STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 20.08.2017
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka viongozi
wa Majimbo wakiwemo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwaeleza wananchi juhudi
zinazochukuliwa na Serikali yao katika kuwapelekea huduma za maendeleo ikiwemo
huduma ya maji safi na salama.
Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kukagua
kisima cha maji ikiwa ni miongoni mwa visima 8 vilivyopo katika kijiji cha
Bumbwisudi, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi, kisima hicho ni
kisima kikubwa kati ya visima vya hapa nchini ambacho kinatoa maji mengi lita
zaidi ya laki2 kwa saa.
Dk. Shein alieleza kuwa ni vyema Wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi nao wakatumia fursa ya kuweleza wananchi juhudi za Serikali kwani
baadhi yao hawazijui juhudi hizo, kwani kazi kubwa inafanywa na Serikali yao katika
kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa mbali ya mradi huo ambao una visima
tisa ambavyo 8 kati ya hivyo viko katika eneo hilo la Bumbwisudi pia, kuna
miradi mingi ikiwemo ule wa JICA, ule ambao fedha kutoka Serikali ya India na
mengineyo, juhudi zote hizo ni kuhakikisha changamoto ya huduma ya maji
inapatiwa ufumbuzi katika kipindi kifupi kijacho.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar
(ZAWA), Dk. Mustafa Ali Garu alimueleza Dk. Shein kuwa kisima hicho ndicho
kisima kikubwa kilicho na uwezo wa kutoa maji mengi kupeleka katika kituo cha
Welezo na hatimae kupeleka katika mji wa Zanzibar ambapo kwa hivi sasa hatua
inayoendelea ni kuweka pampu.
Alisema kuwa katika eneo hilo la Bumbwisudi pekee
yake pamechimba visima vinane na cha tisa kimechimbwa huko Mwembemchomeke mbali
na visima vyengine 4 vya zamani na kulifanya eneo hilo la Bumbwisudi peke yake
kuwa na visima 12.
Meneja wa Mradi huo Aboozar Sadeghi alimueleza Dk.
Shein kuwa Mradi huo unatarajiwa kukamilika Januari mwakani.
Wakati huo huo, Dk. Shein aliweka jiwe la msingi
Tawi la CCM Bumbwisudi alipongeza juhudi za wanaCCM pamoja na viongozi wao wa
Jimbo kwa kujenga jengo hilo jipya la Tawi na kueleza kuwa hatua hiyo ni
miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambayo
yeye chini ya chama hicho anaisimamia.
Dk. Shein ambaye pia, ni Makamo Mwenyekiti wa CCM
Zanzibar aliwaeleza wanaCCM hao kuwa kazi iliyombele yao hivi sasa ni
kutekeleza ahadi walizoziahidi katika
Ilani hiyo yab Uchaguzi huku wakihakikisha wanakilinda chama chao sambamba
na kuyalinda Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Makamo huyo wa CCM Zanzibar alitoa wito kwa
wanaCCM kuwa wamoja na kushirikiana kwa pamoja ili kukiimarisha chama chao
ambacho hakitakiwa kuwa na makundi kwani tokea zama za cha ASP kulikuwa hakuna makundi.
Mapema Dk. Shein aliliwekea jiwe la msingi jengo
jipya la skuli ya Msingi Kihinani katika Jimbo la Mfenesini na baadae aliwahutubia
wananchi wakiwemo wanafunzi wa skuli hiyo na kuwaeleza azma ya Serikali
anayoiongoza katika kuendeleza ujenzi wa madarasa mapya ya skuli za Zanzibar
pamoja na thamani yakiwemo madawati kwa mashirikiano ya wananchi na viongozi
wao.
Alieleza kuwa katika kuhakikisha changamoto ya
upungufu wa madawati inapatiwa ufumbuzi tayari TZS Bilioni 4 kwa awamu ya
kwanza zimeshakusanywa kwa ajili ya ununuzi wa madawati na baadae awamu ya pili
itafuata hiyo yote ni kwa kutambua kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha na nyenzo
kubwa katika maisha ya mwanaadamu.
Alitumia fursa hiyo kutoa pongezi maalum kwa
wanafunzi wa kike ambao ni wengi katika skuli hiyo na kuwaeleza kuwa juhudi
wanazozichukua ni muhimu katika kuwaletea maendeleo wao wenyewe na nchi yao
kwani katika kipindi cha hivi karibuni wanafunzi wa kike wamekuwa wakifanya
vizuri katika masomo yao hasa ya sayansi.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wananchi
pamoja na wananfunzi waliohudhuria katika hafla hiyo kuwa mafanikio yote yaliopatikana
katika sekta ya elimu yanatokana azma ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964
chini ya jemedari Marehemu Mzee Abeid Amani karume ambae alitangaza elimu bure.
Akieleza historia ya elimu hapa nchini kabla ya
Mapinduzi Dk. Shein alisema kuwa wanyonge katika kipindi hicho walikuwa
hawapati elimu kwani haikuwa rahisi na walitakiwa kulipa fedha ambazo
hawakuzimudu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Khadija Bakari alieleza kuwa jumla ya
TZS milioni 24 zimetumika katika ujenzi wa madarasa hayo 4 ambazo ni michango
ya wananchi na Serikali imetoa TZS milioni 45, huku akieleza azma ya Wizara
yake kuzimaliza skuli 288 zilizoanza kujengwa na wananchi katika Bajeti yao ya
mwaka huu.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment