Habari za Punde

MKUTANO WA MWENYEKITI WA BODI YA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA (TPC), MENEJIMENTI NA VIONGOZI WA VYAMA VYA WAFANYAKAZI, DAR ES SALAAM

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Elia Madulesi (wa pili kushoto), akizungumza wakati akimkaribisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPC, Deo Kwiyukwa (wa pili kulia), kuzungumza katika mkutano wa Mwenyekiti wa Bodi ya shirika, Dk. Harun Kondo (kulia), Menejimenti na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wa shirika hilo, Dar es Salaam leo. (Picha zote na Kassim Mbarouk)
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPC, Deo Kwiyukwa, akizungumza katika mkutano huo na kisha kumkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Dk. Harun Kondo (katikati), kuzungumza na Menejimenti na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wa shirika hilo, jijini Dar es Salaam leo. 
Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Dk. Harun Kondo (katikati), akizungumza na Menejimenti na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wa TPC, jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPC, Deo Kwiyukwa na kulia ni Kaimu Katibu wa Shirika, Zuhuru Pinde.
Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Dk. Harun Kondo (wa pili kulia), kuzungumza na Menejimenti na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wa TPC, jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPC, Deo Kwiyukwa na kulia ni Kaimu Katibu wa Shirika, Zuhuru Pinde. 
Baadhi ya viongozi wa Vyama vya wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), wakiandika maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Dk. Harun Kondo, wakati akizungumza nao pamoja na Menejimenti ya TPC, jijini Dar es Salaam leo. 
Baadhi ya viongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) na wa Vyama vya wafanyakazi wa shirika hilo, wakisikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Harun Kondo, katika mkutano wao huo, Dar es Salaam leo. 
Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Dk. Harun Kondo, akifafanua jambo wakati wa akizungumza na Menejimenti na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wa TPC, Dar es Salaam leo. Kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPC, Deo Kwiyukwa.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wakichukua habari wakati Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Dk. Harun Kondo, alipokuwa akizungumza katika mkutano huo. 
Baadhi ya viongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) na wa Vyama vya wafanyakazi wa shirika hilo, wakisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Harun Kondo, katika mkutano wao huo.  
Baadhi ya viongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) na wa Vyama vya wafanyakazi wa shirika hilo, wakifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Harun Kondo, katika mkutano huo. 
Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Dk. Harun Kondo (kushoto), akifafanua jambo wakati akizungumza na Menejimenti na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wa TPC, jijini leo. Kushoto ni Meneja Mkuu Uendeshaji wa shughuli za shirika, Hassan Mwang'ombe na wa pili ni Meneja Mkuu wa TPC, Macrice Mbodo. 
Baadhi ya viongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) na wa Vyama vya wafanyakazi wa shirika hilo, wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Harun Kondo, katika mkutano huo.  
Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Harun Kondo, akifafanua jambo katika mkutano huo.  
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Elia Madulesi (kulia), akiteta jambo na Ofisa Uhusiano wa shirika, Joseph Ngowi.
Baadhi ya viongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) na wa Vyama vya wafanyakazi wa shirika hilo, wakisikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Deo Kwiyukwa katika mkutano huo, leo Dar es Salaam.  
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPC, Deo Kwiyukwa, akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari, wakati wa mkutano huo.
Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Dk. Harun Kondo (katikati), akizungumza na Menejimenti na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wa TPC, jijini Dar es Salaam leo. 


MAELEZO YA MWENYEKITI WA BODI WAKATI WA KIKAO NA MENEJIMENTI NA VIONGOZI WA VYAMA VYA WAFANYAKAZI TAREHE 14 SEPTEMBA 2017

NDUGU POSTAMASTA MKUU

MENEJIMENTI YA SHIRIKA LA POSTA

NDUGU VIONGOZI WA VYAMA VYA WAFANYAKAZI

·         Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutuwezesha kujumuika hapa na kushiriki pamoja katika kikao hiki.

·         Pia napenda niwakaribishe na niwashukuru wote mliofanikiwa kufika katika kikao hiki.
Kama mtakumbuka ni takriban miezi sita tangu tulipokutana tena hapa ikiwa ni kikao changu cha kwanza kabisa kukutana na nyie viongozi wa vyama vya wafanyakazi

Ari mliyonionyesha wakati wa kikao hicho ndiyo imenisukuma kutaka tena leo hii kuzungumza na nyie ikiwa ni kama mwaka mmoja tangu Bodi yetu ilipoteuliwa.

