Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Shein Apokea Msaada wa Vyakula Kwa Ajili ya Wananchi Waliopata Maafa ya Mvua na Upepo Zanzibar.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                               20.05.2017
---
PONGEZI zimetolewa kwa Wafanyabiashara walioonesha kitendo cha kizalendo na kishujaa kwa kuanza kutoa misaada kwa waathirika waliopata maafa ya mvua zilizonyesha maeneo mbali mbali Unguja na Pemba pamoja na upepo mkali uliotokea katika Mkoa wa Mjini Magharibi hivi karibuni na kuleta athari kubwa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi hizo Ikulu mjini Zanzibar mbele ya viongozi wa Serikali, waandishi wa habari na Wafanyabiashara walioongozwa na Mohammed Raza ambaye pia, ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Ahmada Yahya Abdulwakil ambaye pia, ni Mwakilishi wa Kuteuliwa na Rais pamoja na mfanyabiashara maarufu Said Nassor Popar.

Dk. Shein aliwapongeza wafanyabiashara hao ambao pia,  baadhi yao ni viongozi kwa mwanzo mzuri walioanza kuuonesha kwa kufanya kitendo hicho ambacho ni faraja kubwa kwa wananchi waliopata maafa pamoja na kutoa ushirikiano mwema na Serikali yao.

Pia, Dk. Shein hakuchelea kutumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa vyombo vya habari kwa kutoa taarifa ya maafa hayo sambamba na wito alioutoa kwa wale wote wenye uwezo kuwasaidia wale waliokuwa hawana uwezo ambao wamekumbwa na maafa hayo.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa mvua hizo zimeweza kuleta athari kubwa hasa katika kisiwa cha Pemba na kueleza kile alichokiona katika ziara yake hivi karibuni kisiwani humo ambapo kabla ya hapo alifanya ziara kama hiyo katika maeneo ya Unguja hasa katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambao ulikumbwa na mafuriko yaliotokana na  mvua pamoja na upepo mkali.

Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na juhudi zilizochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi , Mawasiliano na Usafirishaji  kwa hivi sasa hakuna barabara wala daraja lisilopitika katika yale yalioharibika na mvua hizo za masika katika barabara za Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa matokeo hayo yote ni shani ya Mwenyezi Mungu hivyo wananchi wanatakiwa wawe na subira na uvuvilivu huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea na juhudi za kuhakikisha wananachi wanapatiwa misaada na maeneo yalioathirika na mvua yanafanyiwa utaratibu maalum ili yasijekuleta madhara  katika mvua zijazo.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali itaendelea kupokea misaada mengine itakayotolewa huku akitoa nasaha zake kwa wafanya biashara hasa katika kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuacha kupandisha bei za bidhaa hasa vyakula kwani Serikali imeamua kwa makusudi kusamehe sehemu ya ushuru wa bidhaa za vyakula ili wafanyabiashara wawauzie wananchi bidhaa hizo kwa urahisi lakini kinachotokea ni tofauti.

Hivyo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwataka baadhi ya wafanyabiashara kuacha mtindo huo mara moya na kusisitiza kuwa iwapo wataendele nao serikali haitowavumilia na kusisitiza kuwa Serikali ikiona hilo linaendelea itaurejesha ushuru huo wa bidhaa za vyakuwa wakati wa mwezi wa Ramadhani kwani wananchi wamekuwa hawafaidiki na chochote.

Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa matarajio yake makubwa kuwa hapatakuwa na ubabaishaji wala hadaa katika ugawaji wa misaada hiyo inayotolewa na wafanyabiashara na ile itakayotolewa na Serikali kwani Kamisheni inayosimamia misdaa hiyo ina wajumbe weledi.

Katika kupambana na athari na maafa ya mvua aliahidi kuwa kwa upande wa Bwawa la Mwanakwerekwe ambapo maji hutuama, kupitia Mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) Awamu ya Pili, maji hayo yataondoshwa kwa kuelekwezwa pwani pamoja na kujenga daraja la kisasa katika eneo la Kibondemzungu.

Alisema kuwa Serikali inafanya tathmini juu ya athari zote zilizotokea katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba pamoja na athari ya upepo mkali uliotokea katika maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi huku akisisitiza akuwa Serikali ni lazima itafute jitihada za kujihami na kukushanya uwezo kwa ajili ya maafa.

Dk. Shein alisisitiza kuwa ni vyema Serikali ikaangalia pale inapojenga barabara ni busara ikajengwa na mitaro ya kupitishia maji kwani athari kubwa iliyotokea katika miundombinu ya barabara nyingi hapa nchini imetokana na barabara kukosa mitaro.

Akitoa nasaha zake kwa niaba ya wafanyabiashara hao Mohammed Raza alieleza kuwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya Zanzibar wataendelea kuwasaidia ndugu zao waliokumbwa na mafuriko na athari za upepo ambapo misaada hiyo ikiwemo ya vyakula, fedha taslim na vifaa vya ujenzi itasaidia hasa katika kipindi cha Mwezi wa Ramadhani unaokaribia.

Raza alisema kuwa kitendo hicho walichokifanya ni utamaduni wa Wazanzibari wa kusaidiana wakati wa furaha na shida ambapo kwa upande wake ametoa fuso nne za vyakula vikiwemo sukari pakiti 500, unga wa ngano pakiti 500, mafuta ya kupikia katuni 100.

Nae Ahmada Yahya Abdulwakil alimkabidhi Rais TZS milioni 10 kwa Unguja na Pemba pamoja na kuahidi msaada wa nondo tani mbili za milimita 10 zenye thamani ya TZS milioni 3 ambapo kwa upande wa  mfanyabiashara Said Nassor Popar ametoa idadi kama hiyo ya vyakula kupeleka kisiwani Pemba ambako vitagawiwa kupitia Ofisi husika, pamoja na tende na sabuni.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.