Habari za Punde

Mama Salma Kikwete awasisitiza wanamichezo pindipo wakihojiwa wajibu kwa kiswahili


Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Mke wa Rais wa awamu ya nne nchini Tanzania Mama Salma Kikwete amehimiza Wachezaji wa soka nchini wanapohojiwa na waandishi wa habari ikiwa nje au ndani ya nchi wazungumze Kiswahili na kufanya hivyo ni kudumisha Utamaduni wa Tanzania na si kama mtu anaezungumza Kiswahili kitupu  hajaenda shule.

Mama Salma ambae ni Balozi wa Kiswahili katika bara la Afrika ameyasema hayo asubuhi ya leo katika hafla maalum ya uzinduzi wa Makavazi na Jumuiya ya Watetezi wa Kiswahili Tanzania (WAKITA) iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) huko Vuga Mjini Zanzibar.

Mama Salma amesema tamko la Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Tanzania Dkt Harrison George Mwakyembe la kuwataka wachezaji wanapohojiwa wajibu kwa Kiswahili yeye amefurahi sana kwani huo ni uzalendo na njia moja ya kukuza Kiswahili.

“Nakumbuka hata juzi tu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo DK Harrison Mwakyembe alitoa tamko muhimu wakati anawapokea wachezaji wa timu ya Taifa wa mpira wa miguu, aliwataka wachezaji wote wanapohojiwa na Waandishi wa Habari wa ndani na nje ya nchi wawe wanajibu kwa lugha ya Kiswahili, tamko hili mimi nimelifurahia kwa kuwa limeweza kukuza na kuitangaza lugha yetu ya Kiwahili ndani na nje ya nchi”. Alisema Mama Salma.

Mwanzoni mwa mwezi huu wa July, 2017 kuliibuka mjadala kwa baadhi ya wapenzi wa soka nchini Tanzania baada ya Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania Elias Maguli kujibu kwa Kiswahili alipoulizwa swali kwa Kiengera na kituo kimoja cha TV huko Afrika ya Kusini baada ya kuibuka kuwa nyota wa mchezo kufuatia kufunga bao katika dakika ya 18 ya mchezo ambapo Stars waliichapa Afrika Kusini bao 1-0 katika Mashindano ya COSAFA CUP.

“Ahsante sana namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuaajilia kuweza kupata ushindi katika mchezo huu. Ulikuwa mchezo muhimu sana ila tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuweza kutoka na ushindi nawashukuru mashabiki waliojitokeza na kuweza kutushangilia na kutupatia nguvu”. Alisema Elius Maguli ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.