-
|
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Tovuti: www.chragg.go.tz
|
Juni 19, 2017
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
THBUB
yalaani watu wenye ulemavu kupigwa na kudhalilishwa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
(THBUB) imepokea taarifa zinazohusu askari polisi kuwapiga na kudhalilisha watu
wenye ulemavu katika tukio lililotokea asubuhi ya Juni 16, 2017, Mtaa wa Sokoine
jijini Dar es Salaam.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
imefuatilia tukio hilo kwa kuzungumza na viongozi wa walemavu na mamlaka
husika, hususani Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam na kuelezwa
kuwa mnamo tarehe 16 Juni 2017 watu wenye ulemavu wapatao 200 wakiwa na vyombo
vya moto, vijulikanavyo kama “bajaji”, waliziba barabara ya Sokoine kwa madai
ya kutaka Mkurugenzi asikilize madai yao yahusuyo wenzao kukamatwa kwa
kuendesha vyombo vyao bila kufuata taratibu za sheria.
Taarifa za vyombo vya habari na mitandao
ya kijamii zilionyesha askari wa Jeshi la Polisi wakiwapiga watu hao wenye
ulemavu.
Pamoja na kwamba watu wenye ulemavu
walikiuka taratibu za sheria,
ni wazi kwamba wakati wa kuzuia uvunjifu
huo wa sheria, kulikuwa na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya watu
hao wenye ulemavu wakati wakikamatwa na kuingizwa kwenye magari.
Haki ya usawa mbele ya sheria kama
ilivyo kwa haki nyingine, inalindwa kisheria na hakuna mtu anayepaswa kuvunjiwa
haki zake wakati wa kutekeleza sheria. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania (1977) Ibara ya 13 (6) (e) ni marufuku kwa mtu kuteswa,
kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha. Haki hizi pia
zimeainishwa ndani ya mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo
Tanzania imeridhia.
Tume inapenda kulikumbusha Jeshi la
Polisi kwamba kukimbilia kuwapiga raia kila wanapoonekana kukinzana na sheria
ni matumizi mabaya ya madaraka yao. Ni wajibu wa polisi kulinda usalama wa raia
bila kuwadhalilisha, kuwatesa na kuwapiga. Matumizi ya nguvu kupita kiasi
wakati wa kutekeleza sheria ni uvunjifu wa sheria.
Pamoja na uvunjifu wa sheria uliotendwa
na watu wenye ulemavu siku ya tarehe 16 Juni, 2017, kitendo cha kuwapiga bila
kuwapa muda wa kutawanyika, au kutoa hoja za malalamiko yao kupitia kwa
wawakilishi wao ni kitendo cha kuwadhalilisha.
Hivyo basi, Tume inatoa wito kwa Jeshi
la Polisi:
1. Kuzingatia
kanuni, sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika utekelezaji
wa majukumu yake ya kila siku.
2. Kuwapatia
mafunzo ya mara kwa mara askari polisi na maafisa wake kuhusu haki za binadamu
na misingi ya utawala bora. Wakati wa kuratibu
na kushughulikia masuala ya maandamano na mikusanyiko ya raia.
3. Kuhakikisha
kuwa maafisa na askari wake hawatumii nguvu kupita kiasi wawapo katika
operesheni zinazohusu raia waliokusanyika kwa amani, na hususan watu wenye
ulemavu, ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
4. Mwisho,
Tume inatoa wito kwa raia kwa ujumla, wakiwemo watu wenye ulemavu, kwamba hamna
mwananchi au mtu yeyote aliye juu ya sheria, na kwamba njia bora ya kutatua kero
au matatizo yanayowakuta wananchi wakidai haki zao ni kwa kufuata taratibu za
sheria. Kwa hivyo, viongozi wa watu wenye ulemavu wafuate taratibu hizo
kufikisha hoja zao kwenye vyombo na mamlaka husika na siyo vinginevyo.
Imetolewa
na:
(SIGNED)
Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Juni 19, 2017
No comments:
Post a Comment