Habari za Punde

Ugonjwa wa kipindupindu wajitokeza Zanzibar, Serikali yapiga marufuku uuzwaji wa vyakula katika maeneo yasiyokuwa rasmi

Wakati mvua za masika zikishika kasi na kuziathiri nyumba kadhaa, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema watu 23 wamegundulika kwa na ugonjwa wa   kipindupindu.


Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo, Waziri wa Elimu, Riziki Pembe Juma amesema miongoni mwa watu hao yumo mtoto wa miezi mitatu na mzee mwenye miaka 75.


Riziki amesema waliobainika kuathirika na maradhi hayo ni wananchi kutoka wilaya za Mjini, Magharibi A, Magharibi B na Kaskazini A kwa upande wa Unguja na wilaya za Micheweni na Wete kisiwani Pemba.


Amesema kambi imefunguliwa Chumbuni na tathmini ya madaktari inaonyesha wagonjwa hao wameathiriwa kutokana na mazingira kuwa machafu kutokana na mvua iliyosababisha baadhi ya nyumba kuzungukwa na maji.


Kutokana na hilo, Wizara ya Afya imepiga marufuku uuzaji wa vyakula usiofuata sheria na kwamba, kwa kushirikiana na taasisi zingine itatoa elimu kwa jamii, kutoa dawa na maji kwa wananchi.


Kaimu Mkurugenzi Huduma za Afya, Dk Mohamed Dahoma amesema ni wajibu wa wazazi na walimu kuwalinda watoto ili wasiambukizwe maradhi hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.