STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 19.08.2017
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua uwamuzi wa makusudi kukiunganisha
Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi kuwa ni Tawi la Chuo Kikuu cha Taifa
Zanzibar (SUZA), ili chuo hicho kizidi kupata hadhi na kutambulikana Kitaifa na
Kimataifa.
Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kuweka
jiwe la msingi jengo la Chuo Cha Utalii, kilichopo Maruhubi mjini Unguja
ambacho kwa hivi sasa chuo hicho ni Tawi la Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar
(SUZA).
Akiwahutubia wanafunzi wa Chuo nje ya jengo hilo
jipya la Chuo cha Maendeleo ya Utalii, Dk. Shein alisema kuwa kwa vile jengo
hilo tayari limeshafikia asilimia 50 ya ujenzi kunatoa matumaini makubwa katika
kukamilisha mradi huo mkubwa ambao utazidisha azma ya Serikali anayoiongoza
katika kuimarisha sekta ya utalii.
Aliongeza kuwa hatua hiyo unakipa hadhi na sifa
kubwa chuo hicho ambacho kwa siku za mbele kitaweza kujiendesha wenyewe na kuwa
Chuo Kikuu cha Utalii kwani vyuo vingi vilianza hivyio na kutolea mfano Chuo
Kikuu cha Muhimbili na kile cha Sokoine Morogoro ambavyo vilikuwa ni Matawi la
Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa lengo kubwa la
Serikali katika kuchukua juhudi hizo ni kutaka vijana wake wasome na kusisitiza
kuwa kazi hiyo kubwa ilibuniwa na Chama Cha Mapinduzi CCM katika Ilani yake ya Uchaguzi.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa
sekta ya utalii hapa Zanzibar ambao umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa uchumi
wa Zanzibar kwa kuingiza fedha za kigeni kwa asilimia 80 na kuchangia pato la
Taifa kwa asilimia 27.
Alieleza kuwa jina la Zanzibar linajiuza kutokana
na utalii na kuwaeleza wanafunzi hao
kuwa hawajakosea kuingia katika kada hiyo ya elimu.
Akitoa maelezo kwa Rais wa Zanzibar Dk. Shein, Meneja
Mkuu wa Mradi wa ujenzi huo Yusuph Msafiri Mlimakifi alieleza kuwa ujenzi huo una eneo la mita 5000 na utakuwa
wa ghorofa tatu na unatarajiwa kugharimu TZS Bilioni 5.2 ambao mradi ho ni
mashirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB).
Mhandisi huyo alieleza kuwa tayari asilimia 50 za
ujenzi huo zimeshafikiwa na matarajio kumalizika kwake ni Disemba mwaka huu
huku akieleza kuwa mbali ya jingo hilo kusaidia katika kutoa mafunzo kwa chuo
hicho pia litakuwa ni eneo la biashara kwa chuo hicho.
Alieleza kuwa jengo hilo litakuwa na ukumbi wa mikutano ambao utakuwa na ukubwa wa
kuingiza watu wapatao 400, mkahawa utakaochukua watu 400 ambao utakaokuwa wazi
wakati wote, ukumbi wa kusomeshea utakaochukuwa wanafunzi 150, jiko la kisasa
la kufundishia na kwa shughuli za biashara pamoja na vyumba 9 vya kulaa vyenye
sifa ya Hoteli ya nyota 4.
Wabunifu na Wasimamizi wa ujenzi wa jengo hilo
ni Kampuni ya Onspace Consult kutoka
Dar-es-Salaam na mjenzi ni Kampuni ya Humphrey kutoka Arusha.
Mapema Dk. Shein alifika eneo la Kilimani mjini
Unguja kwa ajili ya kukagua mradi wa upandaji wa Mikoko pamoja na Ujenzi wa
Matuta ya kuzuia Mmongonyoko wa fukwe na kupongeza kwa hatua zilizofikiwa
katika kuendeleza miradi hiyo ya ujenzi.
Akipata maelezo kutoka kwa Katibu wa Taasisi ya
ZACEDY Jamali Khamis alisema kuwa mradi wa upandaji wa mikoko ni mwa mwaka
mmoja na mikoko inayopandwa ni ile ya aina ya mchu ambayo ndio inayokubali
katika eneo hilo.
Alisema kuwa mradi huo utasaidia katika kupambana
na mabadiliko ya tabia nchi katika eneo hilo la kilimani na tayari wameshapanda
35,000 ambapo changamoto kubwa wanayoipata ni kuwa bado jamii haijaona umhimu
wa mradi huo hivyo kuna haja ya kuelemishwa kwani kuna baadhi ya watu hupita
katika maeneeo hayo wanayopanda mikoko ambayo bado ni michanga licha ya
kuwashirikisha wananchi katika mradi huo.
Nae Meneja Mkuu wa Mradi wa ujenzi wa Matuta ya
kuzuia mmongonyoko wa fukwe Bernard Odhuno alieleza kuwa mradi huo unaendelea
vizuri na wanatarajia kujenga matuta 5 katika eneo hilo kwa ajili ya kuzuia
mmongonyoko huo na wanatarajia kumaliza mnamo mwezi wa Novemba mwaka huu.
Alisema kuwa tayari mradi kama huo wameshaukamilisha huko Kisiwa Panza kisiwani Pemba ambapo
alieleza kuwa mradi huo uko chini ya Ofisi ya Makamo wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Usaidizi wa Miradi
(UNOPS).
Wakati huo huo, Dk. Shein alilifungua Tawi la CCM
la Muembe Matarumbeta katika Jimbo la Jangombe na kupongeza ujenzi huo wa tawi
la kisasa huku akisisitiza haja kwa wanaCCM kuendelea kukitumikia chama chao.
Dk. Shein ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa
CCM Zanzibar alieleza kuwa tawi hilo
litawasaidia kwa kiasi kikubwa wanaCCM katika kufanya shughuli zao wkani Tawi ndio kiini cha siasa ya chama
hicho kwani ni lazima litumike katika kufanya kazi za chama.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza matumaini
yake kwa viongozi wa Jimbo hilo kuwa karibu na wanachama wa chama hicho
kutokana na kuwemo kwa Ofisi zao ndani ya Tawi hilo.
Mapema Dk. Shein alipokea taarifa ya Mkoa huko
ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, Kikwajuni mjini Unguja na baada ya kusomwa taarifa hiyo
na Mkuu wa Mkoa Ayoub Mohammed, Dk. Shein alieleza umhimu wa kuhakikisha yale
yote yalioahidiwa na CCM yanatekelezwa, hivyo ziara yake hiyo imekusudia kwenda
kushuhudia azma hiyo.
Aliongeza kuwa matumaini yake makubwa kuwa
utekelezaji wa Ilani ya Uchgauzi ya mwaka 2015-2020 itavuka asilimia 95
zilizofikiwa katika utekelezajiw a mwaka 2010-2015.
Dk. Shein, pia, alitumia fursa kurejea kauli yake
ya kuwataka Mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kushiriki ziara
hiyo isipokuwa wale wenye shughuli maalum ambao wamemtaarifu kwani hiyo ni
ziara ya kazi na si ya mchezo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment