Habari za Punde

Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania akutana na Makamu wa Pili wa Rais , Balozi Seif

Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq  wa kwanza kutoka Kushoto  aliyefika Zanzibar kujitambulisha rasmi wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyekaa kati kati Ofisi Vuga Mjini Zanzibar.

Wa kwanza kutoka Kulia ni Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Hamood Al – Habsi akifuatiwa na Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akimzawadia Mlango Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq kama ishara ya kufungulia Milango ya uwepo wake Nchini Tanzania.
 Balozi Seif  wa Pili Kutoka Kulia akiwa katika Picha ya pamoja na Mabalozi wa Oman wanaofanya kazi Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania na Visiwa vya Zanzibar.

Kulia ya Balozi Seif ni Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq na Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga.

Kushoto ya Balozi Seif ni Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Hamood Al – Habsi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiagana na Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.Picha na – OMPR –ZNZ.
Na. Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar na Oman zitaendelea kufanya kazi pamoja  katika dhana nzima ya kudumisha ushirikiano wa Damu uliopo wa muda mrefu kwa maslahi ya maendeleo ya Kiuchumi na ustawi wa jamii wa Wananchi wa Mataifa hayo mawili.
Alisema Ushirikiano huo umeimarika zaidi kwa Zanzibar  kupokea ufadhili wa Vijana wake wanaopata fursa za kujiunga na Masomo ya juu Nchini Oman katika fani mbali mbali za mafunzo ikiwemo Udaktari, Uhandisi, Kompyuta pamoja na Lugha.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq  aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi akiambatana pia na Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Hamood Al - Habsi.
Alisema Zanzibar inafurahia kuendelea kuwepo kwa uhusiano huo wa kipekee na wa kupigiwa mfano ambao umekuwa ukileta faraja na matunda mazuri yanayotowa fursa zaidi kwa Zanzibar kutanua wigo wa Kimaendeleo na kuongeza maeneo mengine ya ushirikiano wa Kisiasa, Kiuchumi na Kiutamaduni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi  Ali Abdulla – Al Mahrouq  kwamba uungaji  mkono wa Oman kwa Zanzibar hasa katika utanuzi wa Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni umeleta faraja kwa Wananchi walio wengi kwenye huduma za Afya zinazotarajiwa kuenea katika masafa yasiyozidi Kilomita Tano.
Balozi Seif aliipongeza  Serikali ya Oman kwa msaada wake mkubwa  inayoendelea kutoa kwa Zanzibar hasa kwa kukubali kugharamia matengenezo makubwa ya Majengo ya Kihistoria ya Beit el ajab na Jumba la Makumbusho ya Kifalme yaliyopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Alisema msaada huo wa Majengo hayo muhimu umekuja wakati muwafaka kwa vile utasaidia kuhifadhi Historia ya Kiutamaduni na Kiutawala  ya Visiwa vya Zanzibar inayohusisha pia mafungamano  ya Majengo hayo na Oman.
Akigusia ujio wa Meli ya Kifalme ya Fulk Al Salamah kutoka Nchini Oman Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alieleza wazi kwamba Zanzibar imepata faraja  kubwa ya ziara ya Ujumbe wa Serikali ya Oman uliowasili Zanzibar na Meli hiyo ya Kifahari.
 Alisema Wananchi wa Zanzibar wamepata kujifunza mambo mbali mbali kufuatia ujio wa Meli hiyo kwa kupata taaluma ya kuepuka masuala mazima yanayotokana na Sekta ya mafuta ambayo kwa sasa Visiwa vya Zanzibar vimo katika matayarisho ya awali ya kuendesha Miradi inayotokana na Sekta hiyo.
Akigusia suala la Majanga Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  ameishukuru Serikali ya Oman kwa msaada wake wa kuwawezesha Viongozi Wanne Waandamizi wa Zanzibar kupata fursa ya kujifunza  mbinu na Taaluma ya jinsi ya kujikinga na Majanga.
Balozi Seif alisema mafunzo hayo yameleta faida kubwa kiasi kwamba Oman ingefikiria tena kutoa nafasi nyengine kama hizo kwa watendaji wengine wa Taasisi za Majanga Zanzibar  kupata fursa kama hizo katika kipindi chengine kijacho.
Mapema Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania  Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq  alisema udugu uliopo wa Viongozi  pamoja na hata Wananchi wa kawaida wa Oman na Zanzibar  ni vyema ukaongezeka zaidi katika uhusiano wa masuala ya Kibiashara.
Balozi Al – Mahrouq  alisema pande hizo mbili zimekuwa na historia ndefu ya Kiutamaduni na Kisiasa kiasi kwamba kwa sasa nguvu zikaongezwa katika uimarishaji zaidi wa Kibiashara jambo ambalo linaweza kustawisha kuongeza ukaribu  wa Wananchi wa pande hizo mbili  unaoweza kudumu milele.
Balozi huyo wa Oman Nchini Tanzania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Serikali ya Oman itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha harakati za Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Wananchi wa Zanzibar unazidi kukua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.