Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi CCM Zanzibar Mhe. Najma Giga.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Zanzibar , Mustafa Rashid kumwalu  akimkabidhi Katibu wa Wazazi Wilaya ya  Kaskazini “B” Unguja ,  Bi.  Salma Shaibu, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo Bi.Najma Giga.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Zanzibar Nd. Mustafa Rashid Kumwala akitoa nasaha kwa  Makatibu wa Wilaya Sita za Umoja huo kabla ya kuwakabidhi komputa hizo.

Na.Is-Haka Omar.Zanzibar.
MAKATIBU wa Wilaya za Umoja wa Wazazi CCM Zanzibar  wamewashauri viongozi mbali mbali wa Chama cha Mapinduzi kuongeza  kasi  ya  utekelezaji wa ahadi walizotoa ndani ya taasisi hiyo ili kupunguza changamoto za kiutendaji.

Rai hiyo imetolewa  na baadhi ya Makatibu wa Wilaya Sita za Umoja huo Zanzibar mara baada ya kukabidhiwa Komputa zilizotolelewa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo, Bi. Najma Giga ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi alizowahi kutoa wakati wa  ziara zake  Visiwani humo.

Katibu wa  Wazazi  Wilaya ya  Amani , Bi.Mwanaisha  Ame Mohamed amesema upatikanaji wa vifaa hivyo utaongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya umoja huo kwani watakuwa na vitendendea kazi vya kisasa vitakavyorahisisha utendaji wa kazi zao.

Aidha  Katibu huyo amewataka  baadhi ya Wabunge, Wawakilishi na Madiwani  ambao bado hawajahamasika kuanza kutekeleza  ahadi zao kwa umoja huo na chama kwa ujumla  kufuata nyayo za  viongozi  wenzao walioanza kutatua kero za taasisi hiyo hatua kwa hatua.

“Huu ni wakati wa viongozi mbali mbali wa Chama chetu pamoja na jumuiya zetu kujitokeza kusaidia  baadhi ya Mikoa na Wilaya zenye upungufu wa vitendea kazi ili waweze kukamilisha shughuli za uchaguzi kwa ufanisi.”, alisema Katibu Mwanaisha.
Naye  Katibu wa Wazazi Wilaya ya  Wete Pemba, Bi. Mariam Ali Said  amemshukru Naibu 

Katibu Mkuu wa Wazazi Zanzibar kwa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo na kuongeza kuwa vifaa hivyo ni chachu ya  kumaliza  changamoto za kufuata huduma za  uchapaji wa nyaraka za kiofisi masafa ya mbali.

Akizungumza Kaimu Naibu Katibu Mkuu  Wazazi Zanzibar, Nd. Mustafa Rashid Kumwalu  kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo Bi. Najma Gina mara  baada ya kukabidhi  Komputa  hizo ametoa wito kwa watendaji wa umoja huo kutumia komputa hizo kwa matumizi yaliyokusudiwa  ili shughuli za kiutendaji zifanyike kwa wakati mwafaka.

Nd. Rashid  alieleza kuwa  lengo la umoja huo ni kuhakikisha watendaji wake wanapata vitendea kazi vya kisasa vitakavyosaidia  kutekeleza kwa wakati shughuli za kiutendaji  kwa lengo la kwenda sambamba na matakwa  ya Katiba ya CCM iliyofanyiwa mabadiliko miezi kadhaa iliyopita.

Aidha alisema Komputa zilizokabidhiwa mpaka sasa ni tisa  bado kumi kwa mujibu wa idadi ya komputa zilizoahidiwa kutolewa na Naibu katibu Mkuu wa Umoja huo, ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa kutoka ndani ya Umoja wa Wazazi Tanzania.

Komputa hizo zina thamani zaidi ya shilingi milioni Saba zimekabidhiwa kwa  Wilaya  6  za  Umoja  wa  Wazazi  CCM Wilaya ya Amani, Wilaya ya Mfenesini, Wilaya ya Kati, Wilaya ya Kaskazini “B”, Wilaya ya Wete na Wilaya ya Chake Chake Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.