Habari za Punde

MSHAMBULIAJI WA SERENGETI BOYS AJUMUISHWA KATIKA KIKOSI CHA MJINI UNGUJA, ALIPORUDI GABON TU AFCON KOCHA KING AMDAKA, LEO AANZA MAZOEZI NA WENZAKE

Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.
Mshambuliaji wa Klabu ya Miembeni City, Ibrahim Abdallah “Imu Mkoko” asubuhi ya leo ameungana na wachezaji wa kombain ya Mjini Unguja kwenye mazoezi katika Uwanja wa Amaan kwa kujiandaa na Mashindano ya Vijana ya Rolling Stone yanayotarajiwa kuanyika mwezi July mwaka huu jijini Arusha.
Mkoko amerejea Visiwani Zanzibar juzi akitokea mjini Gentil, Gabon katika michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya AFCON akiitumikia timu ya Taifa ya Tanzania “Serengeti Boys” baada ya kutolewa kwa kufungwa 1-0 na Niger katika mchezo wa mwisho wa Kundi B Uwanja wa Port Gentil mjini Gentil, nchini Gabon.
Mara baada ya kumaliza mazoezi asubuhi ya leo Mtandao huu umefanya mahojiano na mshambuliaji huyo kwa kuelezea kujiunga na timu hiyo ya Mjini.

“Nimefurahi kuona kuwa bado Wanzibar na Watanzania wana imani na mimi, nilipowasili tu Zanzibar kutokea Gabon nkapigiwa simu na kocha King nije kujiunga na timu ya Mjini Unguja, nimefurahi sana na leo nimejiunga na wenzangu kwa kujiandaa na mashindano ya Rolling Stone”.
 Aidha pia Mtandao huu tukataka kujua kipi alichojifunza katika Mashindano ya AFCON ambapo Imu ni miongoni mwa vijana wa Tanzania waliyoweka rikodi kucheza Mashindano hayo.
“Nimejifunza vingi kule, maana nimezidi kuona kuwa mchezaji ana thamani gani, tulipokelewa vizuri, tukakaa hoteli nzuri, tumekula vyakula vizuri, tulikuwa tunalindwa, na kubwa zaidi yaani kule unathaminiwa kama ni Professional Player, kuna tofauti kubwa kucheza mashindano yale na haya tuloyazowea, unapata hela za kusaidia familia yako,  kule Kisandu yaani wewe acha tu,”. Alisema Mkoko.
 Pia tukazungumza na Kocha Mkuu wa Kombain ya Mjini Unguja Mohammed Seif “King” ambapo amesema ujio wa Mshambuliaji wa Imu Mkoko umewafurahisha sana Viongozi wao huku wakiamini watatetea taji lao la Rolling Stone Jijini Arusha mwezi July, 2017.

“Leo mazoezi tumempokea Imu Mkoko na ujio wake tumefarijika sana tunaamini atazidi kuleta hamasa kwenye kikosi chetu na kutetea taji letu”. Alisema kocha King.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.