Habari za Punde

TFC YAANZA KUKUSANYA TAARIFA ZA WANACHAMA WAKE WA USHIRIKA KUBORESHA KANZIDATA

Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwantwinza Mwimbe.
Na Daniel Mbega
SHIRIKISHO la Vyama  vya Ushirika Tanzania (TFC) limeanza zoezi la kukusanya taarifa na kuhakiki wanachama ili kuimrisha kanzidata yake.
Akizungumza na MaendeleoVijijini, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwantwinza Mwimbe, amesema zoezi hilo litarahisisha utendaji wa shirikisho katika kuwafikia wanachama wake pamoja na kujua changamoto na vipaumbele ili kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi.

“Tunahitaji tupate idadi halisi ya wanachama wetu kwa sababu tunaamini kwa sasa wameongezeka na hiyo itatusaidia kuweza kuwafikia kwa urahisi tukitambua kila mwanachama anajishughulisha na nini, na nini changamoto zake pamoja na vipaumbele,” alisema Mwimbe.
Mwimbe amesema kwamba, jukumu la TFC ni kusimamia vyama vya ushirika, lakini katika wakati huu ambao taifa linahitaji kujenga uchumi wake na kuongeza kipato cha kila Mtanzania ili kufikia uchumi wa kati, ni vyema kutambua na kufuatilia kwa karibu shughuli zinazofanywa na wanachama hao.
Amesema asilimia zaidi ya 80 ya wanachama wao wanajihusisha na shughuli za kilimo ambapo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za ukame, pembejeo pamoja na masoko, hivyo kwa kuimaridha kanzidata yao watakuwa na uwezo wa kutambua fursa na changamoto zilizopo katika maeneo yote.
“Lazima tuweke kumbukumbu sahihi, kwa sababu hii itasaidia, kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo, kutafuta changamoto za wakulima pamoja na kuwatafutia fursa, hasa za pembejeo na masoko.
“Kwa kuwa tutakuwa na mawasiliano yote ya wanachama, tunakusudia kuwaunganisha na masoko ya ndani na yale ya nje kupitia simu za mkononi,” amesema Mwimbe.
Aidha, amesema kwamba, kwa kuimarisha kumbukumbu hizo itawasaidia hata wao TFC kutambua makisio ya uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa msimu.
“Kumbukumbu hizi ni muhimu, tunaweza kuwa tunajua kwamba kwa msimu huu, mathalan tumbaku limelimwa katika eneo lenye ukubwa gani na makisio ya mavuno ni kiasi gani, vivyo hivyo kwa mazao mengine kama kahawa, pamba, mahindi, mbaazi, ufuta, korosho na mengineyo.
“Kama tukipata taarifa kutoka nje kwamba kuna watu au kampuni inahitaji tani kadhaa za pamba ni rahisi kuwaunganisha wananchama wetu moja kwa moja na kampuni hizo na wakauza kwa uhakika zaidi,” amesema.

Kuhusu TFC
TFC ndiye mrithi wa uliokuwa Muungano wa Vyama vya Ushirika Tanzania (CUT) na ilibadilishwa kufuatia sera mpya na kuanzishwa kwa Sheria mpya ya Ushirika ya mwaka 2003 ambayo ilikuwa mbadala wa Sheria ya Ushirika ya mwaka 1991 iliyokuwa inaeleza kwamba vyama vya ushirika vilikuwa kama sehemu ya vikundi vya kisiasa vya chama tawala.
Kwahiyo, Sheria mpya ya Ushirika ya mwaka 2003 inaelezea tu usimamizi wa vyama vya ushirika na wanachama wanastahili kuwa na sauti na ushiriki wa moja kwa moja.
TFC ni chombo kinachojitegemea kisichofungamana na upande wowote kikiwa kinamilikiwa na wanachama wenyewe katika mukhtadha wa kufuata sheria na kanuni za kimataifa za ushirika.
 Kwahiyo, TFC ni mwanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Ushirika (International Co-operative Alliance - ICA), Shirikisho la Wakulima Afrika Mashariki (East African Farmers Federation - EAFF), Shirikisho la Kimataifa la Wazalishaji Bidhaa za Kilimo (International Federation of Agricultural Producers - IFAP) na Committee of Artisanal and Workers Cooperatives (CICOPA).
Kitaifa, TFC ni mwanachama mwanzilishi wa Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) na Baraza la Kilimo Tanzania (Agricultural Council Tanzania - ACT), zamani likijulikana kama Tanzania Chamber of Agriculture and Livestock.
TFC inashirikiana na wadau kadhaa wa kitaifa na kimataifa kama wizara za Seriali, Shirika la Kazi Duniani (ILO), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Muungano wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), na kadhalika.

Wanachama wa TFC
TFC ilisajiliwa rasmi Desemba 8, 1994 ikiwa na Hati ya Usajili Namba 5503 ambapo wanachama waanzilishi walikuwa 13 tu.

Pamoja na kwamba hivi sasa wanakusanya na kuhakiki taarifa kwa ajili ya kanzidata, MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, hadi kufikia mwaka 2015 TFC ilikuwa na vyama wanachama 3,339 Tanzania Bara vyenye wanachama mmoja mmoja zaidi ya milioni 1.5.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.