Habari za Punde

Wasaidizi wa sheria wataka watambuliwe na sheria za nchi


NA HAJI NASSOR, PEMBA

WADAU wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, wamezishauri mamlaka husika kuangalia uwezekano, kwa wasaidizi wa sheria waliopo majimboni, kutambuliwa kisheria, ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.

Walisema kazi wanayoifanya ambayo ndio azma ya serikali ya kuwasaidia wananchi katika kutambua haki na wajibu wao, ni nzuri ingawa bado sheria za nchi haziwatambui rasmi, hivyo wakati sasa wakati umefika.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, walisema kwa vile kazi hiyo imekuwa ikiwasaidia wananchi kupata haki zao, lazima mihimili ya nchi iwatambue rasmi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, Sheihan Mohamed Sheihan alisema kabla ya kuwepo kwa wasaidizi wa sheria, ilikuwa wananchi hawana uwelewa wa kuwasilisha mashauri yao, kituoni hapo.

Alisema ingawa kwa sasa hali inayonyesha tofauti, maana wapo wananchi wakati mwengine wanaowaelimisha Polisi, juu ya taratibu na haki zao wanapokuwa kituoni hapo.

“Mimi nasema hawa wasaidizi wa sheria, lazima sasa kuwe na sheria maaluma inayowatambua, maana kazi wanayoifanya ndio ile ile inayofanywa na vyombo vyengine, sasa kusiwe na sababu ya kutotambulika rasmi”,alisema.

Nae Sheha wa shehia ya Mtemani Jimbo la Wete, Mrisho Juma Mtwana ‘magogo’ alisema lazima kwa serikali kuandaa sheria ya haraka, ili kuwatambua wasaidizi wa sheria, waliopo majimboni.

“Sasa hata sisi masheha wakati mwengine huwa wanatueleza taratibu na kazi zetu hawa wasaidizi wa sheria, maana wao wamepata uwelewa wa sheria, sasa ni jambo jema, wakatambulika rasmi”,alishauri.

Msaidizi wa sheria wa Jimbo la Chakechake Riziki Hamad Ali, alisema kama zipo taasisi zimeshatengenezewa sheria  hakuna sababu na wao wasitambuliwe na sheria.

“Mimi naamini kama tukitambulika rasmi na sheria, hata vile vyeti vya uhitimu tunavyopewa, vinaweza kutusaidia katika kupata ajira, maana tunakuwa na uwelewa wa sheria.

“Mwanafunzi wa skuli anatambuliwa na sheria, karafuu zina sheria yake, Ukimwi unasheria yake, magazeti, barabara, waajiriwa serikali, hivyo ni vyema na sisi wasaidizi wa sheria, tukatengenezewa sheria yetu”,alieleza.

Kwa upande wake Katibu tawala wilaya ya Micheweni Hassan Abdalla Rashid, alisema iwapo wasaidizi wa sheria watatambuliwa na sheria za nchi, itakuwa ni jambo jema maana sasa watakuwa wanafanyakazi zao kwa upana.

Hata hivyo alisema, tayari binafsi ameshawahi kushiriki katika vikao vya awali vinavyoonyesha kuwa, sheria ya kuwatambua wasaidizi wa sheria inakuja.

“Ijapokuwa wanavitambulisho vya kazi zao, lakini haitoshi lazima na sheria za nchi ziwatambue, ili wawe na mapana ya kazi yao, tena popote pale”,alifafanua.

Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC taswi la Pemba Fatma Khamis Hemed, alisema umuhimu wa wasaidizi kutambuliwa upo, moja ikiwa ni kufanya kazi zai zao bila ya wasiwasi.

“Kitu kinapokuwa kinatambuliwa na sheria za nchi, basi ndio kipo kisheria, lakini kinyume chake ndio hakitambuliwa kisheria, hivyo lazima serikali ipeleke msaada wa sheria hiyo”,alifafanua.

Afisa Upelelezi wa Dawati la jinsia na watoto kutoka jeshi la Polisi Mkoa wa kusini Pemba, Hamad Fakih Ali, alisema wasaidizi wa sheria, wamekuwa wakiwasaidia katika mapambano dhidi ya kesi za udhalilishaji.

“Sisi wamekuwa wakituibuliwa hata kesi za udhalilishaji, maan kama Jeshi la Polisi, hatupo kila pahala, lakini kuanzishwa kwa mpango wa wasaidizi wa sheria, sasa afadhali twashirikiana vyema”,alifafanua.

Omar Juma Ameir mkaazi wa shehia ya Sizini alisema, yeye alifanikiwa kurejeshewa fedha zake shilingi zaidi ya 1,000,000 (milioni moja), alizotapeliwa baada ya kuuziwa kiwanja kilichokwisha uzwa.

“Mimi nilimtumia msaidizi wa sheria wa Jimbo la Winwgi, na sikwenda Polisi, maana ningechukuwa muda mrefu, lakini alipoitwa tu na msaidizi wa sheria huyo alienitapeli, alikubali kunilipa mara mbili, bila ya mashaka”,alifafanua.

Mratibu wa wasaidiz wa Sheria Pemba, Safia Saleh Sultan alisema wasaidiz hao wa sheria, husoma kwa muda wa miaka miwili mambo mbali mbali, ikiwa ni pamoja na sheria ya ushahidi, mfumo wa sheria wa Afrika wa Mashairiki, Katiba na mfumo sheria, Sheria ya mikataba, sheria ya jinai, sheria ya madhara, sheria ya madai na sheria ya utawala


Mradi wa wasaidizi wa sheria ambao upo chini ya Kituo cha Huduma za Sheri Zanzibar ZLSC, kwa kisiwani Pemba pekee tayari wapo wasaidizi wa sheria 96 ambao wameshahitimu na wapo kila Jimbo la uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.