Habari za Punde

Maoni ya kamati ya Sheria, Utawala bora na Idara Maalum kufuta sheria ya kufuta Mahakama ya Kadhi na kuanzisha upya Mahakama ya Kadhi

HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA SHERIA, UTAWALA BORA NA IDARA MAALUM KUHUSU MSWADA WA SHERIA YA KUFUTA SHERIA YA MAHAKAMA YA KADHI NAM. 3 YA 1985 NA KUANZISHA UPYA MAHAKAMA YA KADHI NA KUWEKA MASHARTI MENGINE YANAYOHUSIANA NA HAYO

Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu ambae ametutujaalia neema ya uhai na uzima mpaka kuweza kutekeleza majukumu yetu ya kila siku, namuomba azidi kutukirimu neema hizo ambazo kwa hakika sote ni wahitaji kwake.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kukushukuru na kukupongeza wewe pamoja na wasaidizi wako, Mhe. Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Baraza kwa namna mnavyoliendesha Baraza kwa umahiri mkubwa, namuomba Mwenyezi Mungu awazidishie hekma na busara katika jukumu lenu la uongozi ili tuweze kutekeleza vyema wajibu wa chombo hiki.
Mheshimiwa Spika;        Aidha, nitumie fursa hii kuishukuru Wizara ya Nchi OR – Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa juhudi zao kubwa walizozifanya katika kuufanyia marekebisho Mswada huu katika Nchi yetu ambayo asilimia kubwa ya wakaazi wake ni Waislamu.
Vile vile, pongezi za pekee ziende kwa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar pamoja Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuona umuhimu wa kufanya marekebisho ya Sheria hii ambayo imekuwa ikileta utata mkubwa katika utekelezaji wake. Pia, nimshukuru mheshimiwa Waziri kwa kuwaongoza vyema watendaji wake kwenye kikao chetu cha kujadili Mswada huu kwa kujibu hoja zetu vizuri na kuweza kuzitolea ufafanuzi zaidi, na hivyo tukaweza kupata uwelewa mkubwa juu ya dhamira ya kuletwa kwa Mswada huu.
Mheshimiwa Spika; hatahivyo, siktokuwa mwingi wa fadhila ikiwa sitowashukuru Wadau wote walioshiriki katika kuuchangia Mswada huu kwa juhudi zao walizoonyesha katika kufanikisha Mswada huu wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Mahakama ya Kadhi Nam. 3 ya 1985 na Kuanzisha Upya Mahakama ya Kadhi na Kuweka Masharti mengine yanayohusiana na hayo.. Kwani sote ni wajibu wetu kuweza kuuchangia kwa maslahi ya watu wetu, lakini pia, kwa faida ya Waislamu wote waishio Zanzibar.
Mheshimiwa Spika; kwa dhati kabisa, Kamati inawashukuru wadau hao kwa michango yao mizuri ambayo naamini itasaidia sana katika kuufanya Mswada huu kuwa bora zaidi. Vilevile, napenda kuwahakikishia kwamba maoni na ushauri wao umezingatiwa na Kamati wakati ilipokaa na Wizara ili kupatiwa ufafanuzi kuhusu Mswada huu.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila iwapo sitotambua mchango wa Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Baraza, ambapo Kamati yetu iliwaalika katika kikao kilichojadili Mswada huu na Wizara.
Mheshimiwa Spika;  Kamati yetu inakubaliana moja kwa moja na kufutwa kwa Sheria ya zamani na kuanzishwa upya Sheria ya Mahakama ya Kadhi kutokana na changamoto mbali mbali ambazo zimekuwa zikijitokeza katika utekelezaji wa Sheria hiyo. Vile vile, Sheria hii inaanzisha Fungu la Bajeti na Fedha za Mahakama ya Kadhi (vote), jambo ambalo ni muhimu sana katika uendeshaji wa Taasisi hii na pia, itaweza kupunguza changamoto nyingi ambazo zimewakabili kutoka na uhaba wa fedha za uendeshaji.
Mheshimiwa Spika; pia, niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati hii pamoja na Makatibu wangu kwa mashirikiano makubwa ambayo wanatupatia katika kuendesha shughuli zote za Kamati yetu.
Mheshimiwa Spika; sasa naomba uwatambue Wajumbe hao kama ifuatavyo:-

1.      
Mhe. Machano Othman Said
Mwenyekiti
2.     
Mhe. Mwantatu Mbaraka Khamis
Makamu Mwenyekiti
3.     
Mhe. Nadir Abdul – latif Yussuf
Mjumbe
4.     
Mhe. Wanu Hafidh Ameir
Mjumbe
5.     
Mhe. Saada Ramadhan Mwenda
Mjumbe
6.     
Mhe. Ali Khamis Bakari
Mjumbe
7.     
Mhe. Suleiman Makame Ali
Mjumbe
8.     
Nd. Ali Alawy Ali
Katibu, na
9.     
Nd. Haji Jecha Salum
Katibu

Mheshimiwa Spika; naomba sasa uniruhusu nieleze baadhi ya marekebisho na mapendekezo mbali mbali ambayo Kamati yetu imeyafanya na pia, naomba kuwatanabahisha Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako tukufu ya kwamba, hotuba hii inatoa ufafanuzi wa baadhi tu ya vifungu ambavyo vimependekezwa na kufanyiwa marekebisho na Kamati, hivyo maelezo zaidi ya mapendekezo hayo yamo katika muhtasari wa marekebisho yetu ambayo Waheshimiwa Wajumbe tayari mmeshapatiwa.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya  Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum ilikutana na Wizara ya Nchi OR - Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora siku ya Jumatano, tarehe 20 Septemba, 2017 na kuupitia Mswada huu kifungu kwa kifungu pamoja na kufanya marekebisho ya kimantiki na kisarufi. Vile vile, Wizara iliwasilisha katika kikao hicho Mapendekezo ya Marekebisho ya Mswada huu katika vifungu vifuatavyo: 2, 3, 5, 8, 10, 11, 20, 28 na 33.

