STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 12.05.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepongeza azma ya Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu
ya Iran ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za
maendeleo kwa lengo la kukuza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati
ya pande mbili hizo.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo katika mazungumzo kati yake na Balozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Moussa Ahmed Farhang, mazungumzo yaliofanyika
Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Dk.
Shein alipongeza juhudi za nchi hiyo za kuendeleza ushirikiano na uhusiano
mwema uliopo ambao una historia na kuihakikishi nchi hiyo kuwa Zanzibar
utaudumisha.
Dk. Shein alisema kuwa
kuna haja ya kuendelea kuitunza na kuiimarisha historia iliyopo kati ya Iran na
Zanzibar kwani watu wa Zanzibar wanafahamu fika uhusiano huo ambao Mabalozi
wote waliofanya kazi kabla ya Balozi Farhang waliuendeleza.
Aidha, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kueleza miongoni mwa mambo muhimu ikiwemo miradi ya
maendeleo ambayo Iran imeisaidia Zanzibar ikiwemo kuendeleza elimu ya amali kwa
kusaidia vifaa, fedha taslim, nafasi za masomo ya elimu ya juu, nafasi za
mafunzo ya utaalamu ya muda mfupi kwa ajili ya walimu wa elimu ya vyuo vya
amali.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado ina
matumaini makubwa ya azma na ahadi ya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kukiimarisha kituo cha Afya cha Mbuzini,
kilichopo Wilaya ya Mgharibi A.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alimueleza Balozi huyo kuwa bado Zanzibar ina kumbuka ahadi ya Serikali
ya Iran ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ambapo tayari Serikali
imeshakijenga na kukiendeleza chuo hicho.
Dk. Shein Shein pia,
alimueleza Balozi Farhang haja ya
kushirikiana katika suala zima la utafiti pamoja na masuala mengine ya
kisayansi.
“Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ikiwemo Zanzibar iko tayari kufanya kazi na kuendeleza uhusiano na
ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa maslahi ya nchi zetu na
watu wake”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano kati
yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni pamoja na kulifanyia kazi wazo la
kuunda timu ya watendaji ambayo itaweza kubadilishana uzoefu, utaalamu pamoja
na kuyafanyia kazi mambo yatakayokubaliwa kimashirikiano kati ya pande mbili
hizo.
Nae Balozi wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Moussa Ahmad Farhang alimuhakikishia Dk. Shein kuwa nchi
yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta za
maendeleo, uchumi na za kijamii.
Balozi Farhang
alimueleza Dk. Shein kuwa Iran inaithamini sana Zanzibar pamoja na watu wake
kwani nchi hiyo ina kumbukumbu nyingi za Zanzibar na jinsi watu wake
walivyokuwa wakishirikiana pamoja na Serikali zao miaka mingi iliyopita.
Alieleza kuwa Serikali
ya Iran iko tayari kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Mbuzini na hivi sasa imo
katika kusubiri taratibu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara
husika zikamilike ili ujenzi huo uanze kwani tayari fedha zake zipo kiasi cha
Dola laki 5.
Aliongeza kuwa Serikali
ya Iran inakumbuka jinsi Zanzibar ilivyoiunga mkono na kuisaida nchi hiyo
wakati ilipowekewa vikwazo, na hivyo haina malipo ya kuilipa Zanzibar bali ni
kuendeleza na kuimarisha ushrikiano na uhusiano wake kwa Zanzibar.
Balozi Farhang aliieleza
matumaini makubwa ya Iran kuwa Zanzibar itaendelea kupata mafanikio zaidi ya
kiuchumi, kijamii na kiutamaduni huku akiahidi Iran kuleta walimu kwa ajili ya
kutoa mafunzo ya walimu wa vyuo vya amali vya Zanzibar.
Hata hivyo, kiongozi
huyo alipongeza hatua za kuimarisha ushirikiano kwa kutembeleana kati ya
viongozi wa pande mbili hizo na kutoa wazo la viongozi kuunda timu kwa ajili ya
mashirikiano ya pamoja kati ya Iran na Zanzibar huku akihadi nchi yake kuunga
mkono na kutekeleza vipaumbe vya Zanzibar.
Sambamba na hayo, Balozi
huyo alimueleza Dk. Shein kuwa umbali uliopo kati ya Iran na Zanzibar sio
sababu ya nchi yake kutoshirikiana na Zanzibar na kumuahidi kuwa ushirikiano uliopo
utadumishwa huku akitumia fursa hiyo kupongeza amani na utulivu iliyopo
Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein ambayo ndio chachu ya maendeleo yaliopo.
Balozi Farhang pia,
alitumia fursa hiyo kumpa Dk. Shein salamu za Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran Rais Hassan Rouhani za kumtakia uongozi mwema ambapo Dk. Shein nae alipokea
salamu hizo kwa furaha na kwa upande wake alimpa Balozi huyo salamu zake kwa
kiongozi huyo wa Iran.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment