Na.Haji Nassor - Pemba.
WADAU wa haki za binadamu kisiwani
Pemba, wamesema tuhuma za rushwa zinazoelekezwa kwenye vyombo vya kisheria kama
vile Polisi na mahakama, isiwe sababu kwa jamii, wanapovunjiwa haki zao za
binadamu, kutovitumia vyombo hivyo kudai haki zao.
Walisema sio
kweli kuwa, vyombo hivyo vinanuka rushwa na havifai kufungua mashitaka, iwapo
kuna mtu au kundi la watu limevunjiwa haki zao, na badala yake wasisite
kuvitumia, maana wapo wanaoshinda na kupata haki zao.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, wadau hao walisema jeshi la
Polisi, Mahakama, Ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka, taasisi kama ZAECA na ZLSC
vipo kwa ajili yao.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa kusini Pemba, Shehah Mohamed Shehan, alisema hata iweje lazima
wananchi walitumie jeshi la Polisi, pale wanapovunjiwa haki zao za binadamu,
hata kama wafanyaji ni Polisi.
Alisema,
kujitokeza kwa mtendaji mmoja wa jeshi hilo, kudaiwa kuchukua rushwa au kufanya
jambo ovu, isiwe sababu kwa jamii kulikataa jeshi lote, wakati wanapovunjiwa
haki zao kwenye shughuli zao za kila siku.
“Jamii isikae
majumbani wanapobaini kuwa wamevunjiwa haki zao za binadamu, kwa dhana potofu
walizonazo kuwa, hata ukipeleka kesi, basi itaambatanisha wa rushwa”,alisema.
Hata hivyo
alisema, upo uhusiano wa karibu baina ya rushwa na utekelezaji wa sheria kwenye
kesi za uvunjifu wa haki za binadamu, ambapo wakati mwengine, husababishwa na
jamii husika.
Nae
Mwanasheria dhamana wa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Pemba, Ali Rajab Ali
alisema, uwepo wa rushwa kwenye vyombo vya kutoa uamuzi, unaathiri upatikanaji
wa haki hasa kwa maskini.
Mwanasheria
huyo, alisema uwepo wa tuhuma hizo, haina mantiki kwa jamii, kwamba wasivitumie
vyombo hivyo, wakati wanapoona wamevunjiwa haki zao za binadamu.
“Kama kuna
Mwendesha mashitaka, Polisi au hakimu mmoja anatuhumiwa kwa rushwa, haina maana
kwamba, sasa jamii iache kuvitumia vyombo hivyo, maana wachukua rushwa sio
wote”,alisema.
Katika hatua
nyengine Mwanasheria huyo, alisema zipo ksei kadhaa ambazo mtu mmoja, amemshitaki
mtendaji wa vyombo vya sheria, ishara inayonyesha hakuna alie juu ya sheria.
Kwa upande
wake, Mdhamini wa Mamlaka ya Kuzuia rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar ZAECA
afisi ya Pemba, Suleiman Ame Juma, alisema jamii isiwe na wasiwasi wa kuviogopa
vyomba vya kisheria, maana wamekuwa wakipokea malalamiko yao, pindi
wakijihusisha na rushwa bila ya kujali vyeo vyao.
Alisema zipo
kesi za viongozi wakuu, kwenye sekta na taasisi hizo za vyombo vya sheria,
wakiwashikilia kutokana na tuhuma za rushwa, jambo ambalo kila kundi linaweza
kutazamwa.
“Jamii iondoe
shaka kuwa, hata Polisi, hakimu, mwanasheria mwengine akionekana na rushwa
ataachiwa, hakuna bali nae sheria itamuandama kama walivyo wengine”,alisema.
Afisa
Mipango wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, Mohamed
Hassan Ali, amesema haki za bindamu, zimeshaundiwa taasisi kama wizara husika,
ili wanaovunjiwa wawe na pahala pakukimbilia.
Alisema hata
mfano wa Kituo chao, kimekuwa kikitumiwa na wananchi waliowengi, pale
wanapohisi wamevunjiwa haki zao za binadamu, hata ikiwa wavunjaji wakuu ni wale
wanaofanyaka kazi kwenye vyombo vya kisheria.
“Sisi ZLSC
tumeshapokea hata malalamiko ya Polisi au mahakimu, wakituhumiwa kwa rushwa, na
malalamiko hayo kuyafanyia kazi, hivyo jamiii isisite kututumia wakiona
wanafanyiwa ndivyo sivyo”,alisema.
Mapema
Meneja miradi kutoka Jumuia kwa ajili watu wenye ulemavu wa akili Zanzibar,
ofisi ya Pemba, Ali Mwadini Haji, alisema, bado kundi analoliongoza limekuwa na
hofu kubwa kushinda kesi zao, kwa hofu ya kuingiliwa na rushwa.
Alisema
asili hasa ya wazazi, walezi na watu wenye ulemavu wa akili wenyewe, wamekuwa
wogo kutetea haki zao, kutokana na utamadani mkubwa uliopo, wa rushwa kwenye kesi
za uvunjifu wa haki za bindamu.
“Mtu mwenye
ulemavu, bado anaona ni sawa anapovunjiwa haki zake kubaki nyumbani, maana
anawasiwasi wa kuzingiliwa na rushwa, anapokwenda kwenye vyombo vya
kisheria”,alisema.
Msaidizi wa
sheria jimbo la Chakechake Riziki Hamad Faki, alisema yapo mahusinao ya karibu
katika upatikanaji wa haki za mashauri ya uvunjifu wa haki za binadamu, na
rushwa.
Baadhi ya
wananchi kisiwani Pemba, walisema bado ipo haja kwa vyombo vya kisheria,
kuendelea kujisafisha ili jamii iwatazame katika jicho la utawala bora.
Haji Makame
Omar wa Wawi, alisema jamii haijaona kuwa ndani ya vyombo vya kutoa haki, kama
Polisi na Mahakama, mtu anaweza kushinda kesi bila ya kutumia rushwa.
“Ndio maana
wapo baadhi hata wanapovunjiwa haki zao za binadamu, hushindwa kuvifikia vyombo
vya kisheria, na ndio maana hupenda kumaliziana kienyeji”,alisema.
Hidaya Said
Omar wa Kengeja, alisema anachoamini yeye kuwa, vyombo vya kisheria,
vitaendelea kuwa ni mali ya wakubwa, watu maarufu na wenye nacho, na sio vyombo
vya kila mmoja kama sheria zinavyoelekeza.
Mrajisi
jimbo mahakama kuu Pemba, Huseein Makame Hussein alisema, sio sahihi
kuvitafsiri vyombo kama vya mahakama kuwa, vinachukua rushwa bali hizo ni dhana
zilizopo zisizo na ushahidi.
Alisema
mahakamani baada ya kupokea kesi, husikilizwa na lazima mwisho wake mmoja wapo ashindwe
na mmoja ashinde, hivyo upande usioridhika, hushutuma uwepo wa rushwa
mahakamani.
Hata hivyo
wadau hao, wameiomba jamii kuendelea kuvitumia vyombo vya sheria, wanapokumbana
na moja ya uvunjifu wa haki za binadamu, na kuacha tabia ya kujichukulia sheria
mikononi.
Tayari tokea
kuanza kwa mwaka huu wa 2017, watu watatu wameshauwawa na watu wanaodaiwa kuwa
na hasira, ndani ya mkoa wa kusini Pemba pekee.
No comments:
Post a Comment