Habari za Punde

UVCCM wajitolea kufanya usafi Hospitali ya Wete

NA/ ZUHURA JUMA, PEMBA.

MWENYEKITI wa Baraza la Mji Wete, Asaa Juma Ali, ameshukuru Umoja wa Vijana UVCCM Wilaya ya Wete kwa kujitolea kufanya usafi katika Hospitali ya Wete na kusema kwamba hiyo ni moja katika kutekeleza Ilani ya chama cha Mapinduzi.

Alisema, suala la usafi limeainishwa ndani ya Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020, ambapo uwepo wao hapo ni kutekeleza kwa vitendo ilani hiyo.

Aliyasema hayo wakati walipokuwa akizungumza na Umoja wa vijana UVCCM Wilaya ya Wete, mara baada ya kufanya walipokuwa wakifanya usafi katika Hospitali kuu ya Wete.

“Kwa kweli vijana wetu hawa wamefanya jambo la busara na kubwa kwa kuamua kuja kufanya usafi katika hospitali yetu, tunawashukuru sana” alisema Mwenyekiti huyo.

Alieleza kuwa, Baraza la Mji Wete limekuwa likifanya usafi wa mji kwa kila wiki katika maeneo mbali mbali, ili kuhakikisha mji unakuwa katika hali ya usafi, hivyo juhudi za vijana hao zimesaidia kiasi kikubwa kwa kuweza kufanya usafi katika Hospitali ya Wete.

Kwa upande wake Katibu wa vijana UVCCM Wilaya ya Wete, Khatib Jabir, alisema  Umoja wa vijana umejitolea kufanya usafi katika Hospitali kuu ya Wete, kwani ni wajibu wao kama vijana kuhakikisha kwamba afya za wananchi zinaimarika siku hadi siku.

“Usafi ni muhimu kwa kila mtu, hivyo vijana tumeamua kujitolea kwa kufanya usafi, ili tuwe vijana wazuri katika Taifa la leo”, alisema Katibu huyo.

Nae, Mwenyekiti wa Vijana UVCCM Wilaya ya Wete Ibrahim Mustafa alieleza kuwa, lengo la kwenda kufanya usafi katika Hospitali hiyo ni kuhakikisha kwamba hospitali inakuwa safi mda wote, ili kuweza kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Akizungumza kwa niaba ya Daktari dhamana Hospitali ya Wete, daktari Muuguzi wa Hospitali hiyo, Ali Haji aliwashukuru vijana hao kwa moyo wao mzuri waliouonesha katika kujitolea kufanya usafi na kusema kwamba wameonesha uzalendo  wa nchi yao.

“Tunashukuru sana kwa kutusaidia kufanya usafi, mungu awalipe, kwani mumefanya jambo kubwa sana, kwa kweli ni faraja kwetu na jamii kwa ujumla”, alishukuru daktari huyo.


Umoja wa Vijana UVCCM Wilaya ya Wete, wamefanya usafi katika Hospitali ya Wete, wakiwa na lengo la kuhakikisha Hospitali hiyo inakuwa katika hali ya usafi na kuridhisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.