Habari za Punde

Vikundi vya Ushirika vinaweza kuwaletea maendeleo wananchi

Na Shaibu Kifaya----Mkoani.

Jamii imeshauriwa kujitokeza kwa wingi katika kujiunga na vikundi vya ushirika  ili kuweza kujikwamua na umasikini na kuondokana na hali duni ya utegemezi wa kiuchumi na kuweza kujiletea maendeleo katika familia zao.

Hayo yalielezwa   na  mshikafedha  wa kikundi cha ufugaji nyuki cha TUSHIKAMANE , Moh’d Khamis Amani, kilichopo katika kijiji cha Likokuu Shehia ya Chokocho Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, wakati alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

 Alisema kuwepo kwa vikundi kama hivi kutatoa  muamko mkubwa kwa vijana ambao bado hawajataka kujishuhulisha na kazi yoyote hivyo kujikusanya pamoja kutawasaidia   kujiendeleza katika shuli zao mbali mbali za  kimaisha na kuweza kujipatia kipato cha halali.

Akizungumzia changamoto wanazozipata  Mwenyekiti wa kikundi hicho  Omari Hamadi Abdala ,alisema  jambo kubwa linalowarejesha nyuma ni kuweka mizinga yao kwa muda mrefu  bila ya kupata mafanikio yoyote .  

Aliongeza kuwa bado hawajapata soko la uhakika la kuuzia asali na kulazimika kutafuta soko katika Wilaya ya Chake Chake,  ambako nako bado hakujawa na uhakika wa kuuza kwa bei yenye kuleta tija.

“ Tunaiomba Serikali kuharakisha kuwapatia soko hilo kama ilivyo katika mipango yao, ili tuweze kupambana na Umaskini unaotukabili “ alisema Mwenyekiti huyo.

Na kwa upande wake,    Said  Makame Ayubu, ambae ni miongoni mwa wana kijiji cha  Likokuu  shehia ya chokocho ,alisema kuwepo kwa kikundi kama hichi cha ufugaji nyuki kunatoa muamko mkubwa kwa vijana ambao bado hawajataka kujishuhulisha na kazi yoyote.


Kikundi hicho  cha ufugaji nyuki cha TUSHIKAMANE kilianzishwa mwaka 2005 kikiwa na wanachama  sita wakiwa ni wanawake wawili na wanaume wane na walikuwa wakitumia zana zao za asili za kutegea Nyuki  hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.