Habari za Punde

Usafiri Ni Huduma Kama Nyingine Wananchi Daini Tiketi Mnapokuwa Safarini.

Na Agness Moshi- Maelezo Dar es Salaam.
Ni asubuhi   nyingine tulivu iliyopambwa na mwanga wa asili, nami nimekaa kiti cha dirishani kwenye daladala nielekea kwenye majukumu yangu katika ujenzi wa Taifa.  Nazishuhudia pilikapilika za hapa na pale kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam zenye lengo la kuboresha maisha yao na Taifa kwa ujumla.

Nashtushwa na sauti ya mwanamke ambaye sikufanikiwa kumuona kwa sura kutokana na msongamano ikidai tiketi ya dalala “Konda mbona hujanipa tiketi yangu, tukipata ajali si utatukana, naomba tiketi’’, alisema mwanamke huyo.

Si jambo geni kwa abiria wanaotumia daladala kutopewa tiketi hususani wanapofanya safari za ndani ya miji,sikatai zipo daladala zinazotoa tiketi kwa abiria lakini abiria wanakua wakiwashawishi wasafirishaji kuto zitoa kwasababu wanazitupa , na wengine hawajali kama wamepewa au hawajapewa.

Abiria  wengi hufikiri tiketi za daladala ni kwa ajili ya wasafirishaji kujua nani aliyechangia huduma ya usafirishaji na nani hajachangia, jambo ambalo si sahihi  tiketi ina umuhuhimu kwa abiria na  ni haki ya kila abiria .

Kwa mujibu wa kanuni ya 25 ya sheria za SUMATRA ya mwaka 2007, abiria ana haki ya kupewa tiketi ambayo itampa  ufahamu  wa nauli ya safari, kituo aendacho, muda wa kuwasili kituoni  na kuanza safari, namba ya usajili ya gari  hilo, anuani na namba ya simu ya mmiliki wa leseni , pia abiria anahaki ya kupewa tiketi itakayoandikwa jina lake na namba  ya kiti chake na nauli halali iliyoidhinishwa.

Sheria hiyo inawagusa wasafirishaji wa ndani ya miji ikiwa ni pamoja na daladala ambapo mmiliki wa gari anapaswa kutoa tiketi zilizochapishwa ambazo zitaonyesha namba ya usajili wa gari lenye leseni, nauli iliyoidhinishwa, jina na anuani ya mwenye gari au mmiliki wake na tarehe ya kutolewa.

Hivyo basi, abiria wanapaswa kufahamu kuwa tiketi ni haki yao kimsingi na ni muhimu  kwao na kwa wasafirishaji na si kwa wasafirishaji pekee kama ilivyozoeleka.
Kaimu katibu mkuu wa Chama cha kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA) ambaye pia ni Afisa msimamizi mkuu wa chama hicho  mkoani Morogoro Bw. Leonard Mapunda  amesema  kisheria  tiketi ni mkataba wa kibiashara ya usafirishaji Kati ya abiria na mmiliki hivyo ina umuhimu pande zote mbili .

Bw.Mapunda ametaja baadhi ya faida za tiketi kwa abiria ambazo ni pamoja na kumthibitishia abiria kuwa amelipa malipo halali na hawezi kudaiwa mara ya pili,inampa ushahidi wa kudai mzigo endapo atakua kausahau kwenye gari,kupata kidhibiti endapo kanyanyaswa na hata ajali ikitokea inampa ushahidi wa tukio.

“ Tiketi zinakua na namba ya mmiliki  hii pia ni faida kwasababu abiria anaweza akatoa
malalamiko  yake moja kwa moja kwa mmiliki  endapo atakua hajatendewa haki ili mmiliki achukue hatua kwa wafanyakazi wake”, alisema Mapunda.

Aidha, Mapunda amesema ni kosa kwa wamiliki na wasafirishaji kutotoa tiketi kwa abiria endapo msafirishaji atabainika atawajibishwa kwa kanuni  na Sheria zilizowekwa ikiwa ni pamoja na kulipa faini ya shillingi 30,000 kwa Askari wa barabarani lakini kama malalamiko yatapelekwa SUMATRA kwa maandishi  mmiliki atafikishwa mahakamani ambapo atatakiwa kulipa   Tsh. 250,000 kwa kosa moja.

Hata hivyo, Mapunda amesema kuwa chama hicho kina kutana na changamoto mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake hususan katika kutetea abiria kwasababu abiria wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya haki ya tiketi na umuhimu wake hivyo kupelekea kupotezea haki zao.

“Linapotokea tatizo inakua ngumu kumsaidia abiria kwa sababu unakuta abiria hana tiketi ambayo ingetusaidia kuipata gari husika,na hata ukiuliza namba ya gari  unakuta abiria hakuisoma au kasahau hivyo basi ni vyema awe na tiketi ili imuwezeshe kupata haki zake”alisema Mapunda.

Hata hivyo, Mapunda amesema kuwa chama hicho kimefanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha inakuza uelewa kwa abiria kuhusu umuhimu wa tiketi na haki zao kimsingi ikiwa ni pamoja na kusambaza maafisa kwenye vituo vikuu vya daladala,shule za sekondari, kwenye magari ya mikoani, na kwenye vikao vya vijiji au mtaa endapo wamepewa ridhaa  kwa lengo la kutoa elimu kuhusu haki ya tiketi kwa abiria na umuhuhimu wake.

Mapunda ametoa rai kwa abiria kuhakikisha wanapewa tiketi kwenye vyombo vya usafiri bila kujali umbali wa safari kwani ni haki yao na ni msaada wao endapo kutatokea tatizo lolote litakalo hitaji msaadaa wa tiketi.

Kwa makala haya nawasihi abiria wenzangu kuona umuhimu wa kudai na kuchukua tiketi kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanatimiza matakwa ya kisheria lakini pia ni kwaajili ya usalama wao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.