput anasema dhumuni la mradi wa PS3 ni kutoa msaada wa kitaalam kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya sekta za umma ili kusaidia utoaji wa huduma za jamii, hususani jamii za pembezoni.

Alisema mradi wa PS3 kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) walikaa kwa pamoja na kuandaa mfumo mpya yaani Government Website Framework (GWF) ili kuwezesha Serikali kuwa na uwazi zaidi katika kuwasiliana na wananchi wake.

“Kupitia mfumo huu, PS3 kwa kushirikiana na TAMISEMI na EGA waliendesha mafunzo hayo ya tovuti kwa awamu ya kwanza mwezi Februari, 2017 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Halmashauri za Mikoa hizo, ambayo ni Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Shinyanga na kuziwezesha tovuti za Mikoa hiyo kwenda hewani” alisema Laput.

Aliongeza kuwa katika Awamu ya pili ya uandaaji wa tovuti na mafunzo hayo yamefanyika katika mikoa yote nchini kwa wakati mmoja kuanzia tarehe 20-27 Februari, 2017 katika kanda tano za Mikoa 22 nchini.

Anaitaja mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Simiyu, Tanga, Mbeya, Songwe, Rukwa, Njombe, Kigoma, Katavi, Tabora, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Dodoma, Iringa, Dar es Salaam,Pwani, Singida, Manyara na Geita.

Kwa mujibu wa Laput alisema pamoja na Mradi wa PS3 kutekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania Bara, kutokana na uundwaji wa tovuti hizo kuwa muhimu kwa kila mwananchi wa Tanzania, USAID imewezesha kufanikisha mafunzo hayo katika Halmashauri na Mikoa yote ya Tanzania Bara bila kubagua.

“Kupitia tovuti hizi, wananchi wataweza kupata taarifa, kuchukua fomu za mahitaji mbalimbali na mahitaji mengineyo ambapo matumizi ya tovuti hizi yatasaidia kupunguza mlolongo wa kukaa kwenye foleni au kutumia muda mrefu kupata taarifa” alisema Laput.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.