Kikao cha wakati ule kilikuwa ni pamoja na kukumbushana juu ya wajibu wa Bodi na Menejimenti ya shirika la posta , na pia ililenga kujitambiulisha na kufahamiana


Ndugu viongozi wa wafanyakazi

Kama mnavyojua shirika letuliko kwenye kipindi cha mabadiliko,
·         Napenda niwaeleze wazi kabisa kuwa mimi binafsi na Bodi ya Wakurugenzi tunayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Shirika ambao ni zaidi ya 1000 mnashiriki na kuchangia mabadiliko ya kiutendaji ndani ya Shirika hili.

·         Kupitia Wizara yetu mama ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nao wanadhamira hiyo.

·         Baadhi yetu tumeshuhudia dhamira hiyo njema wakati Mheshimiwa Waziri Prof. Makame M. Mbarawa na aliyekuwa Naibu Waziri wake Edwin A. Ngonyani walipokutana na Menejimenti na Wafanyakazi na pia kutembelea baadhi ya sehemu za kazi katika Posta yetu Kuu ya Dar es Salaam yaani GPO.

·         Kwa bahati nzuri hii ndio dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli ya kuhakikisha Taasisi na Mashirika yake ikiwa na pamoja na Shirika la Posta yanashiriki na kuchangia jitihada za kuleta maendeleo ya haraka.

·         Napenda Shirika letu hili lisiwe kikwazo bali kichocheo cha kufanikisha jitihada hizi. Tusiwaangushe Watanzania.


Ndugu viongozi wa wafanyakazi

>   Mimi binafsi nimekuwa nakutana na viongozi wa Wizara mara kwa mara kuzungumza juu ya changamoto mbalimbali ambazo shirika linakabiliana nazo ili kupata ufumbuzi wake ,Wizara imekuwa ikinipa ushirikiano mkubwa.

Pia nimekuwa na vikao vya mara kwa mara na Wizara ya Fedha kupitia kwa Msajili wa Hazina kutatua baadhi ya changamoto zinazolikabili Shirika zikiwemo madeni na kodi mbalimbali ambazo tunadaiwa.

Bila shaka mtakuwa mna taarifa kuwa baadhi ya madeni ya pensheni za wastaafu wa Jumuia ya Afrika Mashariki tuliyokuwa tunaidai Serikali tumeshaanza kurejeshewa.  


1.   CHANGAMOTO ZA SHIRIKA

Kama mnavyofahamu mbali na changamoto za mtaji pia shirika linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ;
Ø  Mapungufu katika kusimamia nidhamu, uadilifu, weledi na upimo wa utendaji, kubadilisha mitizamo ya Wafanyakazi, udhibiti wa mapato na matumizi ya Shirika.

Ø  Kurekebisha maslahi ya Wafanyakazi na kuwaendeleza ili kumudu kazi katika mabadiliko ya teknolojia.

Ø  Kuboresha miundombinu ya Shirika la Posta ikiwa ni pamoja na miliki.

Ø  Kulifanya Shirika kuwa Taasisi shirikishi katika kutekeleza na kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa.


Ø  Kuongeza ufanisi wa kiutendaji ili kukuza wingi na ubora wa biashara pamoja na kuhakikisha kunakuwepo faida kwa Shirika na kutoa gawio kwa Serikali.

Ø  Kupanua mtandao na wigo wa soko ili wananchi wote hadi huko vijijini wapate kufikiwa na huduma bora na za kisasa.

Ili kufanikisha azma hiyo ,Bodi imechukuwa hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kusimamisha ,kuachisha na kufukuza wale wote wanaoonekana ni kikwazo cha juhudi hizo.

2. FURSA ZA SHIRIKA
Ndugu viongozi wa wafanyakazi,
Pamoja na changamoto zilizopo, lakini tunazo fursa nyingi tu za kupanua na kuboresha biashara zetu. Mheshimiwa Waziri alisisitiza sana juu ya jambo hili:-
·         Miliki za Shirika ikiwa ni pamoja na majengo na viwanja vilivyoko kwenye “prime areas” za miji mbalimbali hapa nchini. Ingawa hili lina changamoto ikiwa ni pamoja na ukosefu wa rasilimali fedha,kuendelea kwa shirika kuwa chini ya uangalizi, lakini kwa kiwango kikubwa ni fursa nzuri na yote haya yanafanyiwa kazi na serikali yetu.

·         Mtandao wetu mpana wa kitaifa wa ofisi zipatazo 400 zilizounganishwa na ofisi 660,000 duniani unawezesha kupanua na kuboresha zaidi biashara zetu ndani na nje kwa minajili ya kukuza mapato.

·         Matumizi mazuri ya TEHAMA yanawezesha kuanzisha biashara mpya za kimtandao kama Hybrid mail, Digital Stamps, na huduma jumuishi mahali pamoja (Unified Community Services) au huduma Express.

·         Ushindani licha ya kuwa ni changamoto lakini kwa upande mwingine ni fursa nzuri tu ya kuboresha, kupanua na kubuni huduma mpya.

3. MALENGO YA SHIRIKA
Ndugu viongozi wa wafanyakazi,
·         Napenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha wajibu wetu wa uwajibikaji kwa watumishi wa kada zote ndani ya Shirika kwa kujenga nidhamu ya kazi, kujituma, kuheshimu kanuni na taratibu, kuongeza ubunifu na kufanya kazi kwa ufanisi wenye tija. Lazima tubadilishe mitazamo (mind sets) yetu ili tuondokane na kuendesha shughuli kwa mazoea yaani “business as usual”.

·         Natambua kuwa maslahi ya viongozi na ya wafanyakazi siyo ya kiwango cha kuridhisha lakini lazima mzingatie kuwa maslahi bora kwa watumishi yanatokana na ongezeko la ufanisi na tija.

4. MAFANIKIO YA BODI.
Napenda kuwajulisha kuwa katika kipindi hiki kifupi kwa ushirikiano mzuri uliokuweko kati ya  Bodi na menejimenti kunekuwa na mengi kama yafuatavyo;

 (a)Kuanzishwa kwa kampuni tanzu 4
Bodi imeridhia kuanzishwa kwa kampuni tanzu mpya nne ambazo zimekwishasajiliwa kisheria.kampuni hizo ni;
i.       Posta Logistics Ltd,
ii.     Posta Freight and Forward,
iii.    Posta Microfinance,
iv.    Posta Digital.
Kampuni hizo zitakapoanza kufanya kazi zitakuwa kichocheo cha kuliingizia mapato shirika na hivyo kuwezesha kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuboresha zaidi mazingira ya kazi.

(b)Kuridhia muundo mpya wa shirika
Bodi imeridhia mapendekezo ya muundo mpya yaliyowasilishwa na menejimenti. Muundo huo umewasilishwa kwenye mamlaka ya juu ili uweze kuridhiwa na kuanza kutumika mapema iwezekanavyo.

Lengo la muundo huo ni kuboresha utendaji , kuondoa urasimu na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
(C) Miliki za shirika
kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu bodi iteuliwe kwa kushirikiana na menejimenti na watendaji wake shirika limeweza kuweka kumbukumbu sahihi za  viwanja/ miliki za shirika zipatazo 198,ambazo kati ya hizo hati 154 zimekwishapatikana na nyingine zinafuatiliwa  kwa karibu .
(d)Ukusanyaji madeni
Bodi ilipoanza kazi yake rasmi  mwishoni mwa mwaka jana ilikuta shirika linadai madeni ya zaidi ya shilingi bilioni ‘10’.bodi kwa kushirikiana na menejimenti ya shirika iliweka mkakati wa pamoja ambao uliwezesha kukusanya madenini ya shilingi bilioni 7.5 kwa kuwatumia wafanyakazi wa ndani.
(e) Jitihada za kubana matumizi
·         Shirika lilipitia upya mikataba ya upangaji na kuirekebisha na kuhakikisha kuwa kila mpangaji ana mkataba sahihi na pia matumizi yasiyo na tija yameendelea kupunguzwa.
·         Pia bodi ilipitia zabuni mbalimbali na kubaini zabuni zilizokuwa na dosari na kuzirekebisha moja wapo ikiwa ni ile ya valuation ambayo ilikuwa shilingi milion 245 na kuweza kupunguza hadi milion 160.

·         Pia shirika lilifanikiwa kutengeneza muundo mpya kwa kutumia wataalamu wake wa ndani  na kuweza kuokoa shilingi milioni 700 zilizokusudiwa kutumiwa kwa ajili hiyo kwa kutumia wataalam kutoka nje.
(f) Kurejeshewa madeni ya pensheni
Baada ya juhudi za Bodi na Menejimenti kufanyika Serikali imeridhia kurudisha madeni tuliyokuwa tunaidai Serikali ya shilingi bilion 3.9 ambayo ni deni la pensheni za wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki.

Mazungumzo kati ya Shirika la Posta na Serikali yamewezesha kufikia makubaliano ambapo kwa sasa pensheni hizo zitakuwa zinalipwa na Serikali moja kwa moja kwa wahusika .

(g)Payment switch
Mikakati mingine iliyofanywa na bodi na menejimenti mpya kwa katika kipindi hicho ililenga katika kuboresha huduma au biashara zetu kwa mfano sasa hivi mazungumzo yanaendelea kati yetu na TTCL kwa udhamini wa Wizara ya Fedha ili kuona uwezekano wa kutumia payment switch ya TTCL .matumizi ya payment switch hiyo yataenda sambamba  na uanzishwaji wa kampuni tanzu mpya nilizozitaja.
Na kama mnavyojua tumeanzisha mfumo mpya wa kutoa huduma kwa pamoja yaani one stop shoping center ,mfumo ambao utawezesha huduma mbalimbali kupatikana mahali pamoja.Mradi huo umeanza Posta Mpya na unaendelea kuboreshwa.

(h)Mikataba ya kibiashara.
Mikakati mingine mipya ambayo Bodi na Menejimenti imefanya ni kuingia mikataba mipya na taasisi mbali mbali.
Kwa mfano hivi karibuni tumeingia mkataba na ATCL ambapo kampuni hiyo ya ndege itatumia majengo yetu kwa ajili ya kutolea huduma zake na Shirika la Posta litatumia ndege hizo kusafirishaji wa mifuko yake ya barua/vifurushi.

Shirika la Posta liko kwenye mazungumzo na taasisi mbalimbali kwa lengo la kuutumia kikamilifu mtandao wa Posta kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali,ikizingatiwa kuwa Posta iko kila Mkoa kila Wilaya na baadhi ya Tarafa na Vijiji.

(i) Mapitio ya kanuni na sheria za kazi
Shirika linapitia na kuandaa sheria na kanuni mpya za kazi ili ziweze kuendana na maabadiliko ambayo yamekusudiwa ili kujenga mazingira ya kazi yanayofaa kwa wakati wa sasa.

(i)Muonekano mpya wa Shirika
Kwa sasa shirika liko kwenye hatua  za mwisho za  kuboresha muonekano wa ofisi zake  ikiwa ni pamoja na kutambulisha nembo mpya ya Shirika. Lengo lake ikiwa ni kujipanga upya na kuja kivingine.
Pia Shirika kwa kutumia wataalamu wake wa ndani limefanikiwa kuunda mifumo mbalimbali ya TEHAMA.
5. MAWASILIANO YA NDANI.
Nia ya kuwaiteni viongozi wa wafanyakazi ni kuwajulisha yale yanayofanywa na viongozi wenu ili mtakapokutana na wafanyakazi wenzenu muweze kuwajulisha yale yanayofanywa na viongozi wenu kwa niaba yao.

Natambua umuhimu wa mawasiliano katika taasisi yoyote ile, na jinsi yanavyoweza kujenga daraja kati ya Bodi Menejimenti na wafanyakazi wa chini, ndio maana nasisitiza vikao na mikutano ya mara kwa mara ifanyike ili kupeana mrejesho na kupeana taarifa mbalimbali kwa lengo la kujenga umoja na mshikamano.

·         Mawasiliano mazuri husaidia katika kukuza maendeleo ya Shirika kwa ujumla. Kwa wafanyakazi mawasiliano yatakuza utendaji wao wa kazi kwa sababu kutakuwa na uwazi juu ya yanayoendelea na yatarajiwayo kutokea kwa maendeleo ya Shirika.

·         Vilevile kuwepo kwa mawasiliano mazuri katika Shirika kutaongeza nguvu kazi na uwezo wa wafanyakazi katika ngazi zote za Shirika kufanya kazi kwa pamoja kupunguza migogoro na  kufikia malengo ya Shirika.

Mawasiliano ya wazi na ya mara kwa mara kati ya Bodi Menejimenti na wafanyakazi yataondoa au kupunguza minongono na taarifa potofu

Ndugu viongozi wa wafanyakazi.
·         Baada ya kusema haya ninapenda niwashukuru tena kwa kuhudhuria kikao hiki nina imani tutaongeza bidii, tutashirikiana vyema na kwa uwazi kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya katika Shirika letu.

·         Mwisho nakaribisha maoni, maswali au ufafanuzi mnaohitaji kwa ajili ya ustawi wa Shirika letu.Asanteni kwa kuniskiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.