Habari za Punde

Mfanyabiashara Maarufu Zanzibar Ndg. Bopar, Akabidhi Samani kwa Ajili ya Skuli ya Maandalizi Kiombamvua Zanzibar.

Mfanyabiashara Maarufu Nchini Zanzibar Ndg.Said Nassor Bopar akizungumza wakati wa kukabidhi madeski na viti kwa ajili ya matumizi ya Wanafunzi wa Skuli ya Maandalizi Kiommbamvua hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Skuli hiyo. 
Mfanyabiashara Maarufu Nchini Nd. Said Nassor Bopar kushoto akimkabidhi Meza 100 na Viti 200 Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi kwa ajili ya Skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unaguja.
Wa kwanza kutoka Kulia ni Naibu Waziri wa Elimmu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Mmanga Mjengo Mjawiri.
Balozi Seif  kulia pamoja na Mfanyabiashara Said Nassor Bopar waliokaa kwenye Viti wakifurahia msaada wa Vikao hivyo wakati wa makabidhiano yaliyofanyika kwenye Skuli iliyobahatika kupata vifaa hivyo ya Maandalizi ya Kiombamvua.
Balozi Seif Kushoto akimkabidhi Meza na Viti Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Mmanga Mjengo Mjawiri kwa ajili ya Skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua.
Baadhi ya  Viti 200 vilivyotolewa Msaada na Mfanyabishara Said Nassor Bopar vikiwa ndani ya Darasa la Skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua iliyomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unaguja.
Baadhi ya Meza 100 zilizotolewa msaada na Mfanyabishara Said Nassor Bopar zikiwa ndani ya Darasa la Skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua iliyomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na Othman Khamis OMPR.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati  umefika kwa Wazazi wote Nchini kulazimika kupenda kuona Vijana wao wakati wote wanajishughulisha na masuala ya Taaluma  muda wote ambayo ndio kigezo pekee kitakachowasaidia katika maisha yao ya baadae.

Alisema Vijana lazima wapate Elimu iwe ya kawaida au hata ya ujasiri amali ilhali iambatane na mazingira na mfumo wa Kisasa unaokwenda na sayansi na Teknolojia ili ikidhi mahitaji wanayoyatarajia.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa nasaha hizo katika hafla fupi ya kukabidhi Meza 100 na Viti 200 kwa Skuli Mpya ya Maandalizi ya Kijiji cha Kiombamvua iliyopo Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Msaada huo wa Meza na Viti umetolewa na Mfanyabiashara Maarufu wa Uagiziaji wa Vyakula hapa Nchini Ndugu Said  Nassor Bopar ukiwa na thamani ya shilingi Milioni Tisa na Laki Tatu {9,300,000/-}.

Balozi Seif alisema kitu pekee kitakachomsaidia Kijana wa sasa kuweka kukidhi mahitaji yake ya maisha ni Elimu hasa ikizingatiwa kwamba fursa za ajira ndani ya Taasisi za Umma hivi sasa zimepungua kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi wanaomaliza masomo yao.

Hata hivyo Balozi Seif alisisitiza kwamba bado zipo fursa za ajira katika baadhi ya maeneo  ambazo upatikanaji wake unategema jitihada kubwa ya Mwanafunzi anayoichukuwa hasa katika eneo la fani ya Sayansi linaloonekana kuwa na Wataalamu kidogo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimshukuru  na kumpongeza Mfanyabiashara Said Nassor Bopar kwa jitihada anazozichukuwa za kuisaidia Jamii yake iliyomzunguuka hasa katika huduma za Kielimu na wakati Jamii inapokumbwa na Majanga mbali mbali.

Alisema wapo Wafanyabiashara wengi Nchini wenye uwezo na kipato kikubwa cha kusaidia Jamii na wakati mwengine changamoto za Wananchi na jamaa zao zimo ndani ya maeneo na Vijiji walivyozaliwa lakini bado wamekuwa wazito wa kusaidia kupunguza changamoto hizo zinazowakwaza Wananchi.

Balozi Seif  alifahamisha kwamba changamoto ya Vikalio vya Wanafunzi bado inaathiri Skuli nyingi hapa Nchini jambo ambalo Serikali Kuu ililaimika na kufikia uamuzi wa kuunda Mfuko Maalum wa Madeski ili kukabiliana na kadhia hiyo inayoleta usumbufu kwa wanafunzi walio wengi Nchini.

Aliwataka Wanafunzi kuvitunza vifaa hivyo na kuwaagiza Walimu na Wazazi wasimamie vyema watoto wao katika matumizi bora ya vifaa hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu ujao.

Akigusia suala la Amani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuwasisitiza Wananchi wote Nchini kuitunza hazina hiyo inayowapa fursa nzuri ya kuendelea na harakati zao za kimaisha za kila siku.

Balozi Seif Ali Iddi alisema wapo baadhi ya Wanasiasa Nchini wameanza ishara za kuitiribua Amani hiyo wakati Jamii kipindi hichi imeshajielekeza katika njia ya kujiletea maendeleo baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu.

Mapema akitoa shukrani kwa niaba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mheshimiwa  Mmanga Mjengo Mjawiri alisema Vijana lazima wajengwe katika misingi imara ya Kitaaluma.

Mheshimiwa Mjawiri alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha malengo ya Vijana hao yanafanikiwa na kutimia.

Naye akitoa salamu katika hafla hiyo ya makabidhiano ya Meza na Viti Mfanyabiashara Said Nassor Bopar  alisema mchango huo wa Meza na Viti anaoendelea kutoa ni ahadi aliyoitoa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein karibu Miezi michache iliyopita.

Nd. Bopar alisema katika ahadi yake alijitolea kuchangia Vikalio 600 kwa skuli mbali mbali za Zanzibar zinazokumbwa na upungufu huo ambapo vikalio  450 vimenza kusambazwa katika Skuli za Mwanakwerekwe, Muembe Makumbi na Kiomba Mvua kwa Unguja na Vikalio 150 kwa Skuli za Pemba.

Skuli ya Maandalizi ya Kiombamvua imejengwa na Mradi wa Hoteli ya Kimataifa ya Sea Cliff iliyopo katika Kijiji cha Kama katika azma ya Uongozi wa Hoteli hiyo wa kujiwekea mpango na utaratibu wa kusaidia harakati za Kiuchumi na Maendeleo ya Wananchi wa Vijiji vinavyoizunguuka Hoteli hiyo.

Jumla ya Wanafunzi 90 wa elimu ya maandalizi watapata elimu katika Skuli hiyo yenye Madarasa Mawili ambayo ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi Milioni Sabini {70,000,000/-}.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.