Habari za Punde

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA UMOJA WA MATAIFA

Na. Mwandishi OMR.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan  leo ameshiriki maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa ambapo Umoja huo umetimiza miaka 72.

Akihutubia katika hafla hiyo, Makamu wa Rais alisema Tanzania imekuwa ikifanya vizuri tangu ijiunge na Umoja wa Mataifa mwanzoni mwa miaka ya sitini na kufaidika na mambo mengi sana ya Umoja wa huo ikiwemo miradi mbali mbali ya maendeleo na misaada ya kujenga majopo ya wataalamu.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa ni Watu na lazima faida za Umoja wa Mataifa ziwaguse watu na ndio maana Umoja wa Mataifa pia umendelea kuibua na kusimamia miradi mbalimbali vijijini inayowahusu watu na mazingira yao.

Akizungumzia Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ambayo ni Maendeleo ya Viwanda na Utunzaji wa Mazingira kwa Maendeleo Endelevu, Makamu wa Rais alisema imekuja wakati muafaka kwa kuwa Tanzania iko katika muelekeo wa kubadilisha uchumi wake kuwa wa viwanda na wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, “Kwa nchi ambayo zaidi ya asilimia 75 ya watu wake hutegemea kilimo na ambayo asilimia 33 ya mavuno yake huharibika haiwezi kufanikiwa bila kuwa na msingi mzuri wa viwanda” alisisitiza Makamu wa Rais.

Tanzania haiwezi kupuuza umuhimu wa kuendeleza viwanda kwa uchumi wake kwani ni sekta ambayo imeendelea kukua katika kuchangia uchumi na pato la Taifa kila Mwaka.

Makamu wa Rais alisema Serikali inafahamu hofu iliyopo juu ya uendelezwaji wa viwanda na uharibifu wa mazingira kama ilivyokuwa katika kipindi cha Mapinduzi ya Viwanda Ulaya na Marekani katika karne ya 18 na 19 hata hivyo alisisitiza kwamba hofu hiyo haina nafasi tena kutokana na kukua na kuendendela kwa teknolojia na ugunduzi wa kisayansi.

Kuhusu Masuala ya Amani na Usalama, Makamu wa Rais alisema Tanzania imendelea kujihusisha bila kuchoka katika utatuzi na ufumbuzi wa migogoro katika sehemu mbali mbali duniani kama njia ya kuhakikisha inatekeleza wajibu wake kwa Umoja wa Mataifa wa kudumisha na  kuendeleza amani na usalama Kikanda na Kimataifa.

Mwisho Makamu wa Rais alisema Tanzania inaunga mkono jitihada za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa za kufanya mabadiliko katika Umoja huo.Hata hivyo alisema ipo haja ya kuwa na mkakati madhubuti wa kufanya mabadiliko hayo.

Wakati huohuo, Makamu wa Rais amehudhuria ufunguzi wa Mkutano wa Dunia wa Wanawake kuhusu masuala ya Benki uliofanyika katika Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo Makamu wa Rais alisema masuala ya uwezeshaji wanawake kiuchumi hususani ujumuishwaji katika sekta ya kifedha imekuwa ajenda yake kuu.

Aliendelea kusema mkutano huu umekuja wakati muafaka ambapo pamoja na jitihada kubwa za wadau mbali mbali duniani kuongoza na kupigania ujenda ya ujumuishwaji katika masuala ya kifedha ili kupunguza umasikini bado matokeo ni madogo kwa wanawake  waliopo katika sekta zisizo rasmi na maeneo vijijini.

Takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia 50 tu ya wanawake wenye umri wa kufanya kazi ndio wanaofanya kazi ikilinganishwa na asilimia 77 ya wanaume, pia ipo tofauti kubwa ya kipato baina ya wanawake na wanaume ambapo kwa wanawake kipato chao ni asilimia 24 tu kulinganisha kile cha wanaume na asilimia 42 ya wanawake na wasichana duniani wapo nje ya mfumo maalumu wa kifedha.

Pamoja na kutambua kwamba Tanzania inaongoza katika matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya mtandao, Makamu wa Rais aliwaasa washiriki na kuwataka kuangalia namna bora ya kuepeleka huduma za kifedha kwa wanawake waliopo nje ya mfumo maalum wa ajira na waliopo vijijini. Alizitaka benki zilizopo nchini kufungua matawi mengi zaidi vijijini ilikuwezesha wanawake wengi kuingia katika mfumo rasmi wa sekta ya fedha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.