Habari za Punde

Waride asisitiza ubunifu kwa watendaji wa CCM n a serikali

 Katibu wa NEC,  Idara ya Itikadi na Uenezi  CCM Zanzibar,  Waride Bakari Jabu.   (PICHA YA MAKTABA YA AFISI KUU CCM-ZANZIBAR)


NA Is-haka Omar, ZANZIBAR.

KATIBU wa NEC,  Idara ya Itikadi na Uenezi  CCM Zanzibar,  Waride Bakari Jabu amewataka viongozi na watumishi wa Chama na Serikali kubuni miradi na fursa zitakazosaidia kukuza kipato cha wananchi.

Alisema Viongozi Wakuu wa Kitaifa wamekuwa wakisisitiza suala la ubunifu kwa watumishi wa umma ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya watumishi hao kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa.

Kauli hiyo ameitoa  ofisini kwake Kisiwandui Mjini  Unguja, alieleza kwamba ajenda ya maendeleo ya nchi inamgusa kila mtu hasa watumishi waliopewa dhamana ndio wanaotakiwa kupanga mikakati ya kiuchumi kwa kuwahasisha wananchi watumie fursa zilizowazunguka zikiwemo ujasiriamali, kilimo, uvuvi na  ufugaji kujipatia kipato cha halali.

“Nchi yetu inapita katika kipindi kigumu cha kutoka katika uchumi wa Kati kwenda uchumi wa juu unaotegemea viwanda na masoko ya kimataifa ya ndani ya nchi, yote hayo yanahitaji ushirikiano wa kiutendaji miongoni mwetu.”, alisema Waride.

Pia alieleza kwamba wananchi wataendelea kuwa na imani na Chama cha Mapinduzi endapo serikali zote mbili zitaendelea kuwa  karibu na wananchi kwa kutatua kwa wakati kero na matatizo yanayowakabili.

Aidha alisema lengo la CCM ni kuendeleza utamaduni wa kuenzi demokrasia ndani na nje ya taasisi hiyo, sambamba na kuzishauri serikali zitekeleze sera za maendeleo kwa wananchi wote bila ubaguzi wa kisiasa na kidini.

Akizungumzia mipango ya chama hicho kwa sasa kuwa ni kufanikisha Uchaguzi wa ndani ya taasisi hiyo ambao kwa sasa unafanyika kwa ngazi za jumuiya na matawi yake ili kupata  viongozi na watendaji watakaotekeleza majukumu ya CCM kwa ufanisi ndani ya miaka mitano ijayo.

Katibu huyo alisema mpango mwingine ni kusimamia kwa nguvu zote utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho, sambamba na kuandaa mazingira bora ya kisiasa yatakayosaidia wananchi kuichagua CCM kwa kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Hata hivyo alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania  Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi zake za kupambana na vitendo vya ubadhirifu wa rasilimali za Taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.