STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
14.11.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa utekelezaji wa hati ya makubaliano
(MoU) kati ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Teknolojia
(VIT) cha nchini India ni muendelezo wa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria
uliopo kati ya Zanzibar na India.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo Ikulu Mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Teknolojia (VIT) cha nchini India
Dk. Govindasamy Viswanathan akiwa na
wenyeji wake uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA),
ukiongozwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Idris Ahmada Rai.
Katika maelezo yake Dk. Shein alitoa pongezi kwa
uongozi wa Chuo Kikuu cha (VIT) kwa kufika Zanzibar kwa lengo la kuimarisha
uhusiano na ushirikiano kati ya chuo hicho na chuo Kikuu cha (SUZA), hatua
ambayo inazidi kujenga udugu na uhisiano kati ya Zanzibar na India.
Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar ina mambo ya
kujifunza kutoka India hasa katika
masuala ya Teknolojia ya kisasa ambayo nchi hiyo imeweza kupiga hatua na
kupata mafanikio makubwa.
Aliongeza kuwa licha ya chuo Kikuu cha SUZA kuwa
kichanga lakini kimeweza kupiga hatua kubwa na kupata mafanikio, hivyo
kuendeleza uhisnao na vyuo vikuu ulimwenguni kikiwemo chuo Kikuu cha VIT
kutakisaidia chuo hicho kupanua wigo wa maendeleo sambamba na kujenga uwezo wa
wafanyakazi kitaaluma.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inathamini ushirikiano wan chi rafiki hivyo hatua ya chuo
hicho kusaini hati ya mashirikiano kati yake na chuo kikuu cha SUZA kinaipa
Serikali kuendelea kutilia mkazo suala hilo pamoja na kuendelea kutekeleza azma
yake ya kuimarisha sekta ya elimu hapa nchini.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Mkuu huo wa
Chuo Kikuu cha VIT alieongozana na Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa wa chuo
hicho Dk. C. VijayKumar kuwa azma na malengo ya nchi zote za Jumuiya ya Umoja
wa Afrika (AU) ikiwemo Tanzania ni kuimarisha sekta ya viwanda.
Hivyo, alisisitiza kuwa hatua ya ushirikiano huo
utaimarisha zaidi uanzishwaji wa vituo vya ubunifu na ujasiriamali kupitia Teknolojia
ya kisasa na hatimae kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutekeleza
azma ya kuanzisha viwanda vikiwemo vidogo vidogo na vya kati kutokana na
rasilimali zake zilizopo.
Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi
kikubwa kuongeza soko la ajira kwa wananchi wa Zanzibar huku akisisitiza haja
ya kutilia mkazo suala zima la utafiti kwa chuo kikuu cha (SUZA) jambo ambalo
limo katika hati ya makubaliano (MoU) ya vyuo vikuu hivyo.
Kuhusu utafiti wa bahari Dk. Shein alieleza haja
ya kuendeleza utafiti wa bahari ili Zanzibar iweze kufaidika na bahari hasa
ikizingatiwa kuwa maeneo yake yote ya visiwa vya Zanzibar yamezungukwa na
bahari.
Nae Mkuu wa chuo Kikuu cha (VIT), Dk. Govindasamy
Viswanathan alimueleza Dk. Shein kuwa chuo chake kimekusudia kuimarisha
uhusiano na mashirikiano zaidi na Chuo Kikuu cha (SUZA) kwa kwa manufaa ya
pande zote mbili.
Alieleza kuwa Chuo chake kiko tayari kuyatekekeza
yale yote yaliotiwa saini katika hati ya mashirikiano na kusisitiza kuwa tokea
kuanzisha mashirikiano yao mwaka 2013 kumekuwa na mafanikio makubwa.
Alieleza kuwa Chuo cha (VIT) ni miongoni mwa vyuo
maarufu sana nchini India na kwa upande wa vyuo binafsi ni chuo kinachoongoza
nchini humo ambacho kimeweza kupata mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi hiyo
hasa katika masuala ya Teknolojia ya kisasa.
Mapema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar (SUZA) Profesa Idris Rai alimueleza Dk. Shein kuwa mnamo mwaka 2013
vyuo hivyo vilisaini hati ya makubaliano (MoU) na kukubaliana kushirikiana
katika maeneo ya kadhaa yakiwemo kubadilishajna wafanyakazi, kubadilishana
wanafunzi na kufanya tafiti za pamoja.
Aidha, alieleza mashirikiano mazuri na mahusiano
yaliopo kati ya Chuo Kikuu cha (SUZA) na chuo cha (VIT) huku akieleza matumaini
makubwa wanayotarajia katika mahusiano hayo hasa ikizingatiwa kuwa chuo hicho
kimepiga hatua kubwa katika masuala ya Teknolojia.
Aliongeza kuwa mpaka hivi sasa tayari (SUZA)
imeshasomesha walimu wa TEHAMA wawili katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na
mmoja anaendelea na masomo na wamekwua wakipata mashirikiano mazuri na chuo cha
(VIT) katika mafunzo hayo.
Alieleza kuwa moja ya dhamira za ziara ya Mkuu
huyo wa Chuo Kikuu cha (VIT) ni kuweka saini nyongeza ya Hati ya Makubaliano
(MoU), itayowezesha kuanza kwa masomo ya TEHAMA mwaka ujao pamoja na dhamira ya
kufanya mazungumzo juu ya uanzishwaji wa kituo cha Ubunifu na Ujasiriamali
kupitia (TEHAMA) zoezi ambalo lilifanyika hapo jana.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment