Habari za Punde

Katika kutekeleza agizo la Rais: RC Kaskazini Pemba kula sahani moja na walimu watoro


NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MKUU wa Mkoa wa Mkaskazini Pemba, Omar Khamis Othman amesema, katika kutekeleza agizo la rais wa Zanzibar Dk: Ali Mohamed Shein kuhusiana na walimu watoro, ameanza kwa kupata orodha ya walimu wote wa mkoa wake, ili iwe rahisi wakati atakapofanya ziara za ghafla skulini, kuwatambua.

Akizungumza na Zanzibar leo Ofisini kwake Wete alisema, watahakikisha maagizo yote yaliyotolewa na Rais wanayatekeleza ipasavyo likiwemo hilo la waalimu watoro.
Alisema kuwa, walimu hao atawafuatilia kwa kuwapitia katika skuli zao wanazosomesha bila ya kutoa taarifa, ili kuweza kuwabaini walimu wenye kufanya tabia ya utoro.

“Tutakwenda skuli zote kimya kimya na tukifika tu tunazichukua simu za za walimu waliopo, ili wasije wakawapigia”, alisema Mkuu huyo.

Mkuu huyo alieleza kuwa, watazifuatilia skuli moja baada ya moja na endapo watabaini kuna walimu wenye tabia hiyo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Ikiwa mwalimu ana matatizo basi tupate taarifa yake kamili, lakini kinyume na hivyo tutamchukulia hatua za kisheria”, alieleza.

Aidha alieleza kuwa, pia watahakikisha wanapeleka miundombinu ya maji maskulini, ili kuondosha tatizo hilo lililopo kwa baadhi ya skuli, kwani yote yamo katika mkakati wa kufanyia kazi.

Akizungumzia agizo jengine kwa soko la Tumbe Wilaya ya Micheweni Pemba, Mkuu huyo alisema, soko hilo lipo kwenye matengenezo, ambapo ndani ya miezi miwili litaweza kutumika.

“Sasa hivi wanasubiri huduma ya maji safi na salama, ili waingie ndani ya soko, hivyo tutahakikisha ndani ya miezi miwili wafanyabiashara wetu wataingia ndani ya soko hilo”, alisema Mkuu huyo.


Hayo ni miongoni mwa maagizo aliyoyatoa Raisi wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein katika mkoa huo ili yatekelezwe, ambapo tayari maagizo yote yamo katika mkakati wa kufanyia kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.