Habari za Punde

Watu Wenye Ulemavu Wametakiwa Kujengwa Uwezo Kukabiliana na Maafa.


Na.Said Abdurahaman. Pemba.
MKUU wa Wilaya ya Micheweni Ndg.Abeid Juma Ali, amezitaka taasisi  mbali mbali kuendelea kutoa  mafunzo ya kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kuweza kujikinga na majanga mbali mbali.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya siku moja juu ya kukabiliana na maafa kwa watu wenye ulemavu huko katika ukumbi wa “ZANGOG” Micheweni, mkuu huyo wa Wilaya alisema    mafunzo hayo yataamsha ari
kubwa kwa walengwa katika kukabiliana na maafa yatayoweza kutokea katika sehemu zao.

Alieleza  Wilaya ya Micheweni ni miongoni mwa Wilaya zenye watu wenye ulemavu,hivyo mafunzo hayo yametolewa muda muafaka kwa vile Wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na majanga mengi kama vile ukame,ajali za
baharini, mmong”onyoko wa ufukwe pamoja na uingiaji wa maji ya bahari katika maeneo ya kuishi na Kilimo.

“Kuweka mikakati ambayo itayalinda makundi maalum  sambamba na kuzilinda haki za binaadamu wakati wa maafa yanapotokea,au kabla ya kutokea ,”alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Mkuu  huyo wa Wilaya, alitoa wito kwa kamati za kukabiliana na maafa za Wilaya na  shehia za  Micheweni kuchukua stahiki za kujikinga na maradhi ya mripuko pamoja na kuwashajihisha wananchi kupambana na
maradhi ya kipindupindu.

“Pia natoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni kuweka mazingira safi pamoja na kuchemsha maji ya kunywa, kutumia dawa za kusafishia maji ,kuchimba na kutumia vyoo ili kuepusha kuenea kwa vinyesi,’alisema Abeid.

Aliwataka wafanyabiashara wa vyakula kuwa makini sana katika kuzingatia masharti ya afya wakati wanapotoa huduma kwa wananchi hasa katika kipindi hichi cha kuelekea katika shamra shamra za sikukuu ya Iddi –el- fitri.

Mkuu huyo wa Wilaya, aliipongoza Ofisi ya Makamo wa pili wa Rais kupitia kamisheni ya kukabiliana na maafa na Idara ya watu wenye ulemavu Pemba kwa kutoa mafunzo hayo kwa makundi maalum.

Kwa upande wake ,Ofisa Mdhamini wa Ofisi ya Makamo wa pili wa Rais, Ali Salim Mata, alisema   mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo yao kwa watu wenye ulemavu na kuwajengea uwezo kaatika nyanja tofauti.

Alieleza kuwa Ofisi yake tayari imeshatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu makusudi kuwapa uwezo na kuwajengea mustakali mzuri wa maisha yao pamoja familia zao zinazowategemea.

Nae, Mratibu wa kukabiliana na Maafa kutoka Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Pemba, Khamis Arazak Khamis, alisema kuwa tokea kuanza kutoa mafunzo hayo jumla ya watu wenye ulemavu wapatao 150 kwa Pemba
wameshapatiwa mafunzo.

Katika mafunzo hayo jumla ya washiriki 20 kutoka shehia mbali mbali za Wilaya ya Micheweni walishiriki ambapo jumla mada kuu nne ziliwasilishwa kwa walengwa hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.