Habari za Punde

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                               25.08.2017
---
MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameweka jiwe la Msingi katika Tawi la CCM Tibirinzi na kusisitiza kuwa siasa sio ugomvi.

Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la Tawi hilo la Tibirinzi ambalo lilitiwa moto mnamo mwaka 2015 na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa chama kimoja wapo cha upinzani hapa Zanzibar.

Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, alieleza kuwa siasa ya vyama vingi wameitaka wenyewe wananchi hivyo jambo la kushangaza kuwa baadhi ya wanasiasa wamelichukulia jambo hilo kuwa ndio njia moja wapo ya kujengeana chuki, kutukanana na kutovumiliana.

Aliongeza kuwa kwa vile chama cha CCM ndio fundi wa siasa tokea ASP na TANU kitaendelea kuvisomesha vyama vyengine vya siasa nini maana ya siasa na chama cha siasa kinatakiwa kiwe vipi katika suala zima lakuvumiliana, kutojengeana chuki.

Dk Shein alisema kuwa si vyema siasa ikawagawa watu na kuwafanya wakaishi kwa uadui na badala yake watu wanatakiwa kuishi kwa kushirikiana, kupendana na kustahamiliana kwani siasa ni uvumilivu na sio ugomvi.

“Mimi nawaambia wana CCM wenzangu, mfanye kazi za chama vizuri bila woga na muhakikishe mnafanya vikao vya mara kwa mara katika Tawi letu hili, ili muweze kuleta maendeleo katika chama chetu”alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kitaendelea kustahamili na kuwa na subira lakini ifike wakati na vyama vyengine vitambue kuwa subira nayo huwa na mipaka kwani lengo la chama ni kuwapelekea maendeleo wananchi.

Alieleza kuwa kitendo cha kulichoma moto Tawi hilo la CCM kimeonesha wazi kuwa baadhi ya vyama vya siasa bado ni wanagenzi wa siasa na dhana yao kuwa siasa ni chuki, ugomvi na uhasama hali inayoonesha kuwa bado hawajaujua umuhimu na malengo ya kuwepo kwa vyama vingi.

Hivyo, Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alisisitiza kuwa tukio hilo la kuchomewa Tawi lao huilo la CCM liwe la mwisho huko akisisitiza kuwa CCM inafuata miongozo ya dini ikiwa ni pamoja na kukubali suluhu na kutambua kuwa pande mbili zikifarakana ni vyema zikakaa pamoja na kushauriana sambamba na kuwa na subira na kuvumiliana.

Sambamba na hayo, Dk. Shein ambaye ndio alilolijenga Tawi hilo baada ya kutiwa moto na mnamo tarehe 31 Mwezi Mei mwaka huu alifika Tawini hapo kwa ajili ya kulikagua na kujionea hujuma zilizofanywa za kutiwa moto tawi hilo.

Katika kuhakikisha Tawi hilo linakuwa la kisasa na wanachama wake wanaendelea na shughuli zao za chama, aliwataka viongozi wa CCM Mkoa huo wakiwemo Wawakilishi pamoja na Mbunge wa Viti Maalum kulimalizia kwa kuliweka milango, shata za madirisha na umeme.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alitoapongezi zake kwa Rais Dk. Shein kwa juhudi zake hizo za kulijenga upya tawi hilo na kuwa la kisasa huku akiahidi kuwa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui itatoa msaada wa viti kwa ajili ya Tawi hilo.

Mapema wanachama wa CCM wa tawi hilo walitoa pongezi za pekee kwa Dk. Shein kwa kulijenga upya tawi lao hilo baada ya kuchomwa moto na kuteketezwa mnamo Machi 10 mwaka 2016 na kupelekea uharibifu mkubwa.

Mapema Dk. Shein alifika Kiziwani Shungi na kuzindua uchumaji wa karafuu katika Wilaya ya Chake Chake ambapo alishiriki kikamilifu katika uchumaji wa zao hilo katika  shamba la mikarafuu la Bi Fatma Hamad Said ambalo kwa hivi sasa linashughulikiwa na Muhene Ali Salum lenye ukubwa wa eka 4.2 na mikarafuu 197.

Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali zisizorejesheka Pemba, Saidi Juma alisema Wilaya ya Chake Chake imeshakodisha mashamba 85 yenye thamani ya TZS milioni 298.3.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.