Habari za Punde

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tano Ilivyojidhatiti Kuboresha Huduma za Bandari.

Na Ismail Ngayonga. Maelezo Dar es Salaam.                                                                                                     
SERIKALI ya Awamu yaTano inaingia katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpangowa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017– 2020/2021) unaojikita katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.

Lengo kuu la Mpango huo ni kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati inayoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kutumia rasilimali zilizopo na hivyo kuchangia katika kukuza Pato la Taifa.

Ili kufikia adhma, Serikali imechukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuongeza ufanisi na kukuza sekta ya uchukuzi ikiwemo na ujenzi na ukarabati wa miundombinu na huduma za barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege.

Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ilitayarisha Mpango Kamambe wa Miaka ishirini wa Kuendeleza Bandari (Ports Master Plan, 2008-2028) ukilenga kuzifanya bandari zote nchini kuongeza mchango katika maendeleo ya nchi na kuongeza usafirishaji wa mizigo kwa nchi jirani zinazotumia bandari zetu.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa anasema ili kukabiliana na upungufu wa shehena za mizigo, TPA imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kufungua ofisi za huduma za bandari katika miji ya Lubumbashi, (DR Congo), Lusaka  (Zambia), Kigali (Rwanda) na Bujumbura (Burundi).

Aidha Profesa Mbarawa anasema Mamlaka ya Bandari TanzaniA (TPA) pia imefungua na kuanzisha wakala wa Mamlaka huko Kampala, Uganda na kuimarisha usalama wa mizigo bandarini na kutoa huduma za bandari kwa saa 24 kwa siku kwa wiki.

Kwa mujibu wa Waziri Mbarawa anasema katika mwaka 2016/17 Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kuboresha utendaji wa bandari za mwambao wa maziwa makuu ikiwemo kukamilika kwa jengo la ghorofa 35 za kuwaweka pamoja wadau muhimu wanaotoa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Jengo hilo lilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe.Joseph Kabila Kabange tarehe 4 Oktoba, 2016 na linatarajia kuanza kutumika mweziMei, 2017” anasema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa anasema Serikali pia imekamilisha upanuzi wa barabara ya kuingia lango Na. 4 katika Bandari ya Dar es Salaam Oktoba, 2016 pamoja na kukamilisha ukarabati na upanuzi wa barabara ya kuingia lango Na. 5 katika Bandari ya Dar es Salaam Aprili, 2017.

Profesa Mbarawa anasema mwezi Januari 2017, Serikali ilianza Awamu ya kwanza ya ujenzi wa bandari kavu ya Ruvu, iliyolenga kuongeza uwezo wa bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mizigo na kupunguza msongamano wa mizigo na malori bandarini na Jijini la Dar es Salaam.

Waziri Mbarawa anasema Serikali pia ilikamilisha ujenzi wa matishari mawili yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja katika Ziwa Nyasa, matishari hayo yaliendelea kufanyiwa majaribio kabla ya kuanza kutumika rasmi mwezi Mei, 2017.

Anaongeza kuwa Serikali imekamilisha maandalizi ya ujenzi wa gati za Nyamisati, katika bahari ya Hindi; Ndumbi katikaZiwa Nyasa; Lagosa, Kibirizi na Kabwe katika Ziwa Tanganyika, ambapo ujenzi huo unatarajiwa kuanza Juni 2017 na kukamilikaJuni 2019.

Anasema kuwa Wizara yake pia inaendelea na kazi ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Karema, Kigoma ili kuunganishwa na BandariyaKalemie, iliyopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kazi za ujenzi zinatarajiwa kuanza Septemba 2017.

Mbarawa anasema Serikali kupitia TPA pia inaendelea na maandalizi ya msingi ya ujenzi wa bandari ya Mbegani, Bagamoyo, ambapo kukamilika kwa ujenzi wa bandari hiyo kutaongeza uwezo wa kuhudumia shehena ziingiazo nchini na ziendazo nchi jirani za Burundi, DR Congo, Malawi, Rwanda, Uganda na Zambia.

“TPA inaendelea na jitihada za kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kuzingatia ujenzi wa reli mpya (Tanga – Arusha – Musoma) na zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaoathirika limefanyika kwa jumla ya wananchi 2,188, ambapo jumla ya Tsh Bilioni 47.584 zimelipwa hadi Machi, 2017” anasema Profesa Mbarawa.

Aidha Profesa Mbarawa anasema Serikali pia inaendelea na zoezi la upembuzi yakinifu la maandalizi  ya ujenzi wa gati la Chongoleani (Tanga) kwa ajili ya kupokelea mafuta kutoka Uganda, litakalokuwa na  uwezo kuhudumia Meli zenye uzito wa hadi tani 250,000.

Kuhusu Bandari ya Mtwara, Profesa Mbarawa anasema Serikali inaendelea na upanuzi wa bandari hiyo ili kuifanya kuwa ya kisasa kwa ajili ya kuhudumia shehena za gesi; mafuta; madini na mazao ya kilimo kutoka katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara unaojumuisha mikoa ya kusini na nchi za Malawi na Zambia.

Anasema upanuzi wa Bandari hii utahusu ujenzi wa magati manne (4) ambayo yatajengwa kwa awamu, ambapo Awamu ya kwanza itahusu ujenzi wa gati moja lenye urefu wa mita 350 ambapo Kampuni ya China Railway Construction Company (CRCC) ilisaini Mkataba wa ujenzi tarehe 4 Machi, 2017.

Profesa Mbarawa anasema mwezi Agosti 2016, Serikali ilianza kutumia mfumo wa wa TANCIS wa Mamlaka ya Mapato umeanza kutoa huduma ambapo makusanyo yote ya tozo za huduma za bandari (wharfage) kwa mizigo inayoingia nchini (Local and transit goods) kwa bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Stephen Ngatunga anasema katika  kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha sekta ya usafirishaji nchini, TAFFA imeandaa kongamano la siku 4 la wadau zaidi ya 350 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

“Katika kongamano hilo kutakuwa na wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi amabao watatoa mada katika nyanja mbalimbali zinazohusu bandari na usafirishaji wa mizigo” anasema Ngatunga.
Anaongeza kuwa kongamano hilo pia litaiwezesha Tanzania kupata fursa ya kukuza uchumi wake kupitia sekta ya usafirishaji na usambazaji na baadhi ya maswala kama uboreshaji wa bandari na kuifanya iwe ya kisasa, kuongeza vyanzo vya mapato na changamoto zingine zitapewa kipaumbele kwenye majadiliano.

Kwa mujibu wa Ngatunga anasem kongamano hilo linafanyika katika wakati ambao wafanyabiashara wa Kitanzania wanahitaji uelewa zaidi pamoja na maarifa kuhusu njia bora za utendaji kazi ikiwemo matumizi ya kidigitali  inatawala.

Akifafanua zaidi Ngatunga anasema kongamano hilo pia litawezesha ukuzaji wa biashara Tanzania uhusani usafirisaji na uhifadhi wa mizigo hasa katika nchi zisizo na bahari kama Burundi, DRC, Rwanda, Zambia, Malawi na Uganda na kufanya Mataifa hayo kuweza kutumia bandari ya Dar es Salaam kama njia ya usafirishaji mizigo.

“Hii ni mara ya kwanza kwa sisi kuwa wenyeji wa mkutano huu wa kiulimwengu. Tunafurahia sana kupata fursa hii ambayo itaitangaza Tanzania kama kituo kizuri cha usafirishaji na kuongeza wigo na mahusiano ya kibiashara kwa mawakala, kampuni za bima, mtoa huduma,  mtoa bidhaa ama afisa biashara kutengeneza wigo” alielezea Ngatunga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.