Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Ujumbe wa Viongozi wa Manispaa ya Potsdam kutoka nchini Ujerumani

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akisalimiana na Meya wa Manispaa ya Potsdam Berlin Nchini Shirikisho la Ujerumani Bwana Jann Jackobs ambae yupo Zanzibar na Ujumbe wake kwa ziara ya Siku Tatu kwa mwaliko wa Uongozi wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar.
 Balozi Seif  Kulia akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Manispaa ya Potsdam  wa Mji wa Berlin Nchini Shirikisho la Ujerumani uliopo Zanzibar kwa ziara ya Siku Tatu.
 Meya wa Manispaa ya Potsdam Berlin Nchini Shirikisho la Ujerumani Bwana Jann Jackobs wa Tatu kutoka Kulia anayeuongoza Ujumbe wa Viongozi Sita wa Manispaa yake akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Wa kwanza kushoto ni Meya wa Manispaa ya Mjini Zanzibar Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Nd. Aboud Mohamed  Serenge.

Balozi Seif  Kati kati na Meya ya Manispaa ya Potsdam Bwana Jann Jackobs Kulia yake wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mjini ya Potsdan na bUle wa Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba ipo haja kwa  Miji ya Zanzibar na ule wa  Potsdam  wa Nchini Shirikisho la Ujerumani  kubuni miradi ya pamoja inayofanana  Kiuchumi  ili isaidie kunufaisha Wananchi wa Miji hiyo Miwili.

Alisema hatua hiyo itaendeleza ushirikiano wa Uhusiano wa muda mrefu uliopo baina ya Nchi za Miji hiyo  inayofanana Kisiasa na Kimazingira kutokana ya  Ujerumani Magharibi na Mashariki Kuungana pamoja na kuwa Taifa Moja Shirikisho kama zilivyo kwa Tanganyika na Zanzibar  ziliyounda Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa ushauri huo wakati akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Manispaa ya Potsdam  iliyopo Mkoa wa Brandenburg  Nchini Shirikisho la Ujerumani ukiongozwa na Meya wa Mji huo Bwana Jann Jackobs aliokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema faida ya ushirikiano baina ya Miji ya Zanzibar na Potsdam kwa kipindi kirefu imeanza kuleta matumaini hasa ikizingatiwa ile miradi iliyoanzishwa kwa pamoja baina ya pande hizo mbili ya Nyumba za Maendeleo za Kikwajuni 
       { Majumba ya Mjerumani } pamoja na uimarishaji wa Miundombinu ya Ujenzi wa Mitaro ya Maji Machafu katika Manispaa ya Zanzibar.

Balozi Seif  alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa upande wake itazingatia na kuona namna gani inaweza kusaidia nguvu katika  uratibu wa uendelezaji wa ushirikiano wa utendaji wa kila siku wa Miradi ya pamoja itakayoanzishwa na Miji hiyo miwili.

Amehimiza  umuhimu wa  kuendeleaza mabadilishano ya ziara za mara kwa mara kati ya Viongozi, Watendaji na hata Wananchi wa kawaida wa Miji hiyo ikilenga kudumisha  ushirikiano wa Kihistoria uliopo baina ya Ujerumani na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliuomba Uongozi huo wa Manispaa ya Potsdam unaoongozwa na Bwana Jann Jackobs kuwa Mbaalozi wazuri wa kuitangaza Zanzibar Kiuwekezaji Nchini Shirikisho la Ujerumani.

Alisema Zanzibar hivi sasa iko mbioni kuendelea kuimarisha miundombinu katika sekta ya Utalii inayotegemewa kuwa muhimili mkuu wa Uchumi wa Taifa fursa ambayo wawekezaji wa Ujerumani wanaweza kuitumia katika kuweka vitega uchumi vyao katika sekta hiyo.

Balozi Seif alisema Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea Zao la Karafuu ambalo limepitia katika mitihani mbali mbali katika vipindi tofauti kiasi kwamba mabadiliko ya soko la Dunia limeiwezesha Zanzibar wakati mwengine kusua sua katika ushumi wake.

Mapema Meya wa Manispaa ya Potsdam Bwana Jann Jackobs alisema mambo ya msingi ya ushirikiano kati ya Mji wa Potsdam na ule wa Zanzibar  yameshakubalika na tayari yanawekwa saini kipindi hichi kwa ajili ya utekelezaji wa pamoja.

Bwana Jackobs alielezea faraja yake kutokana na sekta ya Utamaduni na Utalii kuanza kuonyesha matumaini ya mafanikio hasa katika baadhi ya matamasha yanayofanyika moja kati ya pande hizo kushirikisha wadau wa sehemu zote mbili.

Hata hivyo Meya wa Manispaa hiyo ya Potsdan  alifafanua wazi kwamba  masuala ya mazingira na fursa za ajira hasa kwa Vijana yanakusudiwa kufanyiwa utaratibu wa utekelezaji wake katika kipindi kifupi kijacho ili kuja kusaidia kustawisha maisha ya Vijana wengi.

Manispaa ya Potsdam iliyomo ndani ya Mkoa wa Brandenburg Kilomita 15 Kusini Magharibi mwa Mji wa Berlin Nchini Shirikisho la Ujerumani ina wakaazi wapatao Laki 167,745  kwa mujibu wa sensa ya Watu ya Mwaka 2015 ikilinganishwa na Manispaa ya Mji wa Zanzibar yenye wakaazi Laki 223,000 kwa mujibu wa sensa ya Watu na Makaazi ya Mwaka 2012.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.