Habari za Punde

Taifa ya Jang'ombe yarejea Zanzibar ikitokea kambini mkoani Tanga


Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Timu ya Taifa ya Jang’ombe wamerejea Visiwani Zanzibar jana jioni wakitokea mkoani Tanga ambapo waliweka kambi ya wiki mbili.

Mara baada ya kuwasili tu Unguja Taifa wakaenda kumjulia hali mdhamini wao mkuu Salim Hassan Turkey huko Mpendae Mjini Unguja.

Turkey ambae pia ni mbunge wa Jimbo la Mpendae amefurahishwa mno kutembelewa na vijana wake ambapo pia amesema wakitwaa ubingwa wa ligi kuu soka ya Zanzibar msimu huu atawafanyia jambo kubwa wachezaji hao.

“Nawapongeza kwa kuja kunijuulia hali, ahsanteni wachezaji wangu, mwaka jana niliahidi mukichukua ubingwa ntakupelekeni China kukaa kambi, lakini kwa bahati mbaya hatukuchukua ubingwa ndo mana tukaenda kambi Tanzania bara, lakini msimu huu ntaangalia mechi mbili kasha ntakupeni ahadi nzito”. Alisema Turkey.

Wakati huo huo kocha mkuu wa Taifa ya Jang’ombe Saleh Mussa Maisara amesema kambi yao ilikuwa nzuri sana na imewasaidia kujijenga vizuri zaidi kwenye ligi kuu ambapo kwasasa kikosi chake kipo tayari kupambana.

“Kambi yetu ilikuwa ni ya wiki mbili, nashkuru tulilolitafuta tumelipata, vijana wapo vizuri sana naamini sasa wapo tayari kupambana”. Alisema Maisara.

Mchezo wake wa kwanza Taifa ya Jang’ombe itacheza dhidi ya Zimamoto mchezo ambao utapigwa Oktoba 5 mwaka huu saa 8:00 za mchana katika uwanja wa Amaan.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.