Mshauri wa Rais katika masuala ya Mazingira
na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya
Tabianchi (AGN) Dkt. Richard Muyungi akizungumza na Watanzania wanaoshiriki Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa kuhusu Mabadiliko
ya Tabianchi (COP 30) unaoendelea katika Jiji la Belem nchini Brazil.
Tanzania
ni miongoni mwa nchi zinazotarajia kunufaika na fedha kiasi cha hadi dola
milioni 20 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi kupitia Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu.
Hayo
yamesemwa na Mshauri wa
Rais katika masuala ya Mazingira na Mwenyekiti wa
Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) Dkt. Richard
Muyungi alipokutana na Watanzania wanaoshiriki Mkutano
wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30)
unaoendelea katika Jiji la Belem nchini Brazil.
Dkt.
Muyungi amesema kuwa katika utekelezaji huo tayari zimetengwa fedha kiasi cha
dola milioni 250 kwa mwaka ujao kwa kwa ajili ya kufadhili miradi hiyo ambayo
Tanzania ni nchi mnufaika.
“Nasisitiza
huu sio mkopo bali ni ufadhili na hadi sasa tuna mambo ya kufuatilia na sisi
kama nchi tumepewa kipaumebele hivyo tunaweza kuwa na miradi hata miwili ambayo
inaweza kuwa na manufaa makubwa, naomba Ofisi ya Makamu wa Rais tuteua mtu
mmoja yaani focal person kwa ajili ya
Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu,” amesema.
Kubwa
zaidi amebainisha kuwa mwaka 2025 Tanzania imeteuliwa kuwa Kituo cha Santiago ambacho
kitakuwa kinaratibu msaada wa kiufundi kwa nchi zinazoathiriwa na hasara na
uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha,
Dkt. Muyungi ameomba Watanzania kutoka serikalini na sekta binafsi wanaoshiriki
mkutano huo wenye takriban washriki 60,000 kusimama kama nchi na kujenga
mitandao ya kuchangamkia fursa ili kuendelea kuinufaisha nchi.
“Kama
tunavyoona hapa COP 30 yapo mabanda mengi yenye wingi wa washiriki nawaomba
tutumie fursa hii kutengeneza network, tuna
timu ya negotiation tufuatilie fursa za
benki , NGOs na Serikali ili tukitoka hapa tutoke na faida,” amesisitiza.
Vilevile,
Dkt. Muyungi alitumia nafasi hiyo kuwaeleza washiriki hao kuwa wana jukumu la kuitangaza
Dira ya Maendeleo 2025 na Serikali ya Tanzania imetekeleza mambo gani ya msingi
kwa wananchi na hivyo kuchagiza upatikanaji wa fursa zaidi kwa maendeleo endelevu
Kwa
upande wake Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter
Msoffe amesema kuwa Ofisi hiyo imejipanga kuhakikisha kila fursa inayotokea inafanyiwa
kazi.
Prof.
Msoffe ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kutafuta fursa na kuomba ushauri wa
kitaalamu kutoka kwa wataalamu kulingana na aina ya fursa wanayokutana nayo.
“Ndugu
zangu kama alivyozungumza Mwenyekiti (Dkt. Muyungi) tutafute fursa na kama
itakuwa inahusu benki basi unaweza kuzishirikisha benki husika na kama utaona
fursa kuhusu biashara ya kaboni usisite kuishirikisha Ofisi ya Makamu wa Rais,”
amesema.
Naye
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Amina Khamis Shaaban ameomba ushirikiano
kwa wote wanaokutana na fursa lengo ni kusukuma mbele maendeleo ya nchi.
Bi. Amina amesema kuwa Wizara hiyo iko tayari kukutana na wadau wote wa miradi ambayo inakuwa tayari imetayarishwa na kupata idhini huku akisisitiza yote haya yanafanyika ili kuendelea kuifanya nchi iendelee kunufaika.
Sehemu ya Washiriki na viongozi kutoka Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja ya kwenye banda la maonesho la Tanzania kwenye Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) unaoendelea katika Jiji la Belem nchini Brazil Novemba 14, 2025.


No comments:
Post a Comment