Habari za Punde

MAKAMU WA RAIS AZINDUA MIRADI KATIKA WILAYA YA KUSINI PAMOJA NA KUZINDUA MPANGO MKAKATO WA KAMISHENI YA KISWAHILI YA AFRIKA MASHARIKI 2017-2022

Na.Mwandishi OMR.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa mkoa wa Kusini Unguja kutunza miradi na kuitumia kwa manufaa ya wote.

Makamu wa Rais aliyasema hayo leo wakati wa Ufunguzi wa Ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Kizimkazi ambao umefadhiliwa na Ubalozi wa Japan.

Mhe. Samia aliwashukuru Ubalozi wa Japan kwa kufadhili ujenzi wa Uboreshaji wa Mazingira ya Elimu katika Wilaya ya Kusini ambao umegharimu dola za kimarekani  laki moja na elfu kumi na mbili  na mia nane na arobaini na tano (112,845) ambazo ni sawa na takribani ya shilingi milioni mia mbili arobaini na saba (247) .Awali Ubalozi wa Japan ulitoa dola za Kimarekani elfu ishirini na nane mia nane na sitini (28,860) takribani shilingi milioni sitini na moja za kitanzania kujenga uzio wa shule  ya Msingi Muyuni .

Makamu wa Rais alimshukuru sana Balozi wa Japan kwa ufadhili huo ambao umeendelea kuimarisha urafiki na mahusiano kati ya nchi mbili hizi, aliwataka wananchi wa Wilaya ya Kusini kutilia mkazo masuala ya elimu na kutunza miradi yote ili inufaishe na vizazi vijavyo.

Makamu wa Rais pia aliwapongeza viongozi wa halmashauri ya wilaya ya kusini kwa kusimamia vizuri fedha za ufadhili na kufanikisha kukamika kwa ujenzi wa miradi kama ilivyopangwa na kukamilika mapema zaidi .

Kwa Upande wake Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida alisema amefurahishwa  na Ushirikiano  alioupata kutoka kwa Makamu wa Rais na wakazi wa Wilaya ya Kusini Unguja na kuahidi kwamba Japan itaendelea kusaidia maendeleo ya Tanzania ambapo alisema ufunguzi wa miradi ya leo ni hatua nyingine kubwa ya kuimarisha  ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi mbili hizi, Japan na Tanzania.

Wakati huo huo
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amezindua Mpango Mkakati wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki 2017-2022 wakati wa Kongamano la Kwanza la Kimataifa  la Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ambapo aliwataka Viongozi wan chi za jumuiya hiyo kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwani lugha hii inatuunganisha watu wa Afrika Mashariki, pamoja na kuzindua rasmi pia Makamu wa Rais alifungua Ofisi ya Kamisheni ya Kiswahili  ya Afrika Mashariki mjini Unguja, Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.