Aidha, Kamati iliyapokea na kuyajumuisha katika Marekebisho ya Kamati ambayo yamewasilishwa ndani ya Baraza baada ya kuvifanyia marekebisho machache pamoja na kufuta marekebisho ya kifungu cha 20.

Mheshimiwa Spika, naomba niende moja kwa moja katika baadhi ya vifungu ambavyo Kamati imevifanyia marekebisho, kama ifuatavyo:-

Kifungu cha 2, tafsiri ya “Mahakama ya Kadhi” imerekebishwa ili iende sambamba na tafsiri iliyopo katika Mswada wa Kiingereza na baada ya marekebisho hayo itasomeka kama ifuatavyo:

“Mahakama ya Kadhi inajumuisha Mahakama ya Kadhi wa Rufaa na Mahakama ya Kadhi wa Wilaya, kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 3 cha Sheria hii”.

Mheshimiwa Spika, aidha, tafsiri ya “Mdaawa” imeongezwa kama ifuatavyo: “Wadaawa maana yake ni mdai na mdaiwa katika shauri la Mahakama ya Kadhi”. Kuongezwa kwa tafsiri hii kumetokana na kwamba neno hili limetumika sana katika Mswada huu, hivyo, italeta utekelezaji bora kwa watumiaji.

Mheshimiwa Spika; kifungu cha 5(1) aya (a), (b), (c), (d), (e) na (f) zimefutwa na kuandikwa upya kwani maelezo yake yapo tofauti na Mswada wa Kiingereza na uhalisia wake. Baada ya marekebisho hayo, aya hizo zitasomeka kama ifuatavyo:-

(a)      ndoa, talaka na mambo yote yanayohusiana na hayo;
(b)     nafasi ya wanandoa;
(c)      matunzo na malezi ya watoto;
(d)     wakfu au amana za kidini, hiba na msaada;
(e)      wasia na urithi;
(f) mgawanyo wa mali ya wanandoa pale ambapo kuna uchangiaji halisi.
  
Mheshimiwa Spika, aya (d) imeongezwa katika kifungu cha 8(5) ambacho kinaongeza sifa ya ziada na muhimu katika uteuzi wa Kadhi Mkuu na Naibu Kadhi Mkuu kitakachosomeka kama ifuatavyo:-

“(d) mwenye taaluma na uzoefu wa dini ya kiislamu unaolingana na sifa za kuteuliwa kuwa Kadhi”.

Mheshimiwa Spika, marekebisho mengine yaliyopendekezwa na Kamati ni kukifuta na kukiandika upya kifungu cha 9(2) kwa ajili ya kuweka muda wa ukomo wa kuongezwa muda wa utumishi kwa Kadhi Mkuu na Naibu Kadhi Mkuu. Kamati inaona kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwekwa kwa muda huo. Mapendekezo ya Kamati ni:-
“Bila ya kujali masharti ya kifungu kidogo cha (1) cha kifungu hiki, Rais anaweza kuongeza muda wa Utumishi wa Kadhi Mkuu na Naibu Kadhi Mkuu kama atakavyoona inafaa lakini muda huo hautazidi miaka mitano (5)”.

Mheshimiwa Spika, Vile vile, Kamati ilifanya marekebisho katika kifungu cha 13(3) kwa kufuta maneno “Qur’an na Sunnah” yaliyojitokeza mwishoni mwa kifungu hicho na badala yake kuweka maneno “Sheria ya Kiislam”. Kamati imeona ni vyema kuyafuta maneno hayo kwasababu tayari yamejumuishwa katika tafsiri ya “Sheria ya Kiislam”.

Mheshimiwa Spika, nina imani kuwa Wajumbe wa Baraza hili wamepata fursa ya kuupitia kwa kina Mswada huu, na kubaini maeneo kadhaa ya kuishauri Serikali kuhusu utekelezaji bora wa Sheria inayotarajiwa kutungwa.

Mheshimiwa Spika; Hivyo ni matumaini ya Kamati kwamba, Wajumbe wa Baraza hili Tukufu, watauchangia, wataujadili ipasavyo na hatimae kuupitisha Mswada huu ikiwa ni sehemu ya jukumu la Baraza, na hatimae kuipa fursa Serikali kutekeleza sehemu ya jukumu lake la utekelezaji wa Sheria itakayotungwa.

Mheshimiwa Spika, Nachukuwa fursa hii kuwashukuru kwa dhati Wajumbe wote wa Baraza lako tukufu kwa umakini wao na usikivu wa hali ya juu waliouonesha wakati wa uwasilishaji wa hotuba hii. Kamati inawaomba waujadili kwa kina na hatimae kuupitisha kwa lengo la kuuboresha kwa ajili ya kuweka misingi mizuri ya Mahakama ya Kadhi katika kuendesha majukumu yao ya kuwahudumia Waislamu wa Nchi hii.

Mheshimiwa Spika, NAOMBA KUWASILISHA.

Ahsante,



…………………………..
(Machano Othman Said)
Mwenyekiti,
Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum,
Baraza la Wawakilishi,

Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.