Habari za Punde

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Mary Mwanajelwa Asema Mpango wa Serikali Kupeleka Mbegu Mpya za Kahawa Wilayani Mbinga ni Kuinua Uzalishaji wa Zao Hilo.

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa (Mb) akijibu maswali Bungeni Mjini Dodoma Leo Novemba 10, 2017.
 Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa (Mb) akijadili jambo na Mhe Jenista Joakim Mhagama ambaye ni Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu
 
Na Mathias Canal, Dodoma
Serikali imesema kuwa Mpango wa Serikali wa kuwapelekea wakulima wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma mbegu mpya za Kahawa ni mahususi kwa ajili ya kuinua uzalishaji kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Kuendeleza Zao la Kahawa katika kipindi cha miaka 10 yaani mwaka (2011 – 2021).

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa (Mb) amebainisha hayo leo Novemba 10, 2017 Bungeni Mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mhe Martin Mtonda Msuha (Mb) Aliyetaka kufahamu kuhusu kushuka Kwa takwimu katika miaka ya hivi karibuni ya  uzalishaji wa Kahawa Wilayani Mbinga kwa mkulima mmoja mmoja (out growers) ambapo alitaja sababu za mojawapo zilizopelekea kushuka kwa uzalishaji huo kuwa ni pamoja na kuzeeka kwa miti ya kahawa.
Mhe Mwanjelwa alisema kuwa Katika mpango huo, utafiti na usambazaji wa miche bora itatolewa ili kuondokana na miche yenye tija duni na iliyozeeka. Ambapo Utekelezaji wake unafanyika kwa kushirikiana na wadau hususani Tanzania Coffee Research Institute (TaCRI).

Alisema, Kituo cha Utafiti na uzalishaji miche cha Ugano kilichopo Wilayani Mbinga, katika mwaka 2016/2017 kilizalisha na kusambaza miche bora ya kahawa 270,869 na kazi mpaka hivi sasa inaendelea.

Aidha, Mfuko wa Maendeleo ya Kahawa (Tanzania Coffee Developemnt Fund (TCDF) umefadhili na kupunguza bei kutoka shilingi 300 kwa mche mmoja hadi shilingi 150 kwa vituo vyote nchini vilivyoko chini ya TaCRI ili miche hiyo isambae kwa kasi.

Mhe Mwanjelwa alisema mnada wa kahawa huendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Kahawa Na. 23 ya Mwaka 2001 hivyo Serikali haina mpango wa kuanzisha soko la mnada wa kahawa Wilayani Mbinga au mahali pengine nchini kwa sababu uwepo wa miundombinu ya mashine ya kielektroniki ya kuendeshea mnada iliyopo Moshi, maabara ya kuonjea kahawa, wataalamu wa kuendesha mnada huo, gharama za mnunuzi ambapo atalazimika kwenda katika kila mnada kama utawekwa kila mahali ambapo kahawa inazalishwa.

Alisema uzoefu unaonyesha kuwa nchi nyingi duniani huweka mnada sehemu moja tu ili kurahisisha uendeshaji. Aidha, tangu kuanzishwa kwake kabla uhuru, mnada uliwekwa Moshi kwa kuwa ndiko kulikuwa na wanunuzi na biashara ukilinganisha na maeneo kama Kagera ingawa uzalishaji unafikia hadi asilimia 40 ya nchi nzima.

“Mnada unauza kahawa ikiwa kwenye maeneo ya uzalishaji (Ex-Mbinga, Ex-Mbeya n.k.) kinachopelekwa Moshi ni sampuli tu kwa ajili ya uonjaji. Aidha, Serikali imeanzisha Soko la Bidhaa (Commodity Exchange) ili kupunguza gharama za uendeshaji wa masoko ya mazao ikiwemo kahawa” Alikaririwa Mhe Mwanjelwa

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa kifungu Na. 29 (ii) cha Kanuni za kahawa 2013, ni kosa kwa mtu yeyote kununua matunda ya kahawa (ripe cherry) hivyo Serikali inakataza biashara ya kahawa mbichi. 

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbinga na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma sambamba na wahusika wengineo wote kwamba hairuhusiwi kabisa uuzaji wa kahawa mbichi.

MWISHO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.