Habari za Punde

GEP WAaiomba Serikali Kuwa Karibu Nao Kuzalisha Ajira Kwa Wingi.

Na.Bakari Mussa. Pemba.

Muungano wa Vikundi vya Ushirika na Saccos (GEP), ulioko katika Jimbo la Gando Mkoa wa Kaskazini Pemba, wanaiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuwa karibu nao ili kuzalisha ajira kwa wingi ili kuondowa msongamano wa vijana wanaosubiri ajira Serikalini ambazo ni chache.

GEP, ilianzishwa mwaka 2011 , ukiwa na muungano wa Vikundi 53 vya Ushirika na Saccos ,ikiwa na Wanachama 948 wakiwemo Wanawake 330 na wanaume 618, kwa lengo la kuzalisha ajira kwa vijana , akinamama naWajane ili waweze kupambana na Umaskini kupitia sekta hiyo ya Ushirika.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi , Katibu wa Muungano huo Hemed Khamis Ibrahim , huko  Kizimbani Wete alisema walianzisha kikundi hicho kwa fedha za kuchanga wenyewe ambapo walikusanya kiasi cha Tshs,37 Milion kwa lengo la kuzalisha ajira kwa vijana lakini hadi muda huu hawajapata msaada wowote kutoka taasisi yoyote pamoja na kupeleka baruwa katika maeneo tafauti.

Alisema katika muungano wao walikusanya Wanaushirika wa fani mbali mbali ikiwemo Kilimo cha mbaoga mboga ambacho kimeonekana kuwa na Soko kubwa Kisiwani Pemba, Ufugaji , kazi za mikono na Green House ili kuwapatia ajira vijana ambao wamekuwa wakikaa vinarazani ama kuzurura ovyo wakisubiri ajira kutoka Serikali na hatimae kujiingiza katika matendo maovu.

Alifahamisha tokea kuanza kwa Kikundi hicho kumekuwa na mafanikio makubwa kwani tayari walishazalisha ajira nyingi zikiwemo za ujasiria mali kwa Vijana na ajira kwa akinamama ambao tayari wameanza kuona matunda ya ajira hizo .

Hata hivyo wameanza na mradi wa kuongezea mazao thamani kwa kuzalisha Tomato Souce, ili Tungule zinazozalishwa na wanavikundi zinapobakia kuuzwa zinaingizwa katika mashine ambayo ipo ndani ya Ushirika huo kwa uzalishaji mwengine.

“Tokea kuanza kwa Muungano wa vikundi hivi, tumeshatowa ajira nyingi za aina mbali mbali na baadhi ya Watu ambao walijifunza taaluma hizo sasa hivi wanafaidika nazo,na kujipatia ajira zao ingawaje kuna changamoto mbali mbali tunazokabiliana nazo ikiwemo masoko kwa baadhi ya bidhaa wanazozalisha,” alifahamisha Hemed.

Katibu huyo , alieleza pamoja na mafanikio hayo lakini wamekuwa na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo ikiwemo ukosefuwa mali ghafi za baadhi ya miradi, utaalamu wa Green House , na ukosefu wa vifungashio vya baadhi ya bidhaa na nyenzo.

Hata hivyo aliwataka Vijana ambao hadi sasa hawajaamuwa kuingia katika miradi ya Uzalishaji kufika katika Ofisi zao kwa lengo la kujipatia utaalamu wa uzalishaji wa mambo mbali mbali na kuingia katika harakati za mapambano ya Umaskini kupitia sekta ya ushirika.

Kwa upande wake Mwanachama wa Ushirika huo, Fatma Seif Khamis, ambae anajishuhulisha na utengenezaji wa Sabuni, Mikoba , na Domet,alisema ni kweli muungano wa vikundi hivyo GEP, umewainuwa akinamama na Vijana mbali mbali wa Jimbo hilo baada ya kupatiwa mafunzo lakini tatizo linalowakabili sasa hivi ni Soko kwa baadhi ya bidhaa wanazozalisha.

Alifahamisha wamekuwa wakitengeneza Mikoba inayotumia Punje za aina mbali mbali lakini malighafi hiyo huipata Tanzaniabara kwa gharama kubwa na wanapotengeneza na kuuza mnunuzi anaona ni bei kubwa.“Tumekuwa tukiuza mikoba kwa bei ya Tshs, 50,000/= hadi 60,000/= ,nah ii inatokana na upatikanaji wa  mali ghafi tunavozipata na huku tukiwa hatuna fedha za kununulia vifaa kwa wingi tukawa navyo ofisini ,” alilalamika Mjasiriamali huyo.

Nao watengeza achari ya ndimu,  Sabubi ya Unga na Tomato Souce, bibi Ghanii Ali Bakar, Mariamu Ali Hamad, walisema kuwa baadhi ya bidhaa zimekuwa na Soko hususan la ndani kama vile za kilimo , lakini bidhaa nyengine zimekuwa na shida kwa vile mali ghafi wanazipata kwa bei ya juu kutoka Tanzaniabara.

Kwa upande wake Msaidizi Mrajis kutoka Idara ya Vyama vya Ushirika Pemba, Abdi Hamza Maalim,alisema taasisi binafsi zinamchango mkubwa katika kuleta maendeleo kwao wao na Taifa kwa ujumla iwapo zitaamuwa kukapamoja na kuanzisha taasisi kubwa ya kifedha kama vile Benk.

Alieleza ni vyema kwa Waushirika kuwa wabunifu katika uzalishaji wa bidhaa ili kuendana na mahitaji ya soko jambo ambalo litakuza vipato vyao ingawaje malengo yao yako kitu kimoja .

Aliwataka Wanasaccos, kuwatayari kupokea mabadiliko ndani ya sekta hiyo kwa kujiunga na Saccos ya Wilaya ili kujenga nguvu ya pamoja na kupata fedha kubwa za kuendeleza shughuli zao.

Hivyo aliwasihi WanaSaccos kuwa na utamaduni wa kukopa na kurejesha kwa wakati sambamba na kuzifanyia miradi ili ziweze kuwafaidisha na wengine